Hizi ndizo dhana potofu kuhusu hedhi

Friday April 5 2019

 

By Florence Majani, Mwananchi

Hedhi. Ni neno dogo lenye herufi chache tu, lakini linabeba maana kubwa kiafya, kiakili na kiuchumi kwa mwanamke.

Ni hali ya lazima kwa mwanamke yeyote ambaye amefikia umri wa balehe. Tunaweza kusema ni jambo linaloleta karaha kimwili lakini kwa upande mwingine lina faida kiafya. Hii ni kwa sababu mwanamke anapofikia umri wa balehe na asipate hedhi, basi atakuwa na matatizo makubwa kiafya.

Wataalamu wa afya wanaichambua hedhi kuwa ni mchakato wa kibaolojia unaosababisha kutokwa damu kwenye ukuta wa uzazi wa mwanamke katika kipindi maalumu. Kiafya hedhi hutakiwa kutoka kila mwezi kasoro wakati wa ujauzito na pindi mwanamke anapokoma hedhi (menopause).

Hata hivyo wapo baadhi ya watu wamekuwa na imani tofauti kuhusu mwanamke aliye katika hedhi. Imani hizo zimesababisha mahudhurio hafifu shuleni, unyanyapaa, ubaguzi na hata kumkosesha mwanamke fursa.

Ukishika mmea, mboga za majani na maua vitanyauka

Dhana hii imekuwapo kwa miaka mingi. Bibi zetu walikuwa wakisema kuwa mwanamke anapokuwa katika siku zake, basi hatakiwi kushika mmea au kuchuma mboga za majani kwa sababu zitanyauka.

Hellen Mbonea,(56) Mkulima na mkazi wa Namtumbo anasema, wamekuta mila hiyo kwa wazazi wao na walikatazwa kabisa kushika mboga za majani wanapokuwa kwenye siku zao.

“Tulisimamia hayo maagizo, kwa sababu hata hatukujaribu kufanya uchunguzi wowote kujua kama ni kweli. Cha muhimu ni kuwa tumekatazwa, basi, ” anasema Mbonea.

Alipoulizwa iwapo aliwahi kushuhudia kama kuna mmea uliowahi kuathirika kwa kushikwa na mwanamke aliye kwenye hedhi, alisema hajawahi kuona.

“Sijawahi kuona. Lakini bado nasimamia hayo maagizo kutoka kwa mama na bibi yangu, na mimi nawafundisha wadogo zangu na wanangu,” anasema.

Usimbebe mtoto mchanga

Baadhi ya imani ni ile ya mwanamke aliye kwenye hedhi kuzuiwa kumbeba mtoto mchanga kwa sababu mtoto huyo ataumwa.

Lilian Mitande(81) ambaye ni mkunga mstaafu anasema mafunzo au maagizo hayo yanatolewa katika familia na kurithishwa vizazi na vizazi.

“Unajua unapokuwa msichana unaambiwa mambo mengi na kwa sababu ni mgeni wa jambo hilo, unalishika sana,” anasema Mitande.

Anasema inaaminika katika kabila la Wayao kuwa mwanamke aliye katika hedhi hatakiwi kushika mtoto kwa kuwa ataumwa.

Ukioga maji ya moto damu itatoka kwa wingi

Floramarie Muchunguzi, mwanafunzi wa kidato cha pili Shule ya Sekondari Arusha anasema anachofahamu na kuamini ni kuwa ukiwa kwenye siku zako za hedhi, ukioga maji ya moto damu itatoka kwa wingi.

“Ninawasikia wenzangu ninaosoma nao na wakati mwingine, baadhi ya ndugu zangu wakubwa. Kwa hiyo nikiwa ‘period’ naoga maji ya baridi tu,” anasema Muchunguzi.

Huwezi kupata mimba ukiwa kwenye siku zako za hedhi

Wapo baadhi ya wanawake na wanaume huamini kuwa unapofanya tendo la ndoa wakati wa siku za hedhi huwezi kupata ujauzito.

Benadeta Mwita anasema anaamini hivyo kwa sababu tayari yai limepevuka na damu inatoka hivyo huwezi kushika mimba kwa wakati huo.

“Kwa kawaida mimi sijisikii amani sana kufanya tendo la ndoa wakati wa hedhi, lakini najua hata nikifanya hivyo siwezi kupata mimba kwa sababu damu inakuwa tayari imeshaanza kutoka ina maana yai limeshajichavusha,” anasema Mwita.

Wataalamu wanasemaje?

Akizungumzia dhana na ukweli kuhusu hedhi, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Kinamama,Hospitali ya Mwananyamala Daniel Nkungu anasema: “Hakuna uhusiano wa hedhi na kunyauka kwa mboga au mimea na hivyo hakuna ukweli katika hili. Hakuna uhusiano wowote kati ya hedhi na mimea. Ni vitu viwili tofauti.”

Kuhusu mwanamke aliye katika hedhi kukatazwa kumshika mtoto mchanga, Dk Nkungu anasema hilo pia halina ukweli.

“Suala hapo la kuzingatia ni usafi tu, lakini mwanamke aliye katika hedhi anaweza kabisa kumshika mtoto au mtu yeyote na akawa salama. Sidhani kwamba mtu anaweza kuwa katika hedhi hadi mikono yake ikawa na damu, sidhani kabisa,” anasema Dk Nkungu.

Akizungumzia kuhusu kushika mimba wakati wa hedhi, Dk Nkungu anasema ni kweli, huwezi kushika mimba wakati wa hedhi.

“Kile kinachohitajika ili kulipevusha yai ndicho hicho kinachotoka ndiyo maana mtu akishika mimba, hapati siku zake.

Kuhusu tendo la ndoa wakati wa hedhi, Dk Nkungu anasema si salama sana kwani damu ya hedhi hushika bakteria kwa haraka zaidi.

“Ingawa hakuna madhara wala mimba lakini ni vizuri kutumia busara kidogo na kusubiri badala ya kufanya tendo la ngono kipindi hiki, nasisitiza busara zaidi na uvumilivu vitumike,” anasema.

Akizungumza wakati wa wiki ya uvumbuzi iliyofanyika Tume ya Sayansi na Teknolojia(COSTECH) Mkurugenzi Mtendaji wa Kasole Secrets watengenezaji wa taulo za kike(pedi) za Glory, Hyasinta Ntuyeko anasema watoto wa kike wanapata unyanyapaa pindi wanapokuwa kwenye siku zao kutokana na dhana hizi.

“Ingawa hatujafanya utafiti wa kisayansi zaidi lakini watoto wa kike wananyanyapaliwa kwa sababu tu ya dhana hizi za hedhi,”anasema.