MAONI: Hivi ma-DC hawaheshimu kauli za mawaziri?

Wednesday December 5 2018

 

Tabia ya baadhi ya wakuu wa mikoa na wilaya waliogeuza Sheria ya Tawala za Mikoa kama fimbo ya kuwachapia watu kwa kuwaweka ndani kila wanapojisikia kufanya hivyo, imeendelea kushika kasi, licha ya viongozi kadhaa, hasa mawaziri kujitokeza kukemea na kuonya mara kwa mara.

Tayari mawaziri kama Selemani Jafo (Tamisemi), Ummy Mwalimu (Afya) na George Mkuchika (Utumishi na Utawala Bora) wameshaeleza namna wakuu hao wasivyozingatia misingi ya utawala bora kwa kuweka ovyo watu mahabusu.

Imefikia mahali wateule hao wa Rais wamekuwa wakiogopwa na wananchi na sasa wawekezaji walio katika maeneo wanayoyaongoza kwa kuwa haifahamiki nini wataibuka nacho kwa sababu hawaishii kupokonya mali kama ardhi pekee, bali kuamuru watu wakamatwe na kuwekwa ndani na mara nyingine wakikadiria muda wa kukaa ndani (mfano awekwe mahabusu kwa saa 48) kana kwamba ni hukumu ya adhabu.

Na katika kile kinachoonekana sheria hiyo inatumika kama adhabu badala ya kuitumia kwa malengo yaliyokusudiwa, zinapoisha saa 24 au 48 hakuna hatua nyingine zinazochukuliwa, kumaanisha kuwa aliyewekwa mahabusu hakuwa anahatarisha amani au maisha yake, bali ilikuwa ni kumuadhibu tu.

Hii haichori picha nzuri na kama tulivyowahi kusema katika safu hii, matumizi mabaya ya sheria hiyo yanaweza kusababisha wengi, hasa wanyonge, ambao ni wale wasio na fedha, wasio na nafasi au wasio na madaraka, kunyanyasika na kukosa amani kwenye ardhi yao.

Akizungumza katika mkutano wa mafunzo kwa wakuu wa mikoa na makatibu tawala ulioandaliwa na Taasisi ya Uongozi mjini Dodoma, Waziri Mkuchika aliwashangaa wakuu hao kwa kuitumia sheria hiyo hata katika mazingira ambayo hayastahili.

Mkuchika alisema imekuwa ni kawaida hivi sasa kwa baadhi ya wakuu wa wilaya na mikoa kuwaweka ndani watumishi wa umma hata kwa mambo ya kawaida kama kuchelewa kufika katika vikao vya kazi, kisha akatoa mfano namna alivyofanya kazi ya u-DC kwa miaka 14 na minane ya u-RC bila kumuweka ndani mtu yeyote, lakini kazi zilifanyika.

Alisema sheria hiyo inawapa mamlaka wateule hao kuchukua hatua kubwa kama hiyo iwapo tu mhusika anahatarisha usalama na amani katika eneo husika au maisha yake yako hatarini, hivyo anahitaji kuhifadhiwa mahabusu kwa muda usiozidi saa 48.

Ni katika msingi huo, aliwaambia wakuu hao wa mikoa na makatibu tawala kuwa atawaelewa zaidi iwapo wataitumia sheria hiyo vizuri kwa kufuata misingi na taratibu.

Hata hivyo, unapotafakari matukio mengi ambayo wakuu hao wamehusika nayo kwa kuwaweka watu ndani, huoni mantiki ya uzito wa makosa yaliyofanywa kiasi cha hatua hiyo kubwa kufikiwa dhidi ya wahusika.

Hivi mtu aliyemilikishwa shamba kwa njia zisizo sahihi anawekwaje ndani? Ni usalama na amani gani aliyotishia mpaka akamatwe na kuwekwa mahabusu badala ya kushtakiwa mahakamani?

Kama walivyosema mawaziri hao, wakuu wa wilaya na mikoa hawana budi kubadilika. Hata hivyo, jambo la kujiuliza hivi ni mpaka nani aseme ndipo wakubali kubadilika? Maana kama ni kuambiwa na wakubwa, mawaziri wameshasema na hata Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliligusia suala hilo juzi akionyesha kushangazwa na namna wanavyoitumia sheria hii.

Ni wakati sasa wa viongozi wa juu kueleza kwa dhati kuhusu matumizi haya mabaya ya sheria na kuweka mkakati kuhakikisha viongozi wa mikoa wanaheshimu maelekezo yanayotolewa na kuyafuata badala ya kuendelea kulalamika.