Imani potofu, umaskini vyachangia wajawazito kuchelewa kufika kliniki

Friday February 8 2019

 

By Rehema Matowo, Mwananchi [email protected]

Umewahi kusikia mtoto anapotea tumboni? Hii ni moja ya imani potofu inayowazuia baadhi ya wajawazito wilaya za Nyangh’wale na Geita kutowahi kliniki ndani ya miezi mitatu ya mwanzo.

Licha ya hali hiyo, kusababisha vifo vya watoto wachanga na wajawazito wakati wa kujifungua, baadhi wanaamini kuwa mtoto aliye tumboni atapotea baada ya mjamzito kupimwa na daktari.

Mbali na imani hiyo pia wengine huamini mimba itaharibika au wenye ‘macho mabaya’ watamroga mtoto.

Imani hizi zimeendelea kuchangia vifo vya wajawazito na watoto wachanga.

Gidesa Paulo, mkazi wa Kijiji cha Nyaseke wilayani Geita anasema ana ujauzito wa miezi saba na ndiyo ameanza kuhudhuria kliniki.

Mkazi huyo ambaye ni mama wa watoto saba anasema hakuwahi kuhudhuria kliniki mapema kwa vile anaamini kama akipimwa mimba changa, mtoto atapotea na hataonekana tumboni.

Anadai kuwa suala la kuwahi kliniki mapema ni uvivu wa kuogopa kazi za nyumbani kwa kuwa atatumia zaidi ya saa sita au zaidi ili aweze kufika kituo cha afya kupata huduma hiyo.

“Kuanza na miezi mitatu (kwenda kilini), nitachoka kutembea halafu ni kupoteza muda wa kazi za nyumbani, Bora nisubiri muda usogee. Labda nikiumwa. Kwa sasa nasikia maji mengi tumboni na tangu juzi (wiki iliyopita) simsikii mtoto akicheza ndiyo maana nimekuja waniangalie,” anasema Gidesa mwenye miaka 38.

Mjamzito Letsia Charles mkazi wa Kijiji cha Nyambogo amelazimika kuanza kliniki akiwa na ujauzito wa miezi saba kutokana na umbali wa kufika katika Zahanati ya Bulela.

Anasema ili aweze kuhudhuria kliniki anapaswa kuwa na Sh6,000 kila mwezi kwa ajili ya kugharamia usafiri wa pikipiki, kiwango ambacho ni kikubwa kwake.

“Natembea zaidi ya masaa matano ili nihudhurie kliniki. Ni lazima nipande pikipiki au baiskeli na mimi mwenyewe kuendesha baiskeli muda mrefu naumia ndiyo maana nilisubiri ili nihudhurie miezi ya mwisho kwa kuwa baada ya muda mfupi nitajifungua na pia sitatumia pesa nyingi,” anasema Charles.

Scola Paulo mkazi wa Kijiji cha Bwihegule Kata ya Mtakuja mjini Geita anasema licha ya elimu inayotolewa na wahudumu ngazi ya jamii kuhusu umuhimu wa kuwahi kliniki, umbali mrefu ni moja ya sababu inayochangia washindwe kupata huduma hiyo.

Asteria Samson ni mhudumu wa afya ngazi ya kijiji anasema licha ya kupatiwa mafunzo ya kuwaelimisha wanawake umuhimu wa kwenda kliniki lakini changamoto kubwa anayokutana nayo ni umbali wa eneo la kutolea huduma.

“Kina mama hujifungulia njiani na hata watoto wanaozaliwa hawapati huduma ya afya katika kliniki yetu. Hii ni shida sana kwetu,” anasema Samson.

Mkazi wa Kijiji cha Gamash, Chausiku Charles anasema alianza kwenda kliniki katika kipindi cha miezi mitatu ya mwanzo ya ujauzito.

Licha ya tumbo kubwa alilonalo, anasema anaendesha baiskeli umbali wa kilometa zaidi ya 10 ili aweze kufika Zahanati ya Bulela kuhudhuria kliniki kila mwezi.

Wahudumu wa afya

Neema Laizer ni muuguzi wa Zahanati ya Bulela iliyopo mjini Geita, anasema mila potofu bado ni tatizo kwa jamii licha ya elimu inayotolewa na watoa huduma za afya.

Neema anasema wanawake huamini kama wakipimwa na daktari au mhudumu wa afya mtoto atapotea.

“Hofu ya kurogwa na umbali wa vituo vya kutolea huduma ni miongoni mwa sababu zinazochangia kinamama kuhudhuria kliniki kuanzia miezi sita ya ujauzito.”

Neema anasema ili mtoto akue na afya njema, mjamzito anapaswa kula vyakula bora pamoja na kutumia dawa kwa ajili ya kinga kwa mtoto na dawa za kuongeza damu.

Muuguzi huyo anasema imani potofu kuwa mama akila asubuhi na kwenda kliniki husababisha mtoto asionekane wakati wa kupimwa, inasababisha wajawazito wateseke na njaa kwa kuwa wanatembea umbali mrefu na wakati mwingine huanguka barabarani.

“Wajawazito wanafika hapa wamechoka na hadi uwapime kisha warudi nyumbani hawawezi hata kutembea. Ukizungumza nao wanasema hawajala na sio kwamba wamekosa chakula bali ni imani tu kuwa mama akila chakula mtoto hataonekana kwenye kipimo.”

Muuguzi huyo anasema hata kwa wale watakaowahi kuhudhuria kliniki bado hawapo tayari kutumia dawa za hospitali kwa madai kuwa wakitumia dawa hizo uchungu utachelewa.

Mratibu wa Afya ya Mama, Baba na Mtoto wa wilayani Nyang’hwale, Jane Mhanda anasema kwa sasa wapo watoa huduma ngazi ya jamii ambao wanapita kaya kwa kaya kuwaelimisha umuhimu wa kuwahi kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupunguza vifo vya mama na watoto wachanga.

Mhanda anasema wilaya hiyo ina jumla ya wahudumu 120 katika ngazi ya jamii wanaotoa huduma za afya kwenda vijijini kutoa chanjo na elimu ya uzazi wa mpango.

Anasema kuna huduma ya Mkoba ambayo imewasaidia kina mama wa pembezoni (vijijini) kutotembea umbali mrefu kufuata huduma na pia imesaidia kupunguza vifo vya watoto wachanga na wajawazito kwa kuwapatia elimu ya uzazi.

Vifo vya watoto wachanga

Takwimu za afya za Wilaya ya Nyang’hwale, zinaonyesha kuwa mwaka 2017 watoto wachanga 27 walipoteza maisha na mwaka 2018 watoto 26 walifariki dunia na kinamama watano walipoteza maisha wakati wa kujifungua.

Felister Felix ni mratibu wa Afya ya Mama Baba na Mtoto wa Halmashauri ya Mji wa Geita, anasema vifo vya watoto katika halmashauri hiyo vimeongezeka lakini takwimu za vifo ngazi ya mkoa zimepungua kutokana na kampeni ya Mbiu ya Tuwavushe Salama, iliyobuniwa na Halmashauri ya Mji wa Geita.

Kwa ujumla vifo vya watoto mkoani Geita vimepungua kutoka 1,070 mwaka 2016 hadi kufikia vifo 690 mwaka jana.

Takwimu za afya za Halmashauri ya Mji wa Geita zinaonyesha kuwa mwaka 2017, jumla ya watoto 382 walipoteza maisha huku mwaka 2018 watoto 403 wakipoteza maisha katika Halmashauri ya Mji wa Geita.

Felix anasema uelewa mdogo kuhusu umuhimu wa mama kuwahi kliniki, mila potofu na umbali mrefu ni sababu zinazochangia wajawazito kutohudhuria kliniki na wakati mwingine husababisha vifo vya watoto wachanga.

Hata hivyo, anasema uwapo wa watoa huduma ngazi ya jamii, umesaidia wajawazito kuwa na mwamko wa kuhudhuria kliniki na kujifungulia kwenye vituo vya afya. Anasema mwaka 2018 wajawazito 38,088 walihudhuria kliniki, kati yao 1,076 walihudhuria miezi mitatu ya awali.

Ripoti ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) iliyotolewa Februari 2018 kuhusu uhai wa watoto inasema katika nchi za kipato cha wastani vifo vya watoto wachanga ni vifo 27 kati ya watoto 1,000 wanaozaliwa salama. Kwa Tanzania watoto wachanga 39,000 hufariki kila mwaka siku moja baada ya kuzaliwa.

Matumizi ya dawa za kienyeji

Felister anasema licha ya kina mama wanaokuja kliniki kuelimishwa madhara ya kutumia dawa za kienyeji wakati wa ujauzito bado wengi wao hutumia dawa hizo ili kuharakisha uchungu. Anasema matumizi ya dawa hizo huchangia vifo.

Takwimu za mkoa watoa huduma

Mkoa wa Geita una jumla ya watoa huduma ngazi ya jamii wapatao 900 ambao wamesaidia kuelimisha jamii umuhimu wa kuwahi kliniki, kupunguza vifo vya mama na mtoto hasa wakati wa kujifungua.

Rashid Abubakar ni mtoa huduma ngazi ya jamii, Kata ya Ihanamilo, anasema wananchi hawaelewi umuhimu wa mama kuhudhuria kliniki mapema.

Anasema changamoto ni wanaume kuona jukumu la kulea mimba siyo lao bali ni la mama, wakiamini kazi yao ni kuhudumia familia, hivyo kutokuwa tayari kumsindikiza mama kliniki.