Polisi wajitenge na lawama zisizo lazima

Thursday November 1 2018

Hatukufika katika kijiji cha Njirii wilayani Manyoni, Mkoa wa Singida kujiridhisha namna ajali ya gari lililokuwa limewabeba wafanyakazi wa Wizara ya Kilimo Jumapili iliyopita, ilivyotokea.

Tuliridhishwa na taarifa ya Polisi mkoani Singida iliyoelezea ajali hiyo iliyohusisha gari lenye namba za usajili STK 8925 na lori lenye namba za usajili RIC 152Y na kusababisha vifo vya wafanyakazi watano wa wizara hiyo.

Taarifa ya polisi ilisema chanzo cha ajali hiyo iliyotokana na magari hayo kugongana uso kwa uso ni mwendo kasi wa dereva la Wizara ya Kilimo, aliyejaribu kuyapita malori mawili bila kuchukua tahadhari.

Tuliamini polisi walitoa taarifa hiyo baada ya kufika eneo la tukio na kwa kuwa siku hizi polisi wa usalama barabarani ni wengi, huenda hawakuwa mbali. Watakuwa walipima na kuhoji watu, kisha wakaandika ripoti waliyoona kuwa ni ukweli dhahiri wa kilichotokea.

Lakini wakati wa maziko ya watumishi hao wa serikali Jumanne mjini Dodoma, Waziri wa Kilimo wa Serikali wanayotumikia polisi waliopima ajali hiyo, alisema: “...narudia tena napinga taarifa hiyo ya polisi wakajiridhishe upya.”

Katika maelezo yake, waziri alisema ana uhakika dereva wao ni mzoefu wa kuendesha magari kwa muda mrefu hata kama hakuwahi kumwendesha yeye, asingeweza kufanya uzembe wa aina hiyo barabarani na kusababisha vifo.

Sababu kubwa ya waziri kupinga ripoti ya polisi ni kwamba alifika eneo la tukio ambako kuna tuta kubwa, akawauliza wananchi mashuhuda na wakamthibitishia kwamba chanzo cha ajali ni lori kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari.

Sisi hatutaki kuingia kwenye ubishi kujua nani anasema kweli kati ya waziri aliyepita mara moja na polisi ambao wajibu wao ni kudhibiti ajali, na pale inapokuwa imetokea kuchunguza sababu na kutangaza hadharani.

Kama waziri amethubutu kupinga hadharani baada ya kuwauliza mashuhuda, tunajiuliza polisi walitunga sababu za ajali na hawakufika eneo la tukio? Ikiwa ripoti yao ni ya uongo walitunga kwa faida ya nani?

Japokuwa tungependa kuona wananchi wanawaacha polisi wafanye kazi yao bila kuingiliwa, kuwaacha huru polisi wapotoshaji ni hatari. Sasa ikiwa waziri wa serikali amekosa uvumilivu amepinga ripoti ya polisi, watu wangapi wanyonge wasio na sauti wameumia kutokana na kubambikiwa makosa kuhusu ajali au dosari katika magari yao?

Tunajua kazi ya polisi – wawe maofisa usalama barabarani au wa kulinda raia na mali zao – ni ngumu na wanafanya kazi wakati mwingine katika mazingira magumu. Hata hivyo, wasikiuke kiapo cha kazi yao.

Tunapenda Jeshi la Polisi lifanye kazi zake kwa weledi, bila kuingiliwa, jeshi linalojitenga na uonevu na upotoshaji na likae mbali na lawama nyingi zisizo za lazima.

Maana mara ngapi polisi wamelalamikiwa kuhusu ripoti za watu wanaodaiwa kufia mikononi mwao? Mara ngapi wananchi wamesusa kuchukua maiti wakishinikiza polisi waseme ukweli kuhusu mazingira ya vifo vya wapendwa wao?

Tunapenda Jeshi la Polisi linalofanya kazi ya kulinda watu na mali zao. Tutaliunga mkono lililoongeze hadhi na heshima yake kwa kuwa rafiki wa raia wema, linalofikika, linalotoa taarifa au ripoti zinazoaminika kwa sababu lenyewe linaaminika.