UCHAMBUZI: Hongera sana Dk Bashiru kukemea maovu

Tanzania ni miongoni mwa mataifa machache barani Afrika ambayo yanasifika kwa amani na utulivu.

Hata hivyo, amani na utulivu uliopo havijapatikana kirahisi bali kuna watu walikaa na kuweka misingi imara ambayo mpaka sasa tunafaidi matunda yake.

Walioweka misingi hii ni waasisi wa Taifa hili, hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Abeid Karume na viongozi wengine waliokuwapo miaka ya nyuma ambao wengi wao sasa wametangulia mbele ya haki.

Viongozi hawa si kama walikuwa hawana polisi wa kudhibiti wapinzani wao, la hasha, mara nyingi waliamini katika mazungumzo na maridhiano.

Hivyo waasisi hawa waliweza kuendesha siasa zao kwa kushughulikiana ndani ya vyama vyao na hivyo wakajenga misingi ya amani, umoja, mshikamano na upendo baina ya Watanzania wote.

Waasisi hawa hawakujali tofauti za kiitikadi, dini, makabila, rangi, utajiri au umasikini badala yake walifanya maamuzi ya haki.

Hata pale ilipotokea baadhi ya wanasiasa machachari walioamua kutofautiana na viongozi hawa, hakuna mabavu yaliyotumika kuwadhiti bali walishughulikiwa taratibu na mifumo iliyopo.

Mwalimu Nyerere aliwahi kuelezea kisa kimoja na kuibuka mgombea binafsi ndani ya Chama cha Tanu katika uchaguzi ambao uliofanyika Agosti 30, 1960 wa nafasi ya mbunge wa Mbulu na mgombea binafsi alishinda na kutangazwa.

Mgombea ambaye alikuwa amepitishwa kugombea na Tanu katika Jimbo la Mbulu alikuwa Chifu Amri Dodo lakini kuliibuka mgogoro na Herman Sarwatt aliyekuwa Tanu na kujiengua, kisha akagombea kama mgombea binafsi.

Uchaguzi huo utabaki kuwa funzo kubwa katika historia ya siasa za kistaarabu hapa nchini. Kulikuwa na jumla ya wagombea 25, kati yao 11 walisimamishwa na Tanu, kugombea lakini jimbo la Mbulu pekee kati ya viti 11 ndipo kulitokea upinzani ndani ya chama hicho na mgombea binafsi Sarwatt akashinda.

Funzo kubwa hapa ni kwamba kumbe hata kukitokea migogoro ndani ya vyama vyetu inaweza kumalizwa kwa amani na utulivu, bila kutumia polisi, Redbrige, Blue guard wala Green Guard.

Katika Jimbo la Karatu katika uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi mwaka 1995, ndani ya CCM kuliibuka mgawayiko hasa baada ya mgombea aliyeshinda kwa kura za maoni, Dk Wilbrod Slaa kuenguliwa na kumpitisha Patrick Qorro ambaye alikuwa akitetea kiti chake.

Kufuatia mgogoro huo, Dk Slaa alitangaza kuhamia Chadema na kugombea nafasi hiyo kwa tiketi ya upinzani.

Licha ya upinzani uliokuwapo, Dk Slaa alishinda kiti hicho bila vurugu zozote kutokea.

Hiyo ndiyo Tanzania ambayo tunajivunia hadi sasa.

Historia ya Taifa hili inaeleza kuwa kunaweza kufanyika chaguzi au mikutano ya wanasiasa kwa amani na utulivu bila jeshi la polisi kuingilia kwa kutumia mabavu.

Ingawa ni kweli kuwa siasa za sasa zimebadilika sana na kuna wakati inabidi nguvu kutumika kurejesha utulivu, lakini matumizi ya nguvu kubwa yamekuwa na dosari kubwa si Tanzania tu bali katika nchi kadhaa barani Afrika.

Nampongeza katibu mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally kwa kutoa kauli ya kiungwana na kushauri kupunguzwa mabavu katika kuwashughulikia na wanasiasa.

Dk Bashiru mzalendo wa kweli ambaye si rahisi kutilia shaka uadilifu wake, ametoa kauli hii katika kipindi ambacho Taifa linajiandaa kwa uchaguzi wa Serikali za mitaa na mwakani Uchaguzi Mkuu.

Kuna hofu ndani ya vyama vyote vya siasa za aina mbalimbali ikiwapo kuenguliwa majina na ‘wakubwa wao’ au kushindwa katika kura za katika chaguzi zijazo, hivyo wanasiasa wengi watamalizana wenyewe.

Hivyo, hakuna haja tena ya kutumia mabavu kwa wanasiasa kwani wengi watajichuja wenyewe na hadi kufika siku ya kupiga kura watakuwa tayari wamejua wapo nje ya ulingo na hawatakuwa na sababu wa kulitupia lawama jeshi la polisi.

Naamini kama alivyosema Dk Bashiru kutumia mabavu kuwadhibiti wanasiasa sasa inabidi kupunguzwa kwani wengi wao tayari wanajua hatima yao kutokana na siasa zilizopo hapa nchini.

Matumizi ya mabavu mara nyingi yamekuwa yakiwajengea chuki wananchi dhidi ya polisi na hivyo kuamua kupiga kura za hasira au kususia chaguzi na mwisho huwa ni majuto kwani wanaochaguliwa wamekuwa hawana uwezo wa kusaidia kusukuma maendeleo.

Mussa Juma ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Arusha