UCHAMBUZI: Haya yafanyike kupata tija msimu ujao

Wednesday June 13 2018Ngollo John

Ngollo John 

Kwa mikoa ya Kanda ya Ziwa, pamba ni zao la kimkakati katika kuinua uchumi wa wananchi na kufanikisha lengo na mpango wa Serikali wa kuwa na uchumi wa kati wa viwanda ifikapo 2025.

Ili kufanikisha malengo hayo, mambo kadhaa yanatakiwa kufanyika kufanikisha kilimo chenye tija katika msimu ujao.

Miongoni mwa mambo hayo, wakulima wanatakiwa kuzingatia kanuni 10 za kilimo ikiwamo kuandaa shamba mapema na kupanda mbegu bora.

Ili kuzingatia hayo, Serikali na wadau wengine ambao katika mnyororo wa thamani wanakadiriwa kufikia milioni 19 wana jukumu la kuhakikisha pembejeo za kilimo zikiwamo viuawadudu na mbolea zinawafikia wakulima kwa wakati.

Huduma hizo zikitekelezwa mapema zitamsaidia mkulima kupata elimu ya kutosha kuhusu kilimo, tofauti na ilivyofanyika mwaka huu ambapo mazao yalishambuliwa na wadudu kutokana na kukosa huduma ya ugani kwenye maeneo mengi.

Hofu ya kushambuliwa na wadudu ilisababisha Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) kutumia zaidi ya Sh30 bilioni kununua na kusambaza chupa zaidi milioni saba za viuadudu.

Baada ya wadudu kudhibitiwa, wakulima hao sasa walikumbwa na tishio jingine; nalo ni mvua za masika hali iliyosababisha zao hilo lisilopenda mvua nyingi lishindwe kutoa matunda.

Changamoto hizo tatu za wakulima, ukosefu wa maofisa ugani na wadudu waharibifu zimefifisha matarajio ya kuvuna zaidi ya tani 600,000 (kilo 600 milioni) za pamba zilizotarajiwa kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga.

Mtunga anasema kiasi hicho kinatarajiwa baada ya wakulima zaidi ya 500,000 kutoka wilaya 54 za mikoa 17 inayolima zao la pamba kulima zaidi ya eka milioni tatu.

Ni imani yangu kuwa endapo changamoto hizo zingetatuliwa mapema zingesaidia kuongeza uzalishaji wa zao hilo kutoka kilo 800 hadi kilo 1,200 kwa eka moja.

Hivyo ni vyema Serikali ikaweka mkazo kutatua changamoto hizo, hasa ni ile ya upatikanaji wa maofisa ugani kwa kila kijiji ili kuwasaidia wakulima kupata elimu ya kutosha kuliko ilivyo sasa ambapo maofisa hao wako katika ngazi ya kata pekee.

Mathalan, mwaka jana changamoto ya ukosefu wa maofisa ugani ilisababisha TCB kutumia wakulima wawezeshaji 4,534 ambao mashamba yao yalitumika kama shamba darasa kufanikisha kilimo chenye tija.

Kwa sasa wakulima wengi wamekata tamaa kuendelea na zao la pamba ambalo katika awamu ya tano ya uongozi yenye sera ya viwanda, viongozi walipiga kelele na kuhamasisha kila kaya kutenga eka moja kwa ajili ya zao la pamba.

Juhudi hizo pia zielekezwe kwa kuajiri maofisa ugani wengi, watakaosaidia katika uboreshaji wa zao hilo ili kuwasaidia wakulima wasikate tamaa.

Sera ya viwanda itatekelezwa endapo kutakuwa na wataalamu wa kutosha kuhusu masuala ya kilimo kwa kuwa hatuwezi kuwa na viwanda vinavyotumia malighafi inayotoka nje, bali izalishwe na wakulima wetu wa ndani.

Nakubaliana na hoja ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa bungeni Juni 7 wakati akijibu maswali ya wabunge kuwa ni vizuri kuandaa mdahalo wa kitaifa kuhusu kilimo, hali itakayosaidia kuchochea maendeleo endelevu.

Mdahalo huo pamoja na mambo mengine pia ujikite katika kutoa elimu kwa wakulima ili wazingatie ushauri wa wataalamu.

Ili kupata tija kwenye msimu ujao wa kilimo tuelekeze nguvu nyingi kwenye kilimo chenye tija.

0757 708277