Kila la kheri wawakilishi wetu Serengeti Boys

Sunday April 14 2019

 

By Mhariri

Timu ya Taifa ya Vijana ya Serengeti Boys leo itaanza kutupa karata yake ya kwanza kwa kupambana na Nigeria kwenye Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Serengeti Boys na Nigeria ndio watakaofungua pazia la michuano hiyo ya vijana wa chini ya umri wa miaka 17 (U-17) na mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Wawakilishi hao wa Tanzania watapeperusha bendera ya Taifa baada ya timu ya Taifa, Taifa Stars kuifunga Uganda Cranes na kufuzu fainali za Afcon ambazo zitafanyika nchini Misri.

Baada ya matokeo hayo, nguvu ya Watanzania imeelekezwa leo kwa Serengeti Boys inayowania kufuzu Fainali za Kombe la Dunia.

Watanzania wote kama ilivyokuwa kwenye mchezo wa Taifa Stars na Uganda Cranes, macho na masikio yao yatakuwa kwenye Uwanja wa Taifa.

Ni vema Watanzania wakaungana kuwasapoti wawakilishi wetu wengine katika mashindano ya kimataifa kama ilivyokuwa kwa mchezo wa Taifa Stars na Uganda Cranes.

Watanzania wana matumaini na Serengeti Boys ambayo ina rekodi nzuri ya kushinda, mfano ilipoweza kuifunga Congo Brazzaville kwa mabao 3-2 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Taifa.

Kikosi hicho kinachonolewa na kocha, Bakari Shime, kitashuka dimbani mbele ya maelfu ya mashabiki wa soka watakaokuwapo uwanjani hapo kuisapoti timu yao.

Matumaini ya Watanzania kwa Serengeti Boys ni makubwa hasa ukichukulia kwamba iliwahi kuwa mabingwa wa Kombe la Vijana la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati Cecafa ya mwaka 2017.

Serengeti Boys walitwaa ubingwa baada ya kuwalaza Somalia mabao 2-0 katika mechi ya fainali iliyochezewa mjini Bujumbura nchini Burundi.

Kinachotakiwa ni kushinda mchezo huo ili kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kufanya vizuri katika mashindano haya makubwa yanayofanyika nchini Tanzania kwa mara ya kwanza.

Tumeshuhudia ahadi iliyotolewa juzi na Mlezi wa timu hiyo Reginald Mengi kwamba atatoa Sh20 milioni kwa kila mchezaji endapo watashinda mechi mbili katika mashindano haya, hivyo tunaamini ahadi hiyo itawatia moyo wachezaji na kuliletea ushindi taifa.

Pia,Mkuu wa Mkoa wa Dar es Saalam, Paul Makonda aliwaeleza wachezaji hao kwamba kama watashinda mechi mbili watakuwa wamemuwakilisha vema mlezi wao Reginald Mengi.

Taifa Stars ilipoishinda Uganda Cranes, Rais John Magufuli aliwapa zawadi wachezaji wa timu hiyo kwa kila mmoja kupata kiwanja kwa ajili ya ujenzi wa nyumba jijini Dodoma.

Zawadi na ahadi zinazotolewa inaonyesha ni namna gani viongozi na Watanzania wanavyopenda michezo na kutaka timu zetu zishinde kwenye michuano ya kimataifa.

Msisitizo wetu ni kwa wachezaji kucheza kwa kujituma muda wote wa mchezo, kuhakikisha wanapata matokeo mazuri kwa mchezo huo.

Kinachotoa matumaini ni kwamba wachezaji wetu wanacheza kwenye uwanja wa nyumbani hivyo ni nafasi ya kufanya vizuri mbele ya mashabiki wake.

Tunafahamu kuwa Watanzania ni wapenda michezo ni wazi watakuwa nyuma ya timu yetu kwa ajili ya kuwapa sapoti.

Kingine ambacho wachezaji wanaweza kujidai nacho ni mazingira na hali ya hewa waliyoizoea.

Tunawatakia kila la kheri wachezaji na mabenchi ya ufundi kuhakikisha kuwa wanacheza kwa kujituma, nguvu na akili kupata matokeo ambayo tunaamini yataipaisha Tanzania kwenye medani ya soka kimataifa. Watanzania wote tuungane katika kuitakia kila la kheri timu yetu ya Serengeti Boys inayofungua pazia la Afcon leo. Mungu Ibariki Tanzania, Mungu ibariki Serengeti Boys.