MAONI: Hatua ya CCM kukataa rafu ni jambo jema

Uchaguzi wa serikali za mitaa unatarajia kufanyika nchini kote Novemba 24 mwaka huu.

Katika kuelekea kwenye uchaguzi huo vyama vyenye usajili wa kudumu tayari vimeanza kuwapanga wanachama wake kwa ajili ya kuwania uongozi katika maeneo mbalimbali nchini.

Miongoni mwa vyama ambavyo vimekuwa vikijipanga kwa uchaguzi huo ni chama tawala cha CCM ambako makada wamekuwa wakichuana kuwania kupitishwa kugombea uongozi katika serikali za mitaa.

Hata hivyo, kumekuwa na malalamiko ya baadhi ya wagombea kulia kuchezewa rafu jambo ambalo limemfanya katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kuingilia kati.

Dk Bashiru akizungumza na waandishi wa habari juzi alikiri kuwapo tatizo hilo na ndio maana ameagiza kurudiwa kwa uchaguzi wa wagombea katika maeneo ambayo yanalalamikiwa.

Dk Bashiru amesema kuwa miongoni mwa matatizo yaliyojitokeza katika uchaguzi huo wa kutafuta wagombea wa chama ni kutofuatwa kwa kanuni, wanachama kususa kupiga kura, wasimamizi kuchelewa kwenye vituo pamoja na vituo vya kupiga kura kubadilishwa na hivyo kuwachanganya wanachama.

Pia kulikuwa na matatizo ya usimamizi mbovu ulioruhusu watu wasiohusika kupiga kura pamoja na siri za chama kuvuja na hivyo kuibua taharuki isiyo ya lazima.

Mambo hayo yote yanatoa ishara mbaya katika kuwapata viongozi wa kuiwakilisha Serikali katika ngazi ya mitaa, hivyo tunaunga mkono hatua ambazo CCM imezichukua.

Tunaamini kuruhusu hujuma za ukiukwaji wa taratibu katika kupata viongozi si tu kwamba kunaweza kukiingiza chama katika matatizo kwa siku zijazo bali pia hali hiyo inaweza kuwasababishia matatizo wananchi wanaotarajia kuhudumiwa na viongozi hao.

Ikumbukwe kwamba viongozi wa ngazi za chini wana nafasi yao katika maendeleo ya nchi hivyo ni vyema kuhakikisha taratibu hasa misingi ya haki inazingatiwa katika kuwapata wawakilishi wa vyama.

Kilichofanywa na CCM ni sawa na kujifanyia tathmini mapema jambo ambalo ni zuri kwani katika kujifanyia tathmini huko wametaka haki itendeke kwa wagombea wote ndani ya chama hicho na kuepusha manung’uniko miongoni mwa wagombea wao.

Madhara ya viongozi wanaopatikana kinyume na taratibu ni makubwa na hayaishii katika chama husika bali yanaigusa jamii hasa mgombea asiyestahili anapopitishwa na chama chake na kushinda kwa nguvu ya chama na hatimaye kuwa kiongozi wa eneo fulani wakati hana sifa.

Bila shaka kiongozi wa namna hiyo ataendelea na michezo hiyo michafu hata akiwa madarakani na hivyo kuathiri jamii nzima ya eneo analoliongoza.

Ndio maana tunaipongeza hatua iliyochukuliwa na CCM na tungependa vyama vingine vinapoona michakato ndani ya vyama vyao haipo sawa, vichukue hatua.

Lakini jambo hilo kwa CCM lisifanyike kwa ngazi za chini tu, tunaamini hata itakapofika katika uchaguzi mkuu mwakani moto huo utaendelea hata kwa madiwani, wabunge na viongozi wengine wanaotaka ridhaa ya kuongoza kupitia chama hicho.

Malalamiko yanapotoka kwa watu au wagombea wengine ni jambo zuri yakawa yanafanyiwa kazi kwa kasi kama tulivyoshuhudia sasa kwa Dk Bashiru kuamuru uchaguzi urudiwe kwa maeneo ambayo yalilalamikiwa nchini kote.

Viongozi wanaochaguliwa ni wa watu wote bila kujali chama ndio maana tunataka wanaochaguliwa wawe na sifa.