Itakuwa vizuri kama mapato yatokanayo na madini yakiwekwa wazi

Hivi karibuni, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi alisema bungeni jijini Dodoma kuwa Serikali haitatangaza hadharani fedha zinazolipwa na kampuni za madini kwa kuhofia kufunguliwa kesi mahakamani kutoka kwa wadai au kampuni zinazoidai.

Alisema kuna watu nje ya nchi walikuwa na madeni na Serikali tangu miaka ya 1970, lakini hawakudai. “Leo hii tunapotangaza kulipwa fedha wanajitokeza kudai madeni yao kwa kufungua kesi mahakamani kwa vile wamejua tuna hela,” alisema. Profesa Kabudi alikuwa akijibu hoja za wabunge waliotaka kujua mwenendo wa mazungumzo kati ya Serikali na kampuni ya Barrick Gold inayotuhumiwa kusafirisha makinikia nje ya nchi kwa kutoa taarifa zisizo za kweli.

Awali, kampuni hiyo iliahidi kulipa fidia ya Dola 300 milioni huku pia ikikubali kulipa hisa za asilimia 16 na mgawo wa asilimia 50 ya mapato ya mauzo ya dhahabu kutoka migodi mitatu inayoimiliki hapa nchini.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Mwenyekiti Mtendaji wa Barrick Gold, Profesa John Thornton kukutana na Rais John Magufuli Ikulu ya Dar es Salaam na baadaye kufanyika kwa mkutano kati ya wajumbe wa Serikali na kampuni hiyo nchini.

Wakati Profesa Kabudi akitoa maelezo hayo, matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya kimataifa ya Financial Secrecy Index (FSI) umeitaja Tanzania kuwa nchi ya 75 kati ya 112 duniani katika viwango cha usiri wa fedha.

Kwa nafasi hiyo Tanzania imepata asilimia 73 jambo linaloashiria kuwapo kwa mwanya wa utoroshaji wa rasilimali yakiwamo madini huku pia kukiwepo mwanya wa utakatishaji wa fedha.

Hatua hiyo inakuja wakati Serikali ikiwa imechukua hatua kali katika sekta ya madini pamoja na kuifanyia marekebisho Sheria ya Madini na kanuni zake.

Hata hivyo, usiri unaogubika mapato ya madini na rasilimali nyingine unaathiri dhamira ya Serikali ya kutaka kupambana na uhalifu katika sekta hiyo, ikiwamo rushwa na utakatishaji wa fedha.

Kwa mfano, katika jitihada za Serikali kupambana na upotevu wa madini, ilifanyia marekebisho Sheria ya Madini ya mwaka 2010.

Katika sheria mpya “The Written Laws (Miscellaneous Amendments) Act, 2017” iliyoanza kutumika Julai 7/2017, kulikuwa na marekebisho kadhaa miongoni mwake ni kuanzisha Tume ya Madini, kufuta Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA), kuongeza malipo ya mrabaha kutoka asilimia nne kwa madini ya metali (mfano dhahabu, shaba, fedha na kadhalika) hadi asilimia sita.

Mengine ni kuongeza malipo ya mrabaha kutoka asilimia tano kwa madini ya almasi na vito hadi sita.

Hata hivyo, sheria hiyo imemnyima Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) upenyo wa kisheria wa kufanya ukaguzi wa hesabu za kampuni za madini ili pamoja na mambo mengine kuwe na uwazi na uwajibikaji usio na shaka kwenye sekta ya madini.

Hapo panatia shaka dhamira ya Serikali. Ni kama vile tunakwenda mbele na kurudi nyuma. Kama kweli Serikali imedhamiria kulinda mapato ya madini, kwa nini ihofie kukaguliwa kwa kampuni za madini?

Tukumbuke pia Tanzania ilijiunga na Mpango wa Uwazi katika Shughuli za Uchimbaji Rasilimali Tanzania (Teiti), Februari16, 2009. Teiti ni chombo kinachojumuisha wadau mbalimbali ambao lengo lao kuu ni kusimamia utekelezaji wa uwazi katika rasilimali madini kwenye mataifa yanayochimba madini.

Mpango huo una wanachama 16 kutoka serikalini, kampuni za mafuta, gesi na madini pamoja na asasi za kiraia. Pamoja na kujiunga na mpango huo, sidhani kama litakuwa jambo jema kwa Serikali kutetea usiri wa mapato ya madini.

Tukumbuke kuwa rasilimali za madini na nyingine ni mali ya Watanzania wote, hivyo wana haki ya kujua nini kimepatikana na kipi kimepotea.

Ni wajibu wa Serikali kuweka wazi mapato hayo na ikiwezekana pia iwe tayari kukiri pale inaposhindwa kufikia malengo.

Isije ikawa Serikali inahofia kukiri kushindwa, lakini kuna mahali upo mwanya unaofanya iwe hivyo.

Hiyo haitawasaidia viongozi wala Watanzania, kwani Waswahili husema “mficha maradhi kifo humuumbua.”

Elias Msuya ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi. 0754 897 287