Uwekezaji unahitajika miundombinu ya umwagiliaji kupambana na umasikini

Muktasari:

  • Takwimu zinaonesha wakulima ni asilimia 62.1, wafugaji asilimia 2.4 na wavuvi asilimia moja. Ripoti mbalimbali zinaonesha wakulima wengi bado wanatumia nyenzo duni kujitafutia ridhiki ya kila siku.

Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 inaonyesha zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania ni wakulima ambao maisha yao yanategemea kilimo, ufugaji au uvuvi.

Takwimu zinaonesha wakulima ni asilimia 62.1, wafugaji asilimia 2.4 na wavuvi asilimia moja. Ripoti mbalimbali zinaonesha wakulima wengi bado wanatumia nyenzo duni kujitafutia ridhiki ya kila siku.

Uendeshaji wa shughuli zao unakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi ambayo yamesababishwa na shughuli za kibinadamu na asili. Mvua hazinyeshi kwa wakati na za kutosha kama hapo awali.

Moja ya njia yenye uthibitisho wa kisayansi ambayo inaweza kutumika angalau kupunguza utegemezi wa mvua zisizotabirika na kuzalisha mazao mengi katika eneo dogo ni ujenzi wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji.

Takwimu za mwaka huu zinaonesha kuna hekta milioni 29.4 zinazofaa kwa kilimo cha umwagiliajo. Kati ya hizo, hekta milioni 2.3 sawa na asilimia 7.82 zinafaa kwa umwagiliaji mkubwa sana wakati hekta milioni 4.8 sawa na asilimia 16.33 zinafaa kwa umwagiliaji wa kati na hekta milioni 22.3 sawa na asilimia 75.85 kwa umwagiliaji mdogo.

Hadi Machi, ni hekta 475,052 sawa na asilimia 47.51 zilikuwa zimetumika huku kukiwa na lengo la kufikisha hekta milioni moja mwaka 2020 sawa na asilimia 1.6 ya eneo lote linafaa kwa kilimo cha umwagiliaji nchini.

Eneo lililotumika hadi sasa limechangia asilimia 24 ya mahitaji yote ya chakula nchini. Kama asilimia 1.6 ya eneo lililotumika kwa kilimo cha umwagiliaji limeweza kuchangia asilimia 24 ya mahitaji ya chakula nchini, inamaanisha asilimia 6.67 ya eneo lote yatakidhi mahitaji ya chakula kwa asilimia 100.

Takwimu za mwaka 2016 zinaonesha Serikali ilikuwa na mpango wa kukamilisha mabwawa 30 ya umwagiliaji nchi nzima na kujenga mapya 40 ili kuvuna maji ya mvua kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na matumizi mengine.

Hata hivyo zipo changamoto ambazo zinapaswa kushughulikiwa ili kufanikisha malengo yaliyopo. Mosi ni fedha kutoidhinishwa kadiri ya mipango na bajeti iliyopitishwa na Bunge.

Kwa mfano mwaka 2017/2018, Wizara ya Maji na Umwagiliaji kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji ilitengewa Sh20.1 bilioni kwa ajili ya miradi ya maendeleo lakini hadi Machi, 2018 tume hiyo ilikuwa imepokea Sh2.5 bilioni sawa na asilimia 12.44 tu ya lengo.

Vilevile, utegemezi wa fedha kutoka kwa wafadhili kutekeleza miradi ya umwagiliaji. Hali ya utegemezi imeendelea kuzorotesha sekta hii hasa wafadhili wanapochelewa au kutotoa fedha walizoahidi.

Changamoto nyingine ni baadhi ya maeneo yanayofaa kwa kilimo cha umwagiliaji kutomilikiwa na Serikali. Hii husababisha Serikali kulipa fidia kwa wahusika pindi inapotaka kuyaendeleza.

Nne ni baadhi ya maeneo ya umwagiliaji kutegemea maji kutoka kwenye vyanzo mbalimbali ikiwemo mito ambayo mabadiliko ya tabianchi yameiathiri hivyo miradi kushindwa kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Licha ya changamoto hizo, zipo faida muhimu za uwepo wa miundombinu ya umwagiliaji kwa kaya, jamii na Taifa kwa ujumla kuwa na uhakika wa chakula kwa mwaka mzima.

Pia husaidia wafugaji kuwa na uhakika wa maji salama kwa ajili ya mifugo na wavuvi kuendesha shughuli zao za kujitafutia kitoweo kukidhi mahitaji yao ya kila siku .

Miundombinu hii pia husaidia kupunguza umasikini kuanzia kutokana na biashara inayofanywa na wadau kilimo, ufugaji na uvuvi.

Aidha miundombinu ya umwagiliaji husaidia kuepusha mafuriko kunapokuwa na mvua kubwa kwani maji huelekezwa kufuata mkondo yalipo mabwawa hivyo kuepusha hasara vikiwamo vifo vya watu na mifugo pamoja na uharibifu wa mali.

Kufanikisha utekelezaji wa mipango na mikakati ya Serikali, ni muhimu kuikaribisha sekta binafsi kushiriki kuinua uchumi wa nchi. Ushiriki wa sekta binafsi katika kilimo cha umwagiliaji sio wa kuridhisha kwa mujibu wa ripoti za Serikali.

Ni wakati sasa kwa sekta binafsi kushiriki katika kilimo cha uwagiliaji ili pamoja na mambo mengine kuwa na uhakika wa chakula na kupambana na umasikini.

Badala ya kila halmashauri kuanzisha skimu ya umwagiliaji inayogharimu bilioni kadhaa hadi kukamilika kwake, ni vyema kila mkoa ukateua halmashauri moja kutekeleza mradi mmoja mkubwa ambao utahudumia mkoa mzima ili kutumia kwa manufaa rasilimali chache zilizopo.

Vilevile, tume ya Taifa ya umwagiliaji iwe na wataalamu kwenye halmashauri badala ya kuishia kanda kama ilivyo sasa ili kuongeza uwajibikaji wa pamoja. Serikali iihamishe sekta ya umwagiliaji kutoka