Fursa hizi Ufaransa si za kukosa kwa vijana

Ufaransa ni moja ya mataifa ya Ulaya ambayo yanaongoza kwa utoaji wa elimu bora duniani na watu kutoka mataifa mbalimbali wamekuwa wakikimbilia nchini humo kufuata elimu katika fani mbalimbali.

Nchi hiyo imekuwa na uhusiano mzuri na Tanzania kwa muda mrefu na Serikali imekuwa ikipokea msaada kutoka Ufaransa, kwa ajili ya maendeleo katika sekta mbalimbali zikiwamo za elimu na utamaduni.

Hivi karibuni, Tanzania na Ufaransa zimeingia katika ushirikiano mpya kwenye sekta ya elimu ya juu kwa Ufaransa kufungua milango kwa Watanzania kwenda Ufaransa kusoma masomo mbalimbali ya shahada ya pili au zaidi.

Mwaka huu, Ufaransa itatoa ufadhili wa masomo kwa Watanzania 50 kwenda kusoma Ufaransa. Idadi hiyo imeongezeka kutoka idadi ya awali ya Watanzania 30 ambayo ilikuwa ikitoa miaka ya nyuma.

Mbali na ufadhili unaotolewa na Ufaransa, pia kampuni na taasisi nyingine zinatoa ufadhili wa masomo nchini humo. Ufadhili huo utawawezesha Watanzania kwenda kusoma Ufaransa katika fani na vyuo mbalimbali vya elimu ya juu.

Kutokana na Watanzania wengi kutokuwa na taarifa za kutosha kuhusu mazingira ya kielimu ya Ufaransa, nchi hiyo iliandaa kongamano la vyuo vikuu lililoshirikisha vyuo vya Tanzania na Ufaransa.

Zaidi ya wanafunzi 900 kutoka vyuo mbalimbali walishiriki kongamano hilo na kutembelea mabanda ya vyuo na kampuni mbalimbali, ili kupata taarifa za vyuo hivyo na kubadilishana uzoefu wa mambo tofauti.

Vyuo vikuu vya Tanzania vilivyoshiriki kongamano hilo ni Taasisi ya Nelson Mandela, Chuo Kikuu cha Kilimo – Sokoine (Sua), Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi cha Muhimbili (Muhas) na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm).

Vyuo vingine ni Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Chuo cha Taifa cha Utalii (NCT), Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU), Makumila, Aga Khan, Taasisi ya Teknolojia Dar es Salaa (DIT), St. Joseph, Chuo Kikuu cha Iringa, Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) na Chuo cha Taifa cha Zanzibar (Suza).

Kwa upande wa Ufaransa, vyuo 10 vilishiriki kongamano hilo, vyuo hivyo ni IMT Atlantique, UniLaSalle, Bordeaux Montaigne, Inseec U, Le Cordon Bleu, Grenoble, Bordeaux, CPU, Fondation Fabre na EM Lyon and EPF.

Hii ni fursa ambayo itawawezesha vijana wengi wa Kitanzania kupata elimu katika masuala tofauti ya kitaalamu ambayo yatawawezesha kujikwamua kimaisha, lakini pia kuleta ujuzi tofauti hapa nchini kwa viwango vya kimataifa.

Balozi wa Ufaransa hapa nchini, Frederick Clavier anasema mpaka sasa kuna wanafunzi 325,000 kutoka mataifa mbalimbali ambao wanasoma Ufaransa na kwamba ifikapo mwaka 2025 idadi ya wanafunzi hao itakuwa 500,000.

Anasema Ufaransa ina vyuo zaidi ya 200 ambavyo vinafundisha fani mbalimbali na zaidi ya programu 1,000 zinafundishwa nchini huko kwa lugha ya Kiingereza, hivyo, anawatoa hofu wanafunzi wa Tanzania ambao hawajui lugha ya Kifaransa.

Balozi huyo anasema elimu ni moja ya vipaumbele vya serikali ya Ufaransa na kwamba nchi hiyo inatenga asilimia 20 ya bajeti yake kwa ajili ya elimu. Anasema nchi yake inashika nafasi ya tatu duniani kwa kuvutia wanafunzi wa kigeni.

Mazingira hayo yaliyowekwa na Ufaransa ni fursa muhimu ambayo ikitumiwa vizuri inaweza kuzalisha wataalamu wenye ujuzi tofauti ambao wataweza kusaidia katika kutatua matatizo ya kijamii hapa nchini.

Rai yangu kwa vijana ni kutobweteka na shahada moja walizonazo bali wajiendeleze kielimu kwa kupata hamasa mpya kutoka vyuo vya nje ambavyo vitawaongezea maarifa tofauti kulingana na mazingira ya kiulimwengu.

Serikali imeanzisha ushirikiano huu na Ufaransa ikitambua kwamba fursa hiyo ya elimu itakuwa na manufaa makubwa kwa Taifa kwa sababu ujuzi watakaoupata huko utatumika kwa manufaa ya Watanzania wote.

Serikali imekuwa ikiweka mkazo kwenye diplomasia ya uchumi, hili nalo ni eneo muhimu ambalo linahitaji kuangaliwa kwa sababu ya umuhimu wa kutafsiri uhusiano wa Tanzania na mataifa mengine ambao una tija kwa maisha ya wananchi.

Peter Elias ni mwandishi wa Mwananchi 0763891422