Hata wewe unaweza kuwa mwekezaji

Saturday May 11 2019Kalunde  Jamal

Kalunde  Jamal 

By Kalaunde Jamal

Uwekezaji kwa tafsiri na lugha rahisi ni kuingiza fedha au kuweka kitu fulani kwa kwa ajili ya kujipatia faida.

Unaweza kuwa ni uwekezaji wa muda mrefu au mfupi, jambo la muhimu ni kufikia malengo ambayo ni kupata faida , bila shaka faida kubwa.

Hauwezi kuwa uwekezaji iwapo aliyeweka anapata hasara na sidhani kama katika akili ya kawaida yupo anayewekeza bure, kila anayefanya hivyo anakuwa na malengo ya kupata mafanikio.

Kuwekeza ndiyo inaweza kuwa njia pekee ya kujiandaa na maisha baada ya ajira kama umepata bahati ya kuajiriwa.

Lakini kama hujaajiriwa na una muda wa kufanya biashara moja unaweza kufanya uwekezaji kwenye maeneo mengine.

Kwa bahati mbaya vijana wengi hususani wasomi huamini katika ajira na kusahau kuhusu kujiandaa na maisha yajayo.

Wengi wanaamini anayepaswa kujipanga kwa ajili ya maisha yajayo ni mzee anayekaribia kustaafu.

Ukweli ni kuwa hakuna kitu ambacho siyo rafiki wa kudumu kama ajira, bila kujali umeipata mwaka jana au mwaka huu.

Hili hutokana na ajira nyingi kuwa kwenye sekta binafsi ambayo wamiliki au waajiri wana uwezo wa kuamua vinginevyo muda wowote.

Ajira si rafiki wa kudumu, muda wowote unaweza kuikosa kwa sababu mbalimbali ikiwamo maradhi.

Uwekezaji ni rafiki wa kudumu, hata ukiwa na maradhi au ulemavu utakaokukwamisha kufanya kazi zako moja kwa moja, ukiwa umewekeza bila shaka kuna watu au taasisi itakuwa inafanya kazi zako na wewe kupata ulichokusudia wakati unawekeza ambacho ni faida.

Hivyo unapotaka kufanya uwekezaji pia, unapaswa uangalie uwekezaji wa aina gani ambao utakuwa rafiki kwako adi mwisho wa maisha yako, kama utatetereka iwe umepata mtihani mkubwa ambao upo nje ya uwezo wako kuuzuia.

Vijana wengi wanataka kuwekeza leo wavune kesho, usiogope kuwekeza kwa sababu hutafaidi matunda yake mapema. Ndiyo maana unaitwa uwekezaji kuwa utakusaidia kesho ijayo na siyo leo.

Kuna uwekezaji rahisi unaopendwa na wengi, maduka makubwa, bidhaa za muda mfupi.

Uwekezaji mzuri na wenye faida kubwa ni ule wa muda mrefu ambao angalau huanzia miata mitano hadi 10.

Kwa sababu katika maisha ya ujana mambo ni mengi na uwekezaji bora ni ule unaowekeza ukiwa unafanya kazi au shughuli nyingine ukijipanga kwa ajili ya maisha uyajayo inaweza kukuwia vigumu kusimamia.

Hivyo njia salama ni kuwekeza kwenye uwekezaji usiohitaji usimamizi wa moja kwa moja.

Hivyo kama una fedha nyingi unaweza kuwekeza kwenye ununuzi wa viwanja au mashamba ambayo baada ya miaka mitano au 10 yataongezeka thamani na utakapouza unaweza kupata fedha mara tatu ya uliyowekeza.

Kwa kuwekeza kwenye mashamba au viwanja hautahitaji muda wa kufuatilia sana zaidi ya kuhakikisha yanakuwa masafi na unaweza kuyatumia kuwekeza kitu kingine ndani yake wakati unasubiri yaongezeke thamani ikiwamo kupanda mazao kama vile miti ya matunda au ya mbao.

Hili linawezekana kulingana na aina ya mkoa uliponunua shamba au kiwanja , ipo mingine haiwezekani kupanda miti unaweza kupanda kitu kingine au kujenga kisha kuuza nyumba kama nilivyokwisha kueleza hapo awali.

Unaweza pia kuwekeza kwa kujenga majengo ya biashara ambayo utayatumia kupangisha, uwekezaji huu huwa na tija zaidi iwapo utafanya hivyo maeneo ya mijini.

Eneo lingine unaloweza kuwekeza ni kwenye masoko ya fedha kwa njia mbalimbali.

Jambo la msingi ni kupata taarifa sahihi ya kampuni zinazofanya vizuri zaidi na kununua hisa kwa ajili ya kufanya uwekezaji huo.

Muhimu zaidi ni kuhakikisha unanunua hisa kwenye kampuni iliyosajiliwa au zilizosajili na Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE).

Hapa utakuwa umewekeza kwenye njia salama, utakuwa na uhakika wa kupata faida itokanayo na fedha ulizowekeza, lakini utaendelea na shughuli nyingine bila bughudha.

Pia unaweza kununua hati fungani za muda mrefu ambazo zinauzwa na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) katika uwekezaji huu utakuwa na uhakika na fedha zako na utapata faida itokanayo na riba ya fedha ulizoweka.

Kumbuka usikurupuke kufanya uwekezaji, kila unapowekeza hakikisha kuna utakachopata cha ziada ikiwezekana kiwe mara mbili ya ulichoweka.

Nasisitiza kabla ya kufanya maamuzi ya uwekezaji wa aina yoyote ile ni vema na muhimu kuonana na wataalamu wa masuala hayo kwa ajili ya kukupa ushauri au ufanye utafiti katika eneo unalotaka kufanya uwekezaji.

Uwekezaji mzuri ni wa muda mrefu na fedha nyingi kiasi, kama unataka kupata faida ukiwekeza zaidi bila shaka utavuna kikubwa pia.

Usisahau na siku zote kumbuka umri wa kuwekeza ni sasa wakati bado una nguvu ya kufanya jambo kutokana na kuwa na uwezo wa kukimbizana, kuzunguka kila kona.

Usisubiri uwe mzee au mtu mzima kwa sababu wakati huo ni wa kutumia na si kutafuta kwa machozi, jasho na damu.