Hiki ndiko chanzo cha mkojo wa mtoto kutoa harufu, kukosa choo

Unajua kuwa mtoto mdogo mwenye umri chini ya miezi sita akijisaidia haja kubwa chini ya mara sita kwa siku ni hatari? Na pia, mkojo wake ukiwa unatoa unatoa harufu kali siyo dalili nzuri?

Wataalamu wa lishe wanasema matatizo hayo ya watoto yanatokana na baadhi ya wanawake kutowanyonyesha maziwa pekee kwa ufasaha.

Suala hilo, hawalipi kipaumbele; lakini wataalamu hao wanaeleza kuwa mkojo wa mtoto wenye harufu kali ni miongoni mwa dalili kuwa mama yake hamnyonyeshi mtoto wake maziwa ya kutosha.

Ili kujua kama mtoto amenyonya kiwango cha kutosha ni lazima atakuwa amepata choo mara sita au zaidi kwa siku na hatakuwa na harufu kali ya mkojo.

Mtafiti wa Masuala ya Lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Dorisce Katana anasema ukiona mtoto mwenye umri chini ya miezi sita, anakojoa mkojo ambao hauna harufu kali na anajisaidia choo kikubwa zaidi ya mara sita kwa siku, basi utambue kuwa mtoto ameshiba maziwa ya mama ipasavyo.

Katana ambaye pia ni ofisa lishe, anasema maziwa ya mama ni chakula bora kwa mtoto kwa kuwa humpatia virutubisho vyote muhimu kwa ajili ya ukuaji wa mwili na kiakili.

Anasema kama mtoto atanyonyeshwa maziwa ya mama ipasavyo itasaidia kuwa na afya bora na kuimarisha kinga ya mwili dhidi ya maradhi mbalimbali.

Je hali ikoje katika unyonyehaji nchini?

Katana anasema utafiti wa hali ya Kidemografia na Afya uliofanywa nchini mwaka 2015/16 (TDHS) unaonyesha kuwa ni asilimia 59 tu ya watoto wenye umri chini ya miezi sita, ndiyo wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee kama inavyoshauriwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Utafiti huo unaeleza kuwa wengine wananyonyeshwa pamoja na kupewa kinywaji au vyakula vingine tofauti na maziwa ya mama.

“Kwa takwimu hizi, inaonyesha wazi kuwa unyonyeshaji wa watoto katika jamii zetu bado uko chini, watoto hawanyonyeshwi ipasavyo. Zaidi ya asilimia 90 ya watoto wananyonyeshwa maziwa ya mama, lakini ni wachache wananyonyeshwa kwa ufanisi na kwa muda unaotakiwa,” anasema Katana.

Anabainisha kuwa ili mtoto aweze kunyonya vizuri, kwanza mama anatakiwa kumnyonyesha mtoto maziwa yake ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa.

“Hii itasaidia mtoto kunyonya maziwa ya mwanzo mazito yenye rangi ya njano ambayo hutoka siku chache za mwanzo baada ya mama kujifungua,” anasema Katana.

Anafafanua kuwa maziwa hayo ni chakula kamili chenye virutubisho vingi na kinga maalumu dhidi ya maradhi.

Pia, maziwa ya njano humsaidia mtoto kutoa kinyesi cha mwanzo chenye rangi ya kijani au nyeusi ambacho humfanya aumwe tumbo siku za mwanzo kama hatonyonya maziwa ya mama.

“Ili kumsaidia mtoto kunyonya ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa inashauriwa mama na mtoto wagusane ngozi kwa ngozi na kisha mtoto awekwe kweye titi la mama ili aanze kunyonya.

“Mama na mtoto hawatakiwi kutenganishwa, wanatakiwa wawe pamoja muda wote ili kuhamasisha unyonyeshaji, ila atatenganishwa tu kwa ushauri wa daktari kama kutakuwa kuna tatizo litakalomuathiri mtoto akiwa na mama yake, mfano ugonjwa wa mtoto au mama,” anasema Katana.

Vile vile mzazi anatakiwa kumnyonyesha maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita ya mwanzo na kwamba katika kipindi hicho mtoto haruhusiwi kupewa chakula au kinywaji kingine zaidi ya maziwa ya mama, isipokuwa dawa zilizoshauriwa na daktari.

Katana anasema katika miezi sita ya mwanzo ya mtoto, maziwa pekee ya mama yanatosha kwa kuwa ni chakula na kinywaji chenye virutubisho vyote anavyohitaji mtoto.

Madhara ya kumpa mtoto vyakula kabla ya miezi sita

Daktari Rehema Mzimbiri ambaye pia ni mtafiti kutoka TFNC, anasema kumpa mtoto vyakula au vinywaji vingine zaidi ya maziwa ya mama katika umri wa chini wa miezi sita ni hatari kwa sababu utumbo wake wake unakuwa laini na hauwezi kufyonza virutubisho vilivyoko kwenye vyakula hivyo kwa ufanisi.

“Kama mtoto chini ya miezi sita atapewa vyakula au vinywaji vingine zaidi ya maziwa ya mama pekee, anakuwa kwenye hatari ya kupata utapiamlo,”anasema Dk Mzimbiri.

Pia, anasema vyakula hivyo vinaweza kuwa vimeshikwa na vimelea vya maradhi na kumsababishia mtoto magonjwa kama kuharisha.

Dk Mzimbiri anasema pia, vinywaji au vyakula hivyo humpunguzia mtoto hamasa ya kunyonya maziwa ya mama.

Faida ya kunyonyesha mtoto

Miongoni mwa faida za kunyonyesha mtoto ni uwezekano mdogo wa mzazi kupata msongo wa mwanzo baada ya kujifungua, saratani ya titi pamoja na kinga dhidi ya maradhi ya unene kupita kiasi kwa mtoto aliyejifungua.

Shamim Ally ni mama aliyejifungua hivi karibuni, katika Hospitali ya Palestina jijini Dar es Salaam, anasema kumyonyesha mtoto maziwa ya mama pekee kwa kipindi cha miezi sita inamsaidia mama kuchelewa kurudi katika mzunguko wa siku zake (hedhi kwa wanawake).

“Hali hii huwasaidia wanawake kuchelewa kupata mimba nyingine mapema na hivyo kupunguza uzazi wa karibu karibu,” anasema Shamim.