Kilimo bora kinahitaji sekta binafsi imara

Thursday August 30 2018

 

By Elias Msuya, Mwananchi [email protected]

Tangu Tanzania ilipopata uhuru, kilimo kimekuwa na mchango mkubwa kwenye uchumi wa Taifa hata kaya ingawa kwa siku za karibuni kimekuw akikikabiliwa na changamoto kadhaa.

Takwimu zinaonyesha sekta hiyo inaajiri watu wawili katika kila watatu huku ikichangia asilimia 30 ya Pato la Taifa (GDP) ingawa kumekuwa na changamoto za uwekezaji hata bajeti inayotengewa.

Kutoakana na mwenendo huo, ukuaji wa sekta ya kilimo umekuwa wastani wa asilimia 3.4 kati ya mwaka 2011hadi 2015 wakati uchumi kwa ujumla ukikua kwa wastani wa asilimia 7.0.

Elias Msuya amefanya mazungumzo na mkurugenzi wa sera, mipango na utetezi wa Baraza la Kilimo Tanzania (ACT), Timothy Mmbaga kuzungumzia mustakabali wa sekta hiyo.

Swali: Baraza linafanya nini kuinua kilimo nchini?

Jibu: Majukumu yetu ni kuwaunganisha wadau wa sekta ya kilimo, kufanya utetezi na kujenga uwezo na uwakilishi kwa wanachama wetu.

Advertisement

Wadau wetu ni pamoja na vikundi vya wakulima, wafugaji, wasindikaji, wafugaji, wavuvi, kampuni na taasisi za uzaliohaji na usafirishaji wa mazao.

Tunafanya ushawishi katika sera zinazowahusu wanachama wetu. Wakati Baraza linaanzishwa lilikuwa na wanachama 30 ila sasa linao zaidi ya 170.

Kazi yetu ni kuyajumuisha mambo yatakayozungumzwa na kuyafanyia utafiti kisha tunayapeleka serikalini ili kuyatafutia ufumbuzi.

Swali: Watanzania wengi wanakitegemea kilimo, baraza limesaidia nini kusukuma mbele gurudumu la sekta hiyo?

Jibu: Wakati tunapata uhuru miaka ya 1960 kilimo kilikuwa kinachangia mpaka 90 kwenye pato la Taifa ila sasa hivi tunazungumzia takriban asilimia 20.

Wakati huo Tanzania ilikuwa inaongoza kwa uzalishaji wa mkonge duniani na mazao mengine ya biashara kama kahawa na korosho. Kilimo kilikuwa kipeumbele cha Taifa.

Lakini, tulipoingia kwenye mfumo wa soko huria na kushuka kwa sera ya ujamaa na kujitegemea kila mtu akawa anafanya lake kiasi cha baadhi ya vituo vya utafiti kufungwa kabisa, wataalamu wa kilimo wengi hawakuajiriwa.

Wadau walikaa na kutafakari suala hilo na wakakubaliana kuazisha baraza litakaloleta msukumo mpya kwenye kilimo. Mwaka 1999 lilianzishwa wakati huo likijulikana kama Chamber of Agriculture and Livestock na 2000 likazinduliwa na Rais Benjamin Mkapa.

Swali: Umesema awali kilimo kilikuwa kikichangia asilimia 90 katika pato la Taifa. Kwa nini tumefika tulipo na nini athari yake?

Jibu: Kilimo kinaweza kufanya vizuri lakini mchango wake kwa Taifa ukawa mdogo. Hiyo ni kwa sababu sekta nyingine zimeimarika sana siku hizi tofauti na zamani.

Tulipopata uhuru mchango wa kilimo ulikuwa karibu asilimia 90, lakini baada ya sekta nyingine kujulikana kilimo kikashuka. Kwa mfano leo kuna gesi, utalii na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano zinazoshindana na kilimo.

Tunazungumzia mapato yanayopatikana katika sekta ya utalii, madini, gesi, mapato yatokanayo na sekta ya mawasiliano, haya yote yanapita kilimo.

Kwa hiyo mchango wa kilimo katika uchumi wa Taifa siyo kitu. Suala ni kilimo kinakuwa kiasi gani. Tunapozungumzia uchumi tunaangalia ukuaji siyo mchango. Kwa sasa tuna matatizo yote mawili kwanza ni kushuka kwa ukuaji na mchango wake kwa Taifa.

Swali: Licha ya ukweli kwamba kuna sekta nyingine zenye mchango mkubwa katika pato la Taifa, kilimo kinategemewa na Watanzania wengi zaidi. Nini kifanyike ili wafaidike zaidi?

Jibu: Kwanza bajeti ya Serikali kwenye kilimo iongezeke. Hii ndio sababu ya viongozi wa Afrika kukutana na kukubaliana kutenga walau asilimia 10 ya bajeti nzima ya Serikali kwa ajili ya kilimo.

