Haraka inatakiwa uamuzi dhidi ya Roundup

Muktasari:

Tayari kuna mashtaka zaidi ya 9,000 yamefunguliwa yakiwa na madai hayo dhidi ya kampuni ambayo inazalisha na kuuza dawa hiyo duniani kote, kwa mujibu wa gazeti la Guardian linalotolewa Marekani.

Katika ukurasa wa tano wa gazeti hili kuna habari inayohusu kiuatilifu aina ya Roundup ambacho hutumiwa na wakulima wengi, hasa wa mpunga kuua magugu kabla ya kupanda mbegu kuanza msimu mpya.

Kiuatilifu hicho kina kiambata aina ya glyphosate ambacho kinadaiwa kuwa na kemikali ambazo zinasababisha ugonjwa hatari wa saratani.

Imani hiyo imeibuka baada ya raia mmoja wa Marekani kufungua mashtaka akidai kuwa matumizi ya kiuatilifu hicho yalisababisha apate ugonjwa huo na hivyo kushinda kesi ya madai ya fidia, akitakiwa alipwe Sh260 bilioni.

Tayari kuna mashtaka zaidi ya 9,000 yamefunguliwa yakiwa na madai hayo dhidi ya kampuni ambayo inazalisha na kuuza dawa hiyo duniani kote, kwa mujibu wa gazeti la Guardian linalotolewa Marekani.

Mjadala wa kiuatilifu hicho na kiambata hicho ambacho ni muhimu katika kuwezesha utendaji kazi wake, umekuwa ni mkubwa kote duniani, ambako watafiti na wanasayansi wanasema athari za kutumia kiuatilifu hicho ni kubwa kuliko faida zake na kushauri kisitumike hadi hapo utafiti utakaotoa majibu kamili utakapofanyika.

Wanasiasa wameshikilia msimamo huo kuwa hawawezi kupiga marufuku kiuatilifu hicho kwa kuwa hadi sasa hakuna ushahidi wa kisayansi unaothibitisha athari za kiuatilifu hicho na kwamba wataweza kuchukua uamuzi huo pale tu watakapothibitisha bila shaka kuhusu athari hizo.

Nchini Tanzania, ambako matumizi ya kiutilifu hicho ni makubwa, kwa mujibu wa waziri wa Kilimo, nako hawajakimbilia kupiga marufuku matumizi yake, bali ndio kwanza wanataka kuanza kufanya utafiti kujua ukweli kuhusu pembejeo hiyo.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alikaririwa akisema kuwa ushahidi ambao unasikika duniani kuhusu kesi ya raia huyo wa Marekani, si sababu ya kutosha kuifanya Tanzania ichukue uamuzi wa kuzuia matumizi ya kiuatilifu hicho.

Alisema kwa sasa anawasiliana na Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu (TPRI) ili kujua wataanza lini utafiti wa suala hilo ili kuiwezesha nchi kuwa na msingi wa kuchukua uamuzi wa kuizuia au kuiachia iendelee kufanya kazi.

Ni kweli kwamba bila ya utafiti, hakuna haki ya kuzungumza, kama Waingereza wanavyosema. Lakini kuna mazingira ambayo yanaweza kusababisha uamuzi uchukuliwe kwanza kusubiri matokeo ya utafiti.

Na mazingira hayo ni pale kitu fulani kinapoonekana kuwa na athari kwa maisha ya watu au kuhusishwa na ugonjwa ambao athari zake ni kubwa kwa binadamu.

Kwa mfano ,wakati huu ambao matumizi ya Roundup hayajapigwa marufuku, uamuzi huo unaweza kuonekana kuwa ni sahihi na muafaka, lakini utafiti utakapofanyika na kubainika kuwa madhara ya kiuatilifu hicho ni makubwa, uamuzi wa kutozuia utaonekana kuwa haukuwa sahihi na muafaka kwa kuwa itakuwa vigumu kufidia athari ambazo wananchi wamezipata kutokana na matumizi hayo.

Ndio maana kunapokuwa na shaka jambo ambalo linaonekana kuwa kubwa duniani kote, busara ni kuzuia matumizi ya dawa kama hiyo ili kuepusha athari zaidi wakati utafiti ukifanyika.

Kwa hiyo pamoja na kwamba Serikali imeamua kupata kwanza sababu za kisayansi zitakazotokana na utafiti ili kuchukua uamuzi dhidi ya kiuatilifu cha Roundup, bado tunaishauri ingechukua hatua ambazo ni za haraka kuzuia kuenea kwa athari zake iwapo zipo.

Ni dhahiri utafiti utachukua muda mrefu, lakini uchambuzi wa haraka wa kujua tafiti nyingine zimetoka na matokeo gani ungeweza kutusaidia kuchukua uamuzi wa awali ambao ungekuwa ni kuzuia matumizi kwanza wakati wa kusubiri matokeo ya utafiti.