Breaking News

MAONI: Hili la mabasi kusafiri saa 24 ni muafaka

Tuesday July 9 2019

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema kuanzia sasa, mabasi ya masafa marefu yanaweza kusafiri kwa saa 24.

Kwa muda mrefu sasa, mabasi hayo yamepangiwa kuanza safari zake saa 12:00 asubuhi hadi saa 6:00 usiku na unapofika muda huo kama hayajafika mwisho wa safari hutakikiwa kusimama na kuendelea na safari siku inayofuata.

Uamuzi wa kupanga muda huo ulitokana na mambo mawili, ajali za usiku na tishio la hali ya usalama katika maeneo mbalimbali kutokana na uwepo wa matukio ya ujambazi.

Hivyo, hatua ya kupiga marufuku usafiri wa mabasi ya masafa marefu usiku ililenga kuokoa maisha ya watu na mali zao, ingawa kwa upande mwingine ilikuwa na athari kwa maendeleo ya kiuchumi kwa kuwa watu walilazimika kuchelewa kwenye shughuli mbalimbali kutokana na usafiri wa umma kuwa na muda mahsusi.

Akitangaza ruhusa hiyo juzi, katika Kijiji cha Namibu, Mwibara wilayani Bunda kwenye mkutano wa hadhara, Lugola alisema kama kilichosababisha kusimamishwa kwa safari za mabasi kwa muda ilikuwa ni kuhofia usalama, kilichotakiwa ni kuimarisha ulinzi.

Alisema wahalifu hasa majambazi wasipewe nafasi ya kutamba, bali wasakwe na kudhibitiwa kila kona ya nchi.

Advertisement

Tunaunga mkono hatua ya Waziri Lugola kuona umuhimu wa mabasi ya masafa marefu kuendelea na safari kwa saa 24 kwa ajili ya kuhakikisha hakuna muda wa uzalishaji mali unaopotea.

Ikiwa kikwazo ni hofu ya uhalifu, suluhisho ni lile aliloagiza waziri huyo kwa makamanda wa polisi katika kila eneo kuhakikisha wanadhibiti usalama wa raia na mali zao muda wote mahala popote bila ya kujali mchana au usiku.

Kama katika baadhi ya nchi zikiwamo za jirani suala la kusafiri kwa saa 24 linatekelezeka bila ya kikwazo, kwa nini lisiwezekane hapa kwetu ambako kuna vyombo imara na mahiri vya ulinzi na usalama wa raia na mali zao.

Wakati Tanzania ikipambana kuingia katika uchumi wa kati, uhakika wa usafiri hasa wa barabara ambao utaendelea kuwa nyenzo muhimu ya kuunganisha eneo moja na jingine hivyo uwapo wake unapaswa kuwa wa muda wote na sio kama ilivyokuwa.

Tunaamini kwamba Jeshi letu Polisi na vyombo vingine vya ulinzi na usalama wanao uwezo mkubwa wa kudhibiti usalama katika barabara kuu ili kuhakikisha kwamba safari zinafanyika muda wote bila ya kujali kama ni mchana au usiku.

Sambamba na agizo hilo la Waziri Lugola ambalo tunaliunga mkono, tunatoa angalizo kwa wamiliki wa mabasi hayo na madereva kuunga mkono hatua hiyo kwa kuzingatia sheria na taratibu za usalama barabarani wakati wote.

Tunaamini kwamba wao ni wadau wakubwa wa kuimarisha usalama kwa kuhakikisha kuwa vyombo vyao vina ubora wa kuingia barabarani na vinaendeshwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.

Hatutarajii kwa mfano, kuona ruhusa hiyo ikitumiwa na wenye vyombo hivyo kuingiza vile ambavyo mchana haviwezi kufanya safari kutokana na kuwa na hitilafu mbalimbali ikiwamo kutokuwa na vibali vinavyotakiwa.

Wakifanya hivyo, itakuwa rahisi sasa kwa polisi kufanya jukumu la pili ambalo ni kuimarisha hali ya usalama katika barabara yanakopita kwa kuongeza doria na ikibidi, kuyasindikiza ili yafike salama.