Jambo la pili tuwe na kilimo cha umwagiliaji. Tanzania inapata mvua nyingi lakini hazinyeshi kwa muda mrefu. Serikali inapaswa kujenga miundombinu. Yakiwepo mabwawa makubwa ya kuvuna maji ya mvua, sekta binafsi itavutika kuwekeza.

Mtu akiona anaweza kumwagilia eka 20,000 hadi 30,000 lazime atakwenda kuwekeza. Hiyo ni miradi mikubwa ya umma ambayo sekta binafsi haiwezi kuitekeleza peke yake.

Jambo jingine ni lazima kuwe na mazingira mazuri ya kufanya biashara. utaratibu wa leo mtu analima lakini kunakuwa na uhaba wa mbolea au mbegu ghali halafu muda wa kuuza anaambiwa haruhusiwi ni tatizo.

Tukifanya hivyo tutaweka mazingira mazuri kwenye kilimo.

Jambo jingine ni kukifanya kilimo kuwa cha biashara. utaratibu huo utasaidia kuwasajili wakulima kama walivyo wafanyabiashara.

Ndiyo maana hata kwenye mfumo wa mbolea za ruzuku, fedha ziliibwa kwa kuwa wakulima hawajasajiliwa. Wakulima wakisajiliwa watahudumiwa kwa urahisi.

Swali: Tangu kuanzishwa kwa baraza hili limetoa mchango gani kutatua kero za kilimo?

Jibu: Mara nyingi huwa tunapiga kelele bajeti ya kilimo iongezwe.

Mwaka 2010/11 bajeti ya kilimo ilifikia asilimia 7 na matrekta mengi yalinunuliwa na Jeshi la Kujenga Taifa kupitia Shirika lake la Uchumi (Suma JKT) ili kuchochea kilimo.

Kwenye suala la kodi na tozo tofauti ambazo zilikuwa kero kwa mkulima tulifanya ushawishi ili kuzishusha. Zaidi ya tozo, kodi na ada 100 zilizokuwapo zimeondolewa.

Kufanikisha masuala yetu huwa tunawasiliana na Serikali kwa ukaribu sana. Tuna makubaliano ya hiari na Wizara ya Kilimo (MoU) na tuna kiti Wizara ya Fedha na Mipango katika kikosi kazi cha kuishauri Serikali masuala ya kodi, tozo na ada za kilimo.

Kwa mfano suala la uzalishaji wa mafuta ya kupikia tuimehangaika sana kwa sababu yalikuwa yanakuja bure kabisa. Miaka ya 1990 tulikuwa tunazalisha tani 10,000 tu lakini sasa yameongezeka kwa kuilinda hiyo sekta kwa kuweka kodi.

Swali: Mpango wa pili wa maendeleo ya kilimo (ASDP II) umezinduliwa hivi karibuni. Unadhani utakuwa na mchango wa kutosha kwenye kilimo?

Jibu: ASDP II ni mpango mkubwa na mzuri kuliko mipango mingine tangu tupate uhuru.

Kwa miaka mitano ya kwanza una bajeti ya Sh13.6 trilioni lakini sekta binafsi inatakiwa ichangie asilimia 60, ndiyo maana tunaiambia Serikali itakuwa ngumu sana kama mazingira ya kufanya biashara hayataboreshwa.

Sekta binafsi iwekewe mazingira rafiki ya biashara iweze kutoa fedha hizo kwa ajili ya kilimo.

Swali: Hivi karibuni kulikuwa na mvutano kati ya Serikali na wabunge wa mikoa ya kusini. Mbona hamkuonekana kufanya lolote?

Jibu: Suala la korosho hatukuliingilia sana kwa sababu halikuwa la kisera bali Seriklali kutoa fedha kutoka upande huu na kuweka mwingine.

Enzi za Mwalimu Julius Nyerere alianzisha viwanda vingi vya kubangua korosho lakini havikufanya kazi hivyo Serikali ikaamua kuvibinafsisha hata hivyo bado havikutumiwa, bali wafanyabiashara walisafirisha korosho ghafi nje ya nchi.

Sasa, ili kupunguza usafirishaji wa korosho ghafi nje ya nchi, Serikali iliweka kodi (export levy). Kwa muda wote Serikali ilikuwa inachukua asilimia chache Serikali inasema fedha hizo zinatumiwa vibaya hivyo inataka ikaenazo ili itoe kwa utaratibu mzuri zaidi.

Kwa hiyo, hilo halikuwa suala la kisera ambalo tunaweza kwenda kukaa na Serikali kulisemea. Lakini tunasubiri kuona matokeo yake, kama yatakuwa mabaya tutakwenda kuwauliza kwani tunafuatilia kwa umakini uzalishaji baada ya kuondolewa kwa mapato ya ushuru wa korosho.

Wakati ushuru huo unakwenda halmashauri uzalishaji wa korosho ulipanda na kufika zaidi ya tani 250,000. Sasa tutaangalia baada ya miaka miwili uzalishaji unaendaje.

Tukiona umepanda tutasema hata ukishuka tutaiambia Serikali mbona uzalishaji umekuwa hivi baada ya kuondolewa kwa ushuru.