Fanya haya kudhibiti maumivu ya shingo

Friday January 18 2019

 

By Dk Shita Samwel

Unapokuwa na maumivu ya shingo Siyo mbaya kufanya usingaji (Massage) au kuchua kwa kutumia mafuta maalumu au kutumia dawa za maumivu za ute mzito za kuchua au zakupulizia.Vile vile unaweza kutumia dawa za kawaida za maumivu za vidonge kwa ajili ya kukupa utulivu.

Pata mapumziko ya kutosha na hakikisha unasitisha shughuli za kuchokoza maumivu haya ikiwamo kuweka shinikizo kubwa katika shingo.Epuka kulalia mto mpaka upone, epuka matumizi ya vitu kama kompyuta kwa kuwa vinachangia shingo kupinda.Fika katika huduma za afya mapema pale maumivu yasipoisha, yanapokuwa makali yasiyovumilika, yatakapoambatana na homa kali na kuvimba shingo, kufa ganzi au kupo-teza hisia maeneo jirani na shingo

Maumivu ya shingo ni moja ya tatizo ambalo wanamichezo na watu wa kawaida limewahi kuwapata katika maisha yao ya kila siku .

Tatizo hilo huwa na maumivu ya wastani mpaka makali yasiyovumilika.

Shingo kwa ujumla imeundwa na pingili za vifupa vidogo vilivyoanzia katika fuvu la kichwa.

Katikati ya vifupa hivyo huwa na santuri plastiki (cervical disc) ambazo hukaa katikati ya pingiri moja na nyingine kazi yake ni kunyonya shinikizo la uzito na kuzuia msagiko.

Vifupa, nyuzi ngumu za ligamenti na misuli ya shingo kazi yake ni kutoa msaada kwa kichwa na kuwezesha mienendo mbalimbali ikiwamo juu chini maarufu kama “ndiyo hapana”, pembeni na kujizungusha.

Wakati wa mazoezi mbalimbali ya kujenga utimamu wa mwili na afya kiujumla mienendo hii inaweza kuleta vijeraha vidogovidogo vinavyosababisha hitilafu, shambulizi au majeraha ya shingo, hivyo kuleta hisia za maumivu katika eneo hili.

Chanzo kikubwa cha kujitokeza kwa tatizo hili ni kujeruhiwa kwa misuli ya shingo pale unapokuwa katika mkao hasi wa kimwili ikiwamo kujipinda kuelekea uelekeo hasi kwa mwili wakati wa mazoezi.

Vile vile kwa wale ambao ni wafanya mazoezi kwa afya ambao wengi wana kazi zao kama ajira wanaweza kujiongezea kujijeruhi shingo zaidi wakati wakulala, utumiaji kompyuta, kukaa katika viti vya gari, ofisini na nyumbani kwa muda mrefu bila kupumzika.

Tatizo hili linaweza pia kuwa ni shambulizi la mifupa pingili za shingo kutokana na kutumika na kulika kwa mifupa hiyo na historia ya kuwahi kupata ajali, magonjwa ya shingo na matatizo ya mishipa ya fahamu.

Mara nyingi wanamazoezi watu wazima ndiyo wanaopata tatizo hilo mara kwa mara hii ni kutokana na umri kuwa mkubwa hivyo kuwa wahanga wa kanuni ya kulika na kutumika kwa viungo vya mwili.

Hutokea mara chache kwa baadhi ya wafanya mazoezi wenye dalili ya maumivu ya shingo likawa ni tatizo kubwa, mara nyingi huwa ni maumivu ya kawaida tu yanayoweza kuisha kwa siku chache.

Kwa kawaida maumivu ya kawaida ya shingo huwa yanaweza kuchukua siku 2-5 yakawapotea yenyewe.

Maumivu haya huwa ni kero na yanaweza kuwa makali kwa sababu shingo inapitisha mamia ya mishipa ya fahamu ndiyo maana huwapo na hisia kali za maumivu.

Mwandishi wa makala haya ni daktari.