MAONI: Hongera Simba kwa ushindi lakini kazi bado

Klabu ya Simba juzi ilianza vyema michuano ya Ligi ya Soka ya Mabingwa Afrika kwa kuitandika Jeunesse Sportive de la Saoura ya Algeria kwa mabao 3-0.

Matokeo hayo ya Kundi D la michuano hiyo lenye timu nne, yanawafanya mabingwa hao wa Tanzania kuongoza katika msimamo kwani katika mchezo mwingine, Al Ahly Sporting Club ya Misri iliifunga AS Vita ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) mabao 2-0.

Huo ni mwanzo mzuri kwa Simba hasa ikizingatiwa kwamba, kwa miaka mingi timu za Tanzania zimekuwa zikinyanyaswa na zile za Afrika Kaskazini kila zilipopangwa katika kundi moja au kukutana katika hatua za mtoano.

Mbali ya kuwapongeza wachezaji kwa kujituma vilivyo uwanjani hadi kupata ushindi huo na kazi kubwa iliyofanywa na uongozi wa klabu, hatuwezi kuwasahau mashabiki – mchezaji wa 12 uwanjani – kwa jinsi walivyojitokeza kwa wingi na kuishangilia timu yao kuanzia mwanzo hadi filimbi ya mwisho.

Tunaamini kwamba kwa kuwa mechi hiyo ilionyeshwa katika televisheni, sehemu kubwa ya dunia ilishuhudia mambo mawili makubwa; uwezo wa timu ya Tanzania katika kusakata kabumbu na pili; jinsi Watanzania wanavyopenda soka.

Mataifa mengi ya Afrika yamekuwa na changamoto kubwa ya kujaza viwanja pindi timu zao zinapocheza hata mechi kubwa kama hiyo, hivyo kilichoonyeshwa na mashabiki juzi kwenye Uwanja wa Taifa ni salamu tosha kwamba Tanzania inauweza mpira wa miguu na inaupenda kwelikweli.

Lakini pamoja na pongezi hizo, tunapenda kuwatahadharisha wana Simba hasa wachezaji na viongozi kwamba huu ni mchezo wa kwanza tu, zimebaki mechi tano kuvuka hatua hii hivyo washangilie ushindi huo wakifahamu kwamba ngwe iliyobaki ni kubwa, ndefu na ngumu zaidi.

Kwa mujibu wa ratiba ya michuano hiyo, Jumamosi ijayo, Simba itakuwa Complexe Omnisports Stade des Martyrs huko Kinshasa kupambana na AS Vita, moja timu kubwa Kusini mwa Afrika ambayo baada ya kujeruhiwa katika mechi ya kwanza, itataka kupata matokeo mazuri nyumbani ili kujiweka pazuri.

Tunaamini kwamba uongozi wa Simba unalifahamu vyema hilo hivyo, wito wetu kwa wachezaji ni kuongeza bidii na kutumia maarifa yao yote kuhakikisha kwamba ushindi unapatikana katika mechi hiyo na zijazo wakijua kwamba kufanya hivyo watakuwa wanajitangazia soko la kimataifa.

Hakuna shaka kwamba hivi sasa mawakala maarufu wa wachezaji duniani wanafuatilia michuano hii, hivyo ni fursa adhimu kwa wachezaji wa Simba kupambana ili wapate nafasi ya kupata mikataba minono zaidi kwenye klabu kubwa kwa manufaa yao na klabu.

Sambamba na wito huo, tunawakumbusha wachezaji wa Tanzania kuongeza juhudi ya kugombea namba na wenzao wa kigeni. Tungependa kuona mafanikio haya yakitokana na idadi kubwa zaidi ya wachezaji wa Tanzania.

Wito wetu kwa wachezaji wa Tanzania waliosajiliwa Simba ni kuongeza bidii ili kumshawishi kocha na kwamba wanaweza kufanya makubwa zaidi ya wageni. Ndiyo, tunaweza.