MAONI: Hoja za korosho zisitolewe majibu rahisi

Tuesday February 12 2019

 

Zao la korosho katika msimu wa 2018/19 limepitia hatua tofauti na kulifanya pengine kuwa ndilo zao lililojadiliwa zaidi kwenye vyombo vya habari na hata vijiweni.

Mjadala huo unatokana na hatua ambazo korosho imepitia tangu uandaaji mashamba wakati wakulima walipopaza sauti kutaka pembejeo ziwafikie kwa wakati ili kuongeza uzalishaji. Kilichofuata baada ya kufunguliwa kwa dirisha la ununuzi wa korosho mwishoni mwa mwaka jana, ni hekaheka za bei zilizosababisha Serikali kuingilia kati ili kuwanusuru wakulima wasipunjike. Rais John Magufuli alitangaza kuwa Serikali imeamua kununua kila kilo kwa Sh3,300.

Bila shaka, haya yote yanatokana na umuhimu wa korosho kwa uchumi wa Tanzania hasa ikizingatiwa ndilo zao linaloongoza kuiingizia nchi fedha za kigeni.

Licha ya umuhimu wake, bado inaonekana kuna baadhi ya mambo yanayofanyika yakiwa hayaendani na kile kinachotarajiwa, hasa katika kujihakikishia kuwa tunapata wanunuzi wasio na doa na wa uhakika kwa ajili ya hapo baadaye.

Moja ya mambo hayo ni hili lililoibuka hivi karibuni kuhusu kampuni ya Indo Power ya Kenya iliyopewa fursa ya kununua tani 100,000 za korosho. mLicha ya makubaliano kusainiwa, wasiwasi umeibuka dhidi ya uwezo wa kampuni hiyo kufanya miamala ya mpaka zaidi ya Sh400 bilioni katika manunuzi.

Uwezo wake unatiliwa shaka .

Januari 30, mwaka huu Serikali ilitangaza kumpata mteja huyo atakayenunua tani 100,000 za korosho kwa dola 180,000 za Kimarekani (zaidi ya Sh418 bilioni), lakini wiki mbili baadaye, gazeti moja la kila wiki la The East African likachapisha taarifa kuwa kampuni hiyo iliyosajiliwa mwaka 2016, haina historia ya kufanya miamala mikubwa kiasi hicho.

The East African liliandika kuwa kampuni hiyo haina tovuti na kwamba taarifa zake za usajili zinaonyesha haina akaunti benki, wanasheria wala katibu wa kampuni na haina wakaguzi wa hesabu.

Lilieleza kuwa katika miamala iliyofanywa na kampuni hiyo tangu ianzishwe, haijawahi kuwa na mkataba japo wa dola 10 milioni na katika maelezo yake Indo Power, fedha za kufanikisha mkataba wake na Tanzania zitatokana na mkopo wa benki ya nje ya Kenya.

Lakini katibu mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Profesha Joseph Buchweishaija alitoa majibu yaliyoongeza utata. Alisema historia si hoja ya msingi waliyoipa kipaumbele kwa kuwa inayouza korosho ni bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko na kwamba jukumu lao lilikuwa ni kufanikisha biashara tu.

Ufafanuzi huo haujatosheleza hoja za shaka zilizowekwa dhidi ya kampuni hiyo. Tunadhani katibu mkuu alitakiwa awajibike kwa wananchi kwa kueleza tahadhari zilizochukuliwa kuhakikisha kwamba hofu yoyote imezingatiwa na kuwekewa mkakati wa kuhakikisha lolote baya halitokei.

Wakati huu nchi ikipambana dhidi ya matumizi ya fedha haramu na kuhakikisha manunuzi ya Serikali hayaachi maswali na pia yanakuwa yamezingatia sheria ambazo tumejiwekea, ni vizuri taarifa muhimu zikawekwa bayana.

Inawezekana Serikali ilifanya uchunguzi kujihakikishia uwezo na uhalali wa kampuni hiyo, hivyo majibu ya katibu mkuu yangelenga kutoa maelezo kuhusu suala hilo.

Hatupingi kampuni za nchi jirani kupewa fursa za biashara nchini, lakini tunahimiza kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa ni pia kutoa ufafanuzi unaoondoa wasiwasi.