UCHAMBUZI: Ni muhimu Serikali kujenga nidhamu ya kazi

Thursday August 30 2018

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro. 

Serikali imetangaza kuzuia matumizi ya mitandao ya kijamii kwa watumishi wa umma wakati wa kazi kwani imebainika kuwa wengi wao wanapoteza muda mwingi kwenye teknolojia hiyo kuliko kutekeleza majukumu yao.

Pia, imebainika kuwa kasi ya mtandao wa Serikali imepungua kutokana na matumizi makubwa yasiyo halali ya mitandao ya kijamii na hivyo kusababisha watumishi wengine wanaotumia mtandao wa intaneti wa Serikali kutekeleza majukumu yao kuathirika.

Katazo hilo lililotangazwa na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Dk Laurean Ndumbaro linazihusu taasisi zote za umma.

Kwa uamuzi huo, ni kama vile Serikali imesikia kilio cha wananchi wengi wanaokwenda kupata huduma kwenye taasisi hizo, mara kadhaa watumishi wamekuwa wazito kuwahudumia wateja wao kutokana na kushughulishwa na mitandao hiyo ya kijamii.

Pamoja na mambo mengine ambayo Serikali imeyaweka kwenye katazo lake hilo, lakini kubwa zaidi na linalogusa wananchi wa kawaida ni watumishi kupoteza muda mwingi kwenye mitandao hiyo badala ya kutekeleza majukumu yao.

Pamoja na ukweli kwamba mitandao ya kijamii kama vile “YouTube”, “WhatsApp”, “Instagram”, “Facebook” na “Twitter” imekuwa njia ya kuu ya kupashana habari miongoni mwa jamii au wanafamilia na kwamba hivi sasa jamii imeelimika katika matumizi yake, kinachokera ni kwa watumishi wa umma kudumaza huduma kwa wananchi kwa sababu ya mitandao hiyo.

Tunaheshimu matumizi ya teknolojia katika kupashana habari, lakini kanuni na taratibu za kazi lazima ziheshimiwe mfano mataifa yaliyoendelea kama Marekani wao walianza siku nyingi kupiga marufuku matumizi binafsi ya simu za mkononi kazini.

Jambo jema kwa katazo la Serikali ni kwamba kwa wale watumishi ambao kwao mitandao ya kijamii ni muhimu katika kutekeleza majukumu yao, wamepewa ruhusa hiyo lakini kwa sharti la kuomba kibali katika mamlaka husika.

Heshima ya Serikali ni pale inapojenga nidhamu ya kazi, hivyo kwa tamko hili la kuzuia matumizi ya mitandao ya kijamii saa za kazi ni muhimu katika kujenga uwajibikaji wenye tija.

Mbali na heshima kwa Serikali, ulegevu wa kutoa huduma uliochangiwa na watoa huduma kushughulika zaidi na mitandao ya kijamii uliwakosesha wananchi haki ya kupata huduma za haraka na kwa uhakika. Kuhusu matumizi ya intaneti yasiyokuwa na tija kwa Serikali, aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa aliwahi kutoa takwimu zilizoonyesha jinsi watumishi wa Serikali wanavyotumia muda mwingi kwenye mitandao ya kijamii na kuwakosesha wananchi huduma stahiki.

Profesa Mbarawa alisema uchunguzi uliofanywa na wizara yake ulibaini megabaiti zinazotumika katika taasisi mbalimbali za Serikali hazitumiwi katika matumizi yenye tija kwa Serikali.

Alisema asilimia saba pekee ndiyo iliyobainika kuwa matumizi yenye tija kwa Serikali, huku asilimia 27 zikitumiwa na wafanyakazi wa Serikali kupakua vitabu vya shule kwa ajili ya watoto wao.

Waziri huyo alisema asilimia 20 zilibainika kutumika kupakua video alizosema kimsingi hazina uhusiano na utendaji kazi wa watumishi wa Serikali na asilimia 37 zinatumika kutumiana mafaili mengine yasiyo na umuhimu katika utendaji kazi.

Tunaamini uamuzi wa kuzuia mitandao ya kijamii kwenye intaneti ya Serikali wakati wa muda wa kazi kuanzia saa 1:30 asubuhi hadi saa 9:30 alasiri umekuja wakati mwafaka.

Katazo hilo sasa litawasukuma watumishi kuwajibika ipasavyo na manung’uniko ya wananchi kuhusu kuchelewa kupata huduma stahiki yatamalizika.