Jifunze kuwa mkweli kwa daktari wako-2

Friday January 18 2019Dk Christopher  Peterson

Dk Christopher  Peterson 

Baadhi ya dalili za matatizo mbalimbali ya kiafya husababishwa na uvutaji wa sigara kama vile kukohoa mara kwa mara, kupungua uzito kwa kasi na maumivu makali ya kifua.

Ni vyema kumwambia daktari kuwa pamoja na dalili hizi pia unavuta sigara kama una tabia hiyo.

Kwa kufanya hivyo utamsaidia daktari kukupangilia tiba ya tatizo lako na kuangalia uwezekano wa kuacha uvutaji wa sigara kwa kuwa ni hatari kwa afya.

Sikufanya tendo la ndoa

Hapa ndipo kwenye tatizo, wagonjwa wengi wanakuwa wagumu kusema ukweli eneo hili, hasa katika tiba ya magonjwa ya zinaa na masuala ya afya ya uzazi kwa ujumla. Sababu kubwa hapa ni aibu. Wengi hujikuta wanapata magonjwa ya zinaa kutokana na tabia kufanya ngono isiyo salama na watu tofauti ndani ya kipindi kifupi. Wagonjwa wengi huwa wazito sana kuwa wawazi kwenye eneo hili, wakijitahidi sana kujaribu kueleza ukweli basi mgonjwa anaweza kusema: “Nilifanya ngono na mshirika mmoja tu mwaka huu.”

Sina magonjwa ya zinaa

Kama una gonjwa lolote la zinaa, unapaswa kukubaliana na ukweli, unaumwa ugonjwa wa zinaa.

Hata kama ulikuwa na gonjwa la zinaa awali, daktari anapaswa kujua hilo. Unaweza kuona aibu kusema hilo, lakini unapaswa kujua ukweli kuwa baadhi ya magonjwa ya zinaa yanaweza kuwa hatari kama hayakupatiwa tiba stahiki. Pia, ni vyema kufahamu kuwa hata kama ulishawahi kuwa na ugonjwa wowote wa zinaa na baada ya muda ukatoweka, upo hatarini kujirudia bila kutibiwa. Ugonjwa unapokurudia unakuwa na hatari zaidi kwa afya ikiwamo kupoteza uwezo wa kuzaa.

Sina tatizo kwenye nguvu zangu za jinsia

Eneo lingine ambalo wagonjwa wangu huwa wanakuwa wagumu sana kusema ukweli ni kwenye suala zima la nguvu za jinsia. Kukosa nguvu za jinsia ni tatizo linaloathiri jinsia zote mbili.

Japo imezoeleka wanaume ndiyo wanaopata tatizo la nguvu za kiume mara nyingi, lakini hutokea hata kwa wanawake kukosa nguvu za kike wakati wa kufanya tendo la ndoa. Hii inaweza kuashiria matatizo mbali ya kiafya kama vile shinikizo la damu (yaweza kuwa la juu hata la chini), kisukari na magonjwa na mengine.

Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ.