Taka zitumike kama fursa kiuchumi

Thursday July 12 2018Lilian Timbuka

Lilian Timbuka 

By LILIAN TIMBUKA

Baada ya suala la usafi kutiliwa mkazo na Serikali, hali imeanza kuimarika ila tatizo bado lipo kwenye utupaji wa taka zinazokusanywa kutoka maeneo tofauti.

Kinachotokea ni kufanywa kwa usafi mtaani na taka kurundikwa pembezoni mwa barabara au vichochoroni badala ya kupelekwa dampo au mahala popote panapohusika na utunzaji wake kabla hazijateketezwa.

Magari mengi ya halmashauri yanayozoa taka yenyewe ni taka zinazotembea. Yamekuwa kero. Baadhi yakipita yanakera, kwa sababu kwanza ni machafu na wakati mwingine hudondosha taka yalizobeba.

Pia yanatoa harufu mbaya kana kwamba wahusika hawafahamu juu ya umuhimu wa kuwalinda watumiaji wengine wa barabara wanazotumia.

Huu ni wakati mwafaka kwa Serikali na jamii kutafuta namna sahihi ya kuzihuisha taka ili ziwe fursa kiuchumi. Nasema hivyo kwasababu takataka zina fursa kwa baadhi ya viwanda kwa wananchi kuanza kuzichambua na kwenza kuziuza katika viwanda vinavyohitai aina fulani ili ziwasaidie wananchi kujipati fedha na kuboresha maisha yao kama zitatumika.

Wataalamu wa mazingira wanasema fursa kuu zilizomo katika taka ni pale zinapochakatwa na kuzirudisha kwenye matumizi kama ilivyo kwa plastiki au kubadilisha matumizi na kutumika kwa shughuli nyingine kama mbolea mashambani.

Wataalamu hao wanaainisha kuwa, zipo taka ngumu na laini na zote zinaweza kutumika kwa mara ya pili endapo juhudi kidogo itatumika kuzirudishia thamani yake. Hili linafanywa kwenye chupa, karatasi, chuma chakavu au maji. Zinatumika na zinatumika tena. Wanasema miundombinu ya kuwezesha hilo kufanikiwa kama tutadhamiria, ipo na inawezekana.

Kwa mfano, Austria ni miongoni mwa nchi zinazoongoza kwa asilimia kubwa kwa kuchakata taka na kuzirudishia thamani kwa ajili ya matumizi ikiwamo mbolea.

Sweden pia imepiga hatua kubwa katika utumiaji wa taka kwa kuzigeuza kuwa bidhaa au kuzalisha umeme na kuchangia upungufu mkubwa wa taka nchini humo kiasi cha kulazimika kununua au kuagiza kutoka nchi jirani kwa ajili ya kuendelea na uzalishaji kwenye viwanda vyao.

Tukirudi Tanzania, bado tuna uhaba wa nishati mbadala na mbolea, lakini kwingineko taka zimekuwa zikizalisha vitu hivi na kutoa mchango mkubwa wa kutunza usafi na mazingira.

Kwa mtazamo huu, Tanzania inaungana na nchi nyingi zinazoendelea ambazo hazijachangamkia fursa ya kuchakata takataka. Tofauti na nchini Misri, kuna kikundi cha watu wanaopita mlango kwa mlango kukusanya taka na kuzichakata.

Kuna baadhi ya mikoa na wilaya zilianza vema harakati za kudhibiti taka ukiwamo Mkoa wa Mtwara uliojenga dampo la kisasa na Wilaya ya Kinondoni iliyojenga kiwanda kwa ufadhili toka Ujerumani ila mpaka sasa hakuna mrejesho wa miradi hiyo.

Halmashauri zinatakiwa kutowekeza nguvu nyingi kutafuta magari ya kuzoa taka, badala yake ziandae mpango wa kujenga viwanda vitakavyochakata taka hizo na kuleta suluhisho la kudumu.

Hili linaweza likafanywa kwa kushirikisha wadau au kutafuta wawekezaji au kuingia ubia na kampuni zenye uwezo huo.

Kufanya hivyo, taka hazitozagaa wala kutiririka mitaani badala yake kila mmoja ataona thamani iliyomo kama ilivyo sasa kwa taka za plastiki ambazo huokotwa kila zinapoonekana kutokana na umuhimu wake kwa vijana wanaochangamkia kipato kinacho ambatana nazo.

Kila halmashauri ikifanikiwa kuwa na kiwanda kimoja au viwili, tatizo la ajira litapungua kwa kiwango kikubwa hata malalamiko yanayoelekezwa kwa Serikali yanaweza yakapungua.

Hili likifanyika tutaanza kuona faida zitokanazo na taka mfano umeme wa biogas utakaozalishwa.

Mwandishi ni mhariri wa jarida la afya la Gazeti la Mwananchi. 0713-235309