Hili la Prisons na Biashara liwe funzo kwa TFF, Klabu za Ligi Kuu Bara

Mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara yamefikia katika hatua muhimu na ngumu baada ya idadi kubwa ya timu kubakiza mechi kati ya tano hadi nane kabla ya kumalizika.

Timu ya Simba pekee ndio imebakiwa na idadi kubwa ya mechi baada ya kucheza michezo 22 kutokana na ushiriki wake wa michuano ya kimataifa.

Hata hivyo, Simba juzi usiku iliaga rasmi michuano hiyo baada ya kuchapwa mabao 4-1 na TP Mazembe ya DR Congo katika mechi ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika

Katika mechi ya kwanza iliyochezwa Aprili 6 Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, timu hizo zilitoka suluhu.

Simba inarejea katika mashindano ya ndani (Ligi Kuu) huku ikikabiliwa na mechi 11 za viporo, hivyo italazimika kucheza mfululizo ili kumaliza mechi zake sawa na timu nyingine.

Wakati Ligi Kuu ikifikia hatua ngumu, timu 10 zinachuana kuepuka janga la kuteremka daraja msimu ujao. Yanga, Azam na Simba zinapambana kileleni kuwania ubingwa msimu huu.

Pamoja na ligi hiyo kuingia hatua ya ushindani, mashindano hayo yamekuwa shubiri kwa idadi kubwa ya timu kutokana na changamoto mbalimbali.

Kitendo cha ligi kukosa mdhamini kimeziweka timu hizo katika mazingira magumu ya kushindana.

Ligi ya msimu huu imekosa mvuto baada ya kukosa mdhamini ambaye wakati wote amekuwa msaada mkubwa kwa klabu.

Pia idadi kubwa ya timu hazina mdhamini na zimekuwa zikijiendesha kwa taabu na wakati mwingine kupata matokeo wasiyotarajia kutokana na ukata.

Maumivu ya ligi na klabu kukosa udhamini yaligusa pia mameneja wa viwanja nchini ambao wameachiwa mzigo wa madeni.

Baadhi ya meneja wa viwanja hawajui watalipa vipi madeni yao baada ya kuingia mkataba na wafanyabiashara wenye maduka ya vifaa vya ujenzi.

Kwa mfano kitendo cha mchezo baina ya Prisons dhidi ya Biashara United kuingiza mapato ya Sh9,000 kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya kinathibitisha namna gani klabu zinavyojiendesha kwa taabu.

Kwa mujibu wa maelezo ya meneja wa uwanja huo, Modestus Mwaluka, mchezo huo uliingiza Sh9000 tu na mashabiki watatu ndio waliokata tiketi kwa kiingilio cha Sh3000 huku yeye akiambulia Sh1000.

Mwaluka anasema alikopa vifaa vyenye thamani ya Sh150,000 vya maboresho ya uwanja na chokaa mifuko 10 ambapo kila mmoja Sh60,000 kwa ajili ya kuweka mistari ya uwanja.

Huu ni mfano tu, lakini wapo mameneja wengi wanaugulia maumivu kwa kuachiwa mzigo wa madeni uliotokana na maboresho kwa ajili ya maandalizi ya mechi husika.

Kimsingi mashindano yanapokosa mvuto idadi ya mashabiki uwanjani itapungua na ndio mwanzo wa wasimamizi wa viwanja (meneja) kuingia katika madeni na wafanyabiashara. Moja ya kazi ya meneja ni kuhakikisha uwanja unakuwa katika hali nzuri ya miundombinu ya nje na eneo la kuchezea.

Ni jukumu la meneja kuhakikisha uwanja unakidhi vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hivyo analazimika kwa njia yoyote ile kufanya maboresho mara kwa mara.

Kwa mantiki hiyo ili uwanja uboreshwe zinahitajika fedha kupitia kodi zinazopatikana kutokana na viingilio vya mashabiki.

Bila mashabiki uwanja hauwezi kuwa katika hali bora kwa mashindano. Hapa sasa ndipo meneja anapolazimika kufanya kazi ya ziada wakati mwingine kukopa fedha nje ya utaratibu ili kufanya maboresho.

Kwa hatua tuliyofikia hakuna namna Shirikisho la Soka (TFF) na Bodi ya Ligi, taasisi hizi zina wajibu wa kutafuta dawa ya kuhamasisha mashabiki kwenda kwa wingi viwanjani.

Ni ndoto soka yetu kupiga hatua kama viwanjani watakwenda watu wachache kuziunga mkono timu zao zinapocheza dhidi ya wapinzani wao.

Ukiondoa mechi za Simba au Yanga zinapocheza mikoani, mechi nyingine zinazokutanisha timu ‘ndogo’ hazina msisimo kutokana na idadi ndogo ya mashabiki kwenda viwanjani.

Kwa kuwa ligi hiyo inaelekea ukingoni, ni vyema TFF na Bodi ya Ligi zikajipanga mapema kwa mashindano ya msimu ujao ili kuepuka aibu kwa klabu na meneja wa viwanja.

Taasisi hizo zinapaswa kuja na mpango mkakati wa kupata mdhamini wa uhakika ambaye atakuwa chachu ya kurejesha utamaduni wa mashabiki kwenda viwanjani kushuhudia mechi za Ligi Kuu.

Naamini ligi yetu ina wachezaji hodari wenye vipaji, hivyo mashindano hayo yakiboreshwa tuna hakika wa kuwapata wakina Mbwana Samatta kila mwaka.

Pamoja na TFF, Bodi ya Ligi, klabu kupitia viongozi wao zina wajibu wa kubadili mifumo yao ya kiutendaji kwa kuacha kufanya kazi kwa mazoezi.

Baadhi ya viongozi wa klabu wameshindwa kwenda na kasi ya mabadiliko ya kiuchumi, badala yake wamekuwa wakifanya kazi kwa mazoea.

Kama viongozi wa klabu wangekuwa na mpango mkakati wa vyanzo vingine vya mapato, naamini ligi hiyo ingekuwa na ushindani kwa kuwa timu zingecheza kwa kiwango bora ili kupata matokeo mazuri.

Hili lililojitokeza kwa Prisons na Biashara kuingiza Sh9000 katika mechi yao liwe funzo kwa TFF, Bodi ya Ligi na viongozi wa klabu.