KAKAKUONA : TBA kama imeshindwa ifumuliwe iundwe upya

Muktasari:

  • Rais alipofanya ziara ya kushtukiza katika mradi huo ambao alishatoa Sh10 bilioni aliongea kwa uchungu na kisha kuwanyang’anya TBA mradi huo na kuwakabidhi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Wiki iliyopita nilifarijika nilipomuona Rais John Magufuli akiwatimua Wakala wa Majengo (TBA) katika ujenzi wa nyumba za Askari wa Gereza la Ukonga Jijini Dar es Salaam.

Nimefarijika kuona kuwa Rais naye ameona mapungufu makubwa ya TBA ambayo naweza kusema hili si jipu, bali ni embe ng’ongo. Yaani ni kama TBA wamelewa sifa wasizostahili.

Embe ng’ong’o lina sifa kuu moja, ukilitizama linavutia na utadhani lina minofu mingi lakini utakapolipasua, utakutana na kokwa kubwa kuliko minofu inayolingana na ukubwa wake.

Hii haina tofauti na TBA kwa sababu ni dude kubwa ambalo liliaminiwa na Serikali lakini miradi mingi iliyosimamiwa nalo ama imejengwa chini ya kiwango au imekamilishwa nje ya muda uliotengwa.

Rais alipofanya ziara ya kushtukiza katika mradi huo ambao alishatoa Sh10 bilioni aliongea kwa uchungu na kisha kuwanyang’anya TBA mradi huo na kuwakabidhi Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

“Nimechoka sitaki manenomaneno. Kanali (wa JWTZ) simamia hii kazi. Ulijenga Mirerani, umejenga nyumba 45 kule Dodoma za makao mkuu, hutashindwa nyumba hizi,” alisema Rais Magufuli.

Aliongeza: “Jenga siku tukiwakabidhi Magereza wafurahie nyumba zilizojengwa na jeshi. Inawezekana siku moja wataanza kujifunza kuona aibu.

“Lakini siku moja wasije wakashangaa (Magereza) kuona namteua mkuu wa magereza kutoka JWTZ. TBA gani mbona nyumba haziishi. Kuanzia leo msionekane hapa mkatafute site nyingine.

“Kazi za TBA hazimaliziki. Pale Magomeni bado kazi haijakamilika. Mjione aibu chombo cha Serikali mnapopewa pesa hamfanyi kazi.”

Kauli za Rais ni mwendelezo wa malalamiko dhidi ya utendaji wa TBA na hii haina maelezo mengine zaidi ya kufanya kazi kwa mazoea.

Hii si mara ya kwanza Rais kukutana na kadhia ya TBA kwani Machi 3, 2015 wakati huo akiwa Waziri wa Ujenzi alieleza kukutana na madudu katika ujenzi wa ofisi za wakuu wa wilaya za Hai na Moshi.

Alisema kuwa ‘slab’ ilitakiwa ijengwe milimita 175 katika majengo yake imejengwa milimita 150 na hata malighafi haikuwa imefikia kiwango kinachotakiwa.

Januari 23, 2018 Waziri mkuu Kassim Majaliwa alimwagiza mkurugenzi mkuu wa TBA kufanya tathmini ya ubora wa jengo la kituo cha pamoja cha Forodha Sirari kilichojengwa na TB mkoani Mara.

Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jafo, naye Juni 15,2018 aliagiza TBA kurudia ukarabati wa sakafu za madarasa ya sekondari kongwe ya Malangalali, baada ya kubaini zilijengwa chini ya kiwango.

Ndio maana nimeanza kwa kumwambia Rais Magufuli kuwa TBA sio jipu tu bali ni embe ng’ongo na anahitaji kuifumia na kuisuka upya na ikibidi iwe ni kitengo ndani ya JWTZ inayoonyesha ufanisi.

Mheshimiwa Rais, kwa hili la TBA hakika nakupongeza ila ongeza ukali zaidi na kama ukiona inakupendeza shirikisha pia sekta binafsi chini ya Bodi ya Wakandarasi (CRB).