Jinsi wazazi wanavyowadunga watoto sindano kuzuia mimba

Friday January 18 2019

 

By Florence Majani, Mwananchi

Ingawa kuna madhara lukuki yanayosababishwa na ngono zembe ikiwamo kupata maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), baadhi ya wazazi wa kijiji cha Nambilanje, wamekiri kuwachoma sindano za uzazi wa mpango, watoto wao wa kike wenye umri wa kuanzia miaka 11 , ili kuwazuia kupata ujauzito.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa habari hii umebaini kuwa, wazazi wameamua kuwapa watoto wao wa kike njia za uzazi wa mpango hasa sindano, wakidai kuwa ni bora kuwazuia kupata ujauzito kuliko kuacha shule.

Mganga mfawidhi wa zahanati ya Nambilanje, Dk Samwel Mathias anasema kwa siku, anapokea wazazi kati ya wawili hadi watatu, wanaotaka huduma ya mabinti zao kuchomwa sindano za kuzuia mimba.

“Mabinti wengine wanaoletwa kuchomwa sindano, wana miaka 11 hadi 12, mimi huwakatalia, lakini hata nikiwakatalia, wanaenda kuchoma sindano kwenye maduka ya dawa,” anasema Dk Mathias.

Anasema tangu aanze kufanya kazi katika kijiji hicho, ameshuhudia mila nyingi za kushangaza ikiwamo wajawazito kufungwa kamba nyeusi kiunoni, lakini hilo la kuwachoma mabinti sindano limeenea kwa kiasi kikubwa na imekuwa kama mtindo.

Dk Mathias anasema kati ya wazazi wote wanaokwenda hospitali, ni wanne tu waliokubaliana naye na kuahirisha kuwachoma watoto sindano hizo.

“Wenyewe hawataki njia nyingine za uzazi wa mpango, hawataki kitanzi, kijiti, mipira ya kiume wala vidonge wanataka sindano tu. Lakini kwa uelewa wangu sindano ndiyo yenye mzigo mzito wa sumu, ina maana ina madhara makubwa,” anasema Dk Mathias.

“Sindano ya uzazi wa mpango ina milligram 150, hivyo kila baada ya miezi mitatu, binti anaingiza dawa hiyo katika viungo vyake vya uzazi. Ina maana akifikisha miaka 30 au 40 atakuwa salama kweli?”

Alipoulizwa msemaji wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Catherine Sungura kuhusiana na vitendo vya wazazi kuwapeleka mabinti zao kuchoma sindano za kuzuia mimba, alisema hilo ni suala binafsi.

Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile alisema hana taarifa kuhusu vitendo hivyo na kuahidi kufuatilia.

Wakizungumza wakati wa mafunzo ya wanakamati za ulinzi na usalama za kuzuia ukatili wa kijinsia yaliyoandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa), baadhi ya kinamama walikiri kuwachoma watoto wao sindano.

“Ni bora nimchome sindano ili asiniaibishe, kwa sababu akipata mimba akiwa shuleni, ataacha shule na Rais ameshasema wanafunzi wakipata mimba hawarudi shule,” anasema Asia Misale mkazi wa Nambilanje.

Mwanamke mwingine, aliyeomba jina lake lihifadhiwe, mkazi wa Nambilanje alisema kinachochochea wazazi kuwachoma sindano za uzazi wa mpango wasichana ni kwa sababu wanaanza kufanya vitendo vya ngono wakiwa na umri mdogo na mzazi wakati mwingine anashindwa kumdhibiti.

“Hujui lini kavunja ungo, anajificha sana, pindi unapojua (kama kavunja ungo) anakuwa tayari kashaanza michezo hiyo, sasa sisi kinamama tukibaini tu kakua, basi haraka sana hospitali ili asije kuzaa zaa hovyo,” anasema.

Mkazi mwingine, Rehema Lingwindi anasema kila aendapo kliniki kumpeleka mtoto wake, anashuhudia wasichana wadogo wengine wenye miaka kati ya 11 na 12 wakiingia kwa daktari wa kinamama na kuomba huduma ya njia za uzazi wa mpango.

Kati ya kinamama 13 waliozungumza na mwandishi wa habari hii, 11 walikiri kuwachoma sindano mabinti, mmoja alisema hana mtoto wa kike na mwingine alisema hajui kuhusu suala hilo.

Ofisa Maendeleo wa Wilaya ya Ruangwa, Rashid Namkulala anasema suala hilo linahitaji mjadala mkubwa na elimu ya kutosha.

“Kiafya sheria hazizuii kutumia njia za uzazi wa mpango, lakini pindi mtoto anapotumia akiwa katika umri mdogo, basi linaweza kuleta madhara makubwa,” anasema Namkulala

Ofisa huyo, anawaasa wanafunzi na watoto wengine wa kike wa kata hiyo, kuacha kutumia uzazi wa mpango wakiwa katika umri wa mdogo.

Mwalimu wa Taaluma wa Shule ya Sekondari Nambilanje, Takiyu Mutafungwa alisema watoto wa kijiji hicho wanaanza kufanya vitendo vya ngono wakiwa katika umri mdogo na hawaogopi.

“Kinachowapa jeuri ni hizo sindano za uzazi wa mpango ambazo wamehalalishiwa na wazazi wao. Ina maana mzazi akishamchoma mtoto sindano, ndiyo karuhusu hivyo vitendo,” anasema mwalimu Mutafungwa.

Anasema wazazi wa kike ndiyo wanaoshirikiana na watoto wao kutoa mimba na wengine wanawafahamu wanaume wanaoshiriki ngono na watoto wao, lakini hawachukui hatua.

Wanafunzi wa shule ya Sekondari Nambilanje, walikiri kuwa wenzao wengi wanatumia sindano hizo.

Nasma Juma, mwanafunzi wa kidato cha nne, anasema wazazi wanawasaidia watoto wao wa kike kuchoma sindano lakini wanafunzi nao wanapata ujuzi kupitia makundi.

“Mzazi anapojua tu mtoto kavunja ungo, anampeleka kwa daktari, wakati huo hata mtoto mwenyewe hajui kwa nini anachomwa sindano. Hata anapokuja kujua kwa nini alichomwa hiyo sindano, anakuwa kashazoea naye anaendelea,” anasema mwanafunzi huyo.

Anasema wanafunzi wenzake wanapokaa katika makundi husimuliana namna wanavyochoma sindano hiyo na wapi huduma hiyo inapatikana.

“Yaani wanavyosema kama ukikosa kwa daktari, unaenda kwenye duka la madawa unalipa Sh2,000 tu,” anasema.

Walimu wanane waliozungumza na mwandishi wa habari hii, walikiri kufahamu kuhusu tabia hizo za wazazi kuwachoma sindano mabinti au mabinti kufanya hivyo wenyewe.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nambilanje, Liberat Kinyaiya anasema wanafunzi wanaanza kutumia sindano hizo tangu wakiwa shule za msingi.

“Hizo kesi ni nyingi, tunazisikia siyo mara moja au mbili, lakini ni siri kati ya mama na mtoto na ni vigumu kuona kwa macho,” anasema na kuongeza:

“Kwa namna moja au nyingine sindano hizi zinaweza kuwapa athari kiafya, kwa mfano saratani ya mlango wa kizazi na hata wakati mwingine, pindi anapofikia umri wa kutaka kupata watoto, anakosa watoto.”

Anasema akiwa mlezi wa wanafunzi, anatumia vipeperushi na majarida ili kuwaelimisha wanafunzi kuhusu madhara yanayotokana na uzazi wa mpango.

“Pia tunahimiza na kutoa elimu kwa watoto wasijamiiane kabla ya umri ili kujikinga na mimba,” anasema.