MAONI: Kero, lawama zimezidi uchaguzi serikali za mitaa

Sunday November 3 2019

Tangu kuanza kwa uchukuaji fomu za wagombea wa nafasi za uongozi wa serikali za mitaa, lawama zinatolewa kila siku na kibaya zaidi zinaongezeka huku baadhi ya taarifa zikihusu mapigano baina ya wafuasi au mgombea kupigwa.

Malalamiko dhidi ya ukiukwaji wa taratibu yamekuwa mengi na yanatoka kila kona ya nchi. Baadhi wanalalamika kuwa watoaji fomu, yaani wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wamekuwa wakiingia ofisini kuwasubiri wagombea wa chama kimoja tu. Wanapofika wanawapa fomu na kutoweka.

Wakati wagombea wa vyama vingine wanapofika hawakuti mtu ofisini.

Wengine wanalalamikia kupewa fomu zisizokamilifu na hivyo kuhofia kuenguliwa mwishoni kwa hoja kwamba hawakujaza fomu sahihi au fomu zao zina mapungufu. Sehemu nyingine wanalalamikia vitendo vya wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi kuwapa fomu watu wanaojibambikia vyama bila ya kuangalia kama wana vielelezo vya kutosha vinavyostahili kutambulika kama wagombea.

Wapo wanaolalamika kuwa wagombea wao walipigwa au kupokea vipigo wakati wakienda kuchukua fomu na wengine kukamatwa.

Kwa kifupi, lawama dhidi ya wasimamizi zimekuwa nyingi na ingawa Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo amekiri kuwepo udhaifu, hakuna hatua kubwa za kisheria zilizochukuliwa kuwaogopesha wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ili warudi katika njia sahihi.

Advertisement

Kauli nyingine kama ya Naibu Waziri wa Tamisemi, Mwita Waitara kuwa kutoonekana ofisini kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wakati wagombea wa upinzani wakienda kuchukua fomu kunatokana na watu hao kuwa na majukumu mengine, haiweki uwajibikaji wa kutosha kwa watendaji hao.

Badala yake kauli hiyo inatoa mwanya zaidi kwa wasimamizi hao kutoonekana ofisini kwa sababu wana majukumu mengine.

Na ndio maana chama kama ACT Wazalendo kimetoka na tamko kuwa kinachoendelea katika mchakato huo si dosari, bali ni hujuma. Hii inatokana na chama hicho kuona hakuna hatua zinazochukuliwa kuwawajibisha wasimamizi wanaowanyima fomu wagombea kwa njia ambayo si sahihi.

Kitu kikubwa katika uchaguzi wowote ule ni wadau kuwa na imani nao. Na imani kwenye uchaguzi inakuja pale wadau wanapoona sheria na kanuni zinafuatwa, hakuna upendeleo kwa baadhi ya wagombea, dosari zinarekebishwa haraka na uchaguzi una uwazi ambao unaruhusu kila mdau kujua kinachoendelea.

Lakini hayo yanapokosekana ndipo jitihada binafsi zinapoanza. Vyama kutafuta njia za kuhakikisha vinatendewa haki, kuamua kulinda wagombea wao, kulinda kura zao kulazimisha kupewa au kuona taarifa muhimu za uchaguzi na masuala mengine mengi.

Matokeo yake ni mapambano dhidi ya waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi ambao ni lazima wataomba nguvu ya dola na mwishoni huwa ni vurugu.

Taifa letu lilijipatia uhuru wake kwa hoja za mezani na si kwa vurugu na hivyo linastahili kuendelea kufanya mambo yake kwa hoja za mezani na si vurugu. Haki aliyotupokonya mkoloni tuliirudisha kwa nguvu ya hoja na hivyo ni lazima tuendeleze utamaduni huo ili Taifa liendelee kuwa la amani na utulivu.

Ni muhimu basi kwa Serikali kuamua kukomesha matukio yanayolalamikiwa na wadau ili uchaguzi usijae matukio yanayoweza kuondoa amani na utulivu tulionao.

Wadau wangependa kuona matukio haya yanapungua kwa kiwango kikubwa ili kutotoa mwanya kwa mtu yeyote kutaka kufanya vurugu mwishoni mwa mchakato kwa madai kuwa haki haikutendeka.

Serikali za mitaa ni ngazi muhimu kwa wananchi kwa kuwa ndiyo iliyo karibu nao zaidi. Na kwa sababu watu wanajuana kwa kiwango kikubwa, wanajua nani anaweza kuwaongoza vizuri hivyo utaratibu wa vyama usiwaondolee haki yao ya kuchagua mtu anayewafaa na anayejua matatizo yao.