MAONI: Itakuwa fedheha Kombe la Kagame likivuka mpaka

Monday June 11 2018

 

Wiki iliyopita, Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) lilitangaza ratiba ya mashindano ya soka ya kuwania Kombe la Kagame, yatakayoanza Juni 29 jijini Dar es Salaam.

Kufanyika kwa mashindano hayo ni baada ya kusimama kwa miaka miwili mfululizo, tangu 2015 na zaidi ni kwa Cecafa kudai kuwa hawakuwa na fedha za kuendesha mashindano hayo.

Kwa sasa Cecafa inafadhiliwa na Azam TV na Rais Kagame na ndiyo sababu za kufanyika mwaka huu.

Timu zitakazoshiriki kutoka Kundi A ni Azam FC (Tanzania), Vipers SC (Uganda), JKU (Zanzibar), Kator FC (Sudan Kusini) wakati Kundi B lina timu za Rayon Sports (Rwanda), Gor Mahia (Kenya), Lydia Ludic (Burundi) na Ports ya Djibout.

Kundi C lina timu za Yanga (Tanzania), Simba (Tanzania), St. George (Ethiopia), na Dakadaha ya Somalia.

Hata hivyo, kuna taarifa za awali kabisa kuwa klabu za Yanga na Gor Mahia zinajitoa kwenye mashindano hayo kwa kuwa zina msongamano wa mashindano.

Yanga imesema inajitoa kwa kuwa inataka kujiandaa na mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia ya Kenya pamoja na kufanya usajili wa maana na pia kusimamia maandalizi ya timu kwa ujumla.

Haijawekwa wazi kama kweli Gor Mahia na wenyewe wanataka kujiondoa ama la, japo imeelezwa kuwa sababu zao ni kama za Yanga.

Tayari Rais wa TFF, Wallace Karia ametoa saa 48 kuitaka Yanga kutengua au kufuta uamuzi huo.

Ukiacha hayo ya Yanga, ni wakati wa timu za Tanzania kujipanga kwa mashindano hayo.

Ilikuwa tuseme kuwa Tanzania inajivunia kuwakilishwa na timu nne, za Simba, Yanga, JKU na Azam, lakini kama hali itakuwa hivyo kwa Yanga, basi Tanzania itabakiwa na timu tatu.

Hata hivyo, kwa Simba, Azam na JKU au hata timu nyingine itakayochukua nafasi ya Yanga endapo itatokea hivyo, zinatakiwa kupambana na kuhakikisha kombe linabakia nyumbani.

Itakuwa fedheha kuona kombe likivuka mpaka kwenda kwenye mataifa mengine huku timu za Tanzania zikitoka bila kitu. Kutwaa kombe, japokuwa si kazi ndogo, lakini kwa maandalizi, kujipanga na wachezaji kujituma hilo linawezekana. Tusema au tuamue kuwa kombe litabaki lakini si kuliachia likivuka mipaka. Ni aibu.

Kufanya hivyo, itakuwa inaakisi hotuba ya Rais John Magufuli aliyoitoa wakati akiikabidhi Simba kombe la ubingwa wa Ligi Kuu aliposema kuwa anataka kuona vikombe vikija au vikibaki Tanzania.

Hiyo ni changamoto ya kuipokea kwa timu zote zitakazowakilisha Tanzania kwenye mashindano hayo ya klabu Afrika Mashariki na Kati.

Baada ya ratiba kutangazwa, timu zote zilizo kwenye mashindano zinatakiwa kuanza maandalizi mapema baada ya mapumziko ya kumalizika kwa Ligi Kuu Bara.

Hakika haitapendeza na ni fedheha kwamba kombe limetwaliwa tangu 2015 na Azam halafu tunaliachia kizembe.

Huu ni wakati wa makocha kukuna vichwa kuangalia wapi ni wapi kwa ajili ya kutengeneza vikosi imara kwa ajili ya fainali hizo. Tunazitakia kila la kheri timu zote katika maandalizi yao.

Huku tukiamini kuwa timu za Tanzania zitafanya vizuri, mashabiki wanapaswa kushiriki kikamilifu kwa kushangilia na kulinda usalama wa timu zote.