UCHAMBUZI: Kauli ya Mbowe kuhusu ofisi kila wilaya ijitosheleze

Muktasari:

  • Kupitia chama hicho Chief Karumuna ni meya wa manispaa hiyo pengine akiwa ndiye meya kijana mwenye mvuto zaidi kwa sasa unapotaja suala la uwezo wa kupambana na kumiliki jukwaa.

Utapata tabu sana kutafuta ilipo ofisi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Manispaa ya Bukoba, chama kinachoongoza baraza la madiwani na kupitia chama hicho, Wilfred Lwakatare ni mbunge wa Bukoba Mjini.

Kupitia chama hicho Chief Karumuna ni meya wa manispaa hiyo pengine akiwa ndiye meya kijana mwenye mvuto zaidi kwa sasa unapotaja suala la uwezo wa kupambana na kumiliki jukwaa.

Siyo jambo linalotarajiwa kwa chama kilichopewa hadhi na wananchi kwa kuwa na idadi kubwa ya madiwani na kufanikiwa kumsimika meya na mbunge halafu ofisi zake ziwe eneo lisilojulikana.

Hivi karibuni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe aliagiza uongozi wa chama hicho kila wilaya kuhakikisha ifikapo mwaka 2020 kuwe na ofisi na kuondokana na adha ya kupanga.

Akiwa wilayani Tarime mkoani Mara ambapo alikagua jengo lenye vyumba vitatu vya ofisi, alisema hatua hiyo itapunguza gharama ya majengo ya kupanga.

Kauli ya mwenyekiti huyo ikichukuliwa kwa uzito unaojitosheleza inaweza kuwa mwanzo wa kufunika aibu inayoonekana kwenye majengo mengi ya kupanga yanayotumiwa na viongozi wa chama hicho. Kwa baadhi ya wilaya unaweza kupata shida kuamini kama kweli majengo yanayotumiwa kuwa ofisi za chama hicho ni kweli wanapanga na kulipa kodi au wamepewa na wasamaria wema waendeshe shughuli zao.

Kwenye maeneo mengine majengo yanayotumika kama ofisi ni mali binafsi za wanachama baada ya kuyatoa yatumike kama mchango wao wa kuimarisha demokrasia. Pale wanapoamua kurejea CCM ni hapo jengo lenye ofisi ya Chadema huwa limefungwa. Kutumia majengo yaliyochoka na sehemu nyingine viongozi kuendesha shughuli za chama kwa kutumia ofisi zao binafsi ni mambo yanayotumiwa na mahasimu wao kisiasa kuwadhoofisha.

Chama kisichokuwa na uwezo wa kuwa na jengo lake la ofisi kila wilaya, wakati wa uchaguzi ni ajenda inayoweza kupimwa kwa uzito mkubwa na wapiga kura ambao wanaweza kupoteza imani na kuhoji umakini wa chama hicho kupewa dola.

Ni vigumu kueleweka wakati wa kuhubiri sera na mipango mizuri ya maendeleo baada ya kukamata dola ilhali kwenye vijiji, kata, wilaya na miji hauna makazi ya kudumu ya chama kuendeshea shughuli zake.

Ni katika hatua hii ambapo ajenda ya ruzuku inayopokewa na chama kutokana na idadi ya wabunge kinaopata inapoibuka na wananchi kuwa na kiu ya kujua ni mambo yapi ya kipaumbele hupewa nafasi ya kwanza.

Inawezekana ruzuku imeangaliwa na mambo mengi ya kuimarisha chama, lakini fungu hilo haliwezi kuwa dogo kiasi cha kuishia kulipia kodi kwenye baadhi ya majengo yanayokodiwa na chama hicho.

Maeneo ya vipaumbele ingekuwa ni pamoja na wilaya zenye wabunge wa chama hicho kujengewa ofisi kutokana na mchango wa ruzuku inayopatikana kupitia kwa mbunge husika.

Hiyo itakuwa ni njia ya kukijenga chama na kukiwekea msingi wa kujitegemea na kuwa na sauti katika eneo lake, tofauti na ilivyo sasa ambapo majengo yanayotumika hayalingani na hadhi waliyopewa wagombea wa chama hicho na wapigakura.

Chama chenye jengo la ofisi inayofanya kazi muda wote hakiwezi kupata aibu ya wagombea wake wa udiwani kuenguliwa kwa sababu tu ya kushindwa kujaza vyema fomu za kuomba kuteuliwa kugombea kama ilivyotokea kwa wagombea wa Chadema.

Makosa kama haya yanatokea kwa sababu maeneo mengine hakuna ofisi ambayo mgombea anaweza kukutana na viongozi wakaelekezana na kujisahihisha kabla ya uwasilishaji wa fomu.

Hivyo agizo la Mbowe kuwa chama hicho kiwe na ofisi kila wilaya iwe ni kauli inayojitosheleza na viongozi wa chama hicho waone kuwa wana wajibu kuhakikisha jambo hilo linatekelezeka.

Phinias Bashaya ni mwandishi wa gazeti la Mwananchi mkoani Kagera