UCHAMBUZI: Kocha mpya wa Taifa Stars aje na mkakati wa kuwanoa wazalendo

Tuesday July 30 2019

 

Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ ipo kwenye harakati za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaoshiriki Ligi za Ndani (Chan) na jana ilicheza dhidi ya Kenya kwenye mechi ya kwanza.

Timu hizo zitarudiana Nairobi, Agosti 4 na ile ambayo itapata matokeo mazuri kwenye mechi hizo mbili, itafuzu hatua inayofuata ya mashindano hayo.

Lakini wakati Stars ikiwa kwenye mapambano ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za Chan ambazo zitafanyika mwakani nchini Cameroon, Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) lipo kwenye mchakato wa kumsaka kocha mpya wa kudumu wa timu hiyo.

Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya usimamizi wa kocha wa muda, Etienne Ndayiragije baada ya kutimuliwa kwa Emmanuel Amunike mara baada ya Stars kufanya vibaya kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) ambako ilishika mkia baada ya kupoteza mechi zote tatu, ikifunga mabao mawili na kufungwa manane.

Kwa mujibu wa Rais wa TFF, Wallace Karia na Katibu wake, Wilfred Kidao, takribani makocha 100 wametuma maombi ya kuinoa Taifa Stars ambao wote ni raia wa kigeni.

Uwingi wa maombi hayo unatoa taswira kwamba soka la Tanzania ni bidhaa ambayo imeanza kuwa adimu na Taifa Stars ni timu ambayo imekuwa ikiwapa tamaa makocha kuinoa.

Advertisement

Kundi hilo la makocha 100 na wengine ambao wataendelea kutuma maombi siku za usoni, hapana shaka kwamba wana sifa, ubora, tabia na mbinu tofauti za kiufundi.

Upo ulazima kwa kamati ya ufundi na ile ya utendaji ya TFF, kuendesha na kusimamia mchakato wa kumsaka kocha mkuu mpya wa Stars kwa umakini wa hali ya juu badala ya kufanya kwa pupa jambo ambalo litaleta hasara na majuto siku za usoni.

Kocha mpya anayehitajika kwa sasa kwanza anapaswa kuwa na ufahamu na uzoefu wa kutosha wa soka la Afrika na ni lazima awe ameshafundisha katika mazingira ya bara hili kwa muda wa kutosha.

Kingine kinachohitajika kwa huyo kocha mpya atakayepatikana ni yule ambaye ana elimu na wasifu mkubwa na unaoeleweka na kufahamika wa ukocha na sio vinginevyo.

Hilo litamfanya kuheshimika na kupata mwitikio chanya kutoka kwa wachezaji lakini hata mashabiki jambo ambalo litamwezesha kutimiza majukumu yake pasipo kuingiliwa na pia kuheshimika na wachezaji pindi anapokuwa anafanya nao kazi.

Lakini pia tunahitaji kocha ambaye atakuwa chachu ya maendeleo kwa makocha wazawa kwa maana kwamba anapaswa awe mkufunzi wa walimu wa hapa nyumbani.

Ikumbukwe kwamba kocha wa timu ya taifa anafanya kazi na kuishi na wachezaji kwa muda mfupi kulinganisha na wenzake wa klabu ambao hao ndio huwaandaa wachezaji kwa ajili ya kuwatumia kwenye timu yake.

Kama makocha hao watakuwa na uwezo duni, maana yake watazalisha wachezaji wasio na ubora kwenda kuchezea timu ya taifa, jambo litakalosababisha ipate matokeo mabovu na yasiyoridhisha.

Upo mfano mzuri wa makocha wa timu ya taifa ambao waliwahi kuja hapa nchini na wakawa chachu kwa wale wazawa kutokana na programu mbalimbali za kuwapiga misasa ambazo waliziendesha kwa nyakati tofauti.

Mfano wa makocha hao ni Marcio Maximo, Jan Poulsen na Kim Poulsen ambao kwa nyakati walizofundisha timu ya taifa, waliweza kuimarisha ubora wa baadhi ya makocha wazawa.

Hakuna haja ya kuleta kocha ambaye atajitazama mwenyewe na kisha baadaye akaondoka huku akiwa hajaacha chochote kwa makocha wetu ambao wengi tuna ndoto na mategemeo ya kuwaona wakipiga hatua kubwa siku za usoni.

Mamlaka za shirikisho ambazo zina jukumu la kumsaka kocha mpya, zinapaswa kufahamu kwamba kuna mabadiliko makubwa ambayo yametokea kwenye mchezo wa soka ulimwenguni katika miaka ya karibuni.

Mabadiliko hayo yamesababisha hata makocha kuwa na majukumu mengi ya nje na ndani ya uwanja kuliko yale yaliyozoeleka kwa muda mrefu ya kupanga kikosi na kusimamia timu kwenye mechi na mazoezi.

Si vibaya kama wakaomba msaada kwa wataalamu wa ufundi wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) na Afrika (CAF) ili kupata kilicho bora.