UCHAMBUZI: Itapendeza siku moja Mtibwa Sugar ikichezea uwanja wake wa kisasa

Monday April 15 2019

 

By Dk Mshindo Msolla

Klabu ya soka ya Mtibwa ni moja ya klabu kubwa nchini na kwa kipindi kirefu imetoa mchango mkubwa katika maendelo ya mpira wa miguu iwe katika ngazi ya klabu, kuwalea wachezaji walionao vizuri, kuwa na utaratibu mkubwa wa kuibua vipaji na kuviendeleza na kuwa na wachezaji wengi katika timu za Taifa za umri tofauti.

Kama hayo hayatoshi, klabu ya Mtibwa imewahi kuwa mabingwa wa Tanzania tena kwa miaka miwili mfululizo na katika msimu wa 2017/2018, Mtibwa ndio walichukua ubingwa wa Kombe la Shirikisho na kuiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa.

Ni jambo la faraja kuuona uongozi wa Mtibwa kwa namna ambavyo umesaidia kuendeleza mchezo huu nchini.

Makala yangu hii ya leo ina lengo la kuuhamasisha uongozi wa Mtibwa kwamba pamoja na mchango wao huo mkubwa, bado uongozi haujaweza kuwa na uwanja wake ambao unakidhi viwango.

Pamoja na mafanikio yote hayo na kuwa katika kiwango cha juu cha uendelezaji wa mpira wa miguu hapa nchini, uwanja wa Manungu hauna hadhi ya klabu hiyo na mafanikio yote hayo ya timu.

Haiwezekani klabu ambayo imechangia maendeleo ya mpira wa miguu kwa kiwango hicho kuwa na uwanja uliozungushiwa mabati tena mabati mengi yakiwa chakavu.

Unapoangalia mechi zinazochezwa Manungu au ukiwa pale Manungu, unashindwa kuamini kwamba huo ndio uwanja wa klabu kubwa kama Mtibwa ambayo imetikisa soka la bongo kwa takribani miongo miwili katika ligi kubwa nchini.

Mara kadhaa ninapokuwa na wageni kutoka nje ya nchi wanaopenda mpira, hutaka kuona mechi za TPL zinazorushwa na Azam TV, mara kadhaa wanapenda kuona mechi za klabu kubwa nchini na mimi huwaeleza kwamba Mtibwa ni moja ya klabu kubwa nchini, hivyo huangalia mechi hizo wakati mwingine zikichezewa Manungu.

Jambo la kwanza ambalo huuliza huwa ni kama kweli uwanja huo wanaochezea ni wa kiwango cha mechi za TPL?

Unapowaeleza historia ya mafanikio ya timu hiyo na idadi ya miaka ambayo klabu hiyo imekuwepo, wanakuwa na maswali ambayo unakuwa huna majibu ya kuwaeleza na wakaridhika.

Naamini uongozi unaiona hali hiyo na ushauri wangu ni huu huu ufuatao;

Kuingia ubia na wadau

Inawezekana gharama za uendeshaji wa klabu unachukua rasilimali nyingi kama si zote ambazo walizipanga kuihudumia timu na hivyo kutoweza kuujenga uwanja kwa wakati mmoja.

Njia mojawapo ambayo inaweza kutumika ni kwa klabu kuingia ubia na mdau/wadau ambaye anaweza akaujenga uwanja kwa muda mfupi ukiwa na mahitaji yake muhimu.

Makubaliano yanaweza kuwa, mathalani, kuchukua mapato yote ya mechi ambazo Mtibwa atacheza hadi hapo gharama zile zitakapokuwa zimerejeshwa.

Naamini kwamba uwanja unaweza ukaisha mapema na malipo ya gharama hizo yakaendelea kulipwa kwa utaratibu huo.

Uongozi kuanza kuujenga uwanja

Uongozi pia unaweza kuanza kuujenga uwanja kwa kuanza na ujenzi wa ukuta kwa awamu kwa kila mwaka na hivyo hatimaye kuumaliza.

Aidha, uongozi unaweza kuanzisha harambee maalumu kwa ajili ya kutafuta fedha za ujenzi wa uwanja na kwa namna ambavyo klabu ya Mtibwa inavyochukuliwa na wadau kwamba ni moja ya klabu zenye uongozi madhubuti, wadau watajitokeza kusaidia katika jitihada hizo za kujenga uwanja.

Naamini kwa dhati kwamba kama uongozi wa klabu ya Mtibwa ukijipanga vizuri, unaweza kuwa na kiwanja cha mpira kinachoendana na hadhi ya Mtibwa.

Moja ya faida kubwa ya klabu kubwa kama ya Mtibwa kuwa na uwanja wake ni kwamba, kwa klabu ya nje ambayo inataka kuwa na uhusiano wa kiushirikiano katika kuendeleza soka, watahitaji klabu ambayo inatambua misingi ya kuendeleza soka, msingi mkubwa ukiwa ni klabu kuwa na uwanja wake unaokidhi vigezo.

Kwa namna Mtibwa ilivyo pamoja na wasifu mzuri wa mchezo huo, naamini klabu ya nje ambayo itakuwa inatafuta klabu za kuwa na mashirikiano nayo, Mtibwa itakuwa ni mmoja wapo.

Kitakachowaangusha ni uwanja wao kutokidhi vigezo na hivyo kukosa fursa kama hizo.