Tafsiri ya Nanenane ionekane shambani

Thursday August 9 2018

Jana ilikuwa kilele cha Sikukuu ya Nanenane inayowahusu wakulima na wafugaji wa Tanzaniapamoja na wadau wao. Sherehe hizi za kila mwaka huangalia mafanikio na changamoto kwa wakulima na wafugaji kuanzia ngazi ya kijiji hadi taifa.

Ni sherehe ambazo wengine huziita ni ‘darasa huru kwa wakulima na wafugaji’ kwa kuwa katika maonyesho hayo wataalamu wa kilimo na mifugo hutoa elimu kwa wadau wao kuhusu kilimo bora na ufugaji bora.

Matarajio ya maonyesho haya ni kuwawezesha wakulima na wafugaji kupata elimu juu ya pembejeo halisi ikiwamo mbegu na dawa za mifugo ili kuwasaidia kuepuka kununua dawa na mbolea feki ambazo huwasababishia hasara na kuwakatisha tamaa.

Sherehe hizi huambatana na maonyesho ya bidhaa za kilimo na namna ya ufugaji bora yanayofanywa na wakulima na wafugaji, ikiwamo mashirika yanayojihusisha na masuala ya kilimo na ufugaji kwa ajili ya kubadilishana uzoefu na wataalamu.

Pia, wakulima wadogo ambao ni wengi ukilinganisha na wakubwa, hujifunza mbinu mpya za kitaalamu zinazoendana na wakati tulionao kwa maana ya mabadiliko ya kiteknolojia na tabianchi ili walime kisasa na kunufaika kiuchumi.

Kwa wafugaji, maadhimisho haya huwasaidia kupata utaalamu wa namna ya kufuga kwa faida, badala ya kuwa na mifugo mingi ambayo mara nyingi faida yake haionekani haraka na wakati mwingine huwaingiza kwenye matatizo ya uharibifu wa mazingira.

Pia, kwa muda mrefu wakulima wamekuwa wakilima kilimo cha mazoea ambacho hakizingatii kanuni za kitaalamu, hivyo kukata tamaa na kuona kuwa kilimo hakilipi kutokana na mbinu duni walizozitumia.

Sherehe hizi zimekuwa zikifanyika kwa miaka mingi, miaka ya nyuma zilifanyika Julai 7 na zilipewa jina la Sabasaba baadaye zikahamishiwa Agosti 8 na ndiyo maana zinaitwa sherehe za Nanenane, lakini tangu wakati huo hali za wakulima na wafugaji zimeendelea kuwa duni.

Rai yetu sasa, sherehe hizi ziwe chachu ya kuwasaidia wakulima waondokane na kilimo cha kubahatisha cha kutegemea mvua na badala yake wajikite katika kilimo cha umwagiliaji ambacho ni cha uhakika, kinachoweza kubadilisha maisha yao kiuchumi.

Pia, ziwasaidie wafugaji ambao si tu wameshindwa kuinuka kiuchumi, lakini waachane na ufugaji wa asili ambao umewaingiza kwenye mapigano kati yao na wakulima kwa kugombea maeneo.

Sekta ya kilimo inapaswa kuangaliwa kwa jicho la tatu kutokana na umuhimu wake katika nchi na ustawi wa jamii, ni sekta ambayo imeajiri watu wengi zaidi kuliko nyingine zote zikiunganishwa ikielezwa kwamba zaidi ya asilimia 75 ya Watanzania wanategemea sekta ya kilimo kama ajira yao na kwa sehemu kubwa, ni kile kinachoendeshwa na wakulima wadogo.

Karibu asilimia 70 ya ardhi ya kilimo na mazao inalimwa kwa kutumia jembe la mkono, asilimia 20 hutumia maksai na asilimia 10 hutumia trekta. Rai yetu sherehe hizi ziwe chachu ya kubadili namba hizi, ya mwisho iwe ya mwisho.

Hilo litawezekana kwa wakulima na wafugaji kusimamiwa vyema katika kuzingatia mbinu za kilimo na ufugaji bora sambamba na kuonyeshwa fursa za masoko ili mazao yao yasiozee ghalani na mifugo yao kukosa soko zuri.

Tunapenda kuona mikakati mizuri ya Serikali ya kutafsiri sherehe hizi ili zionekane katika mashamba na mifugo ya wakulima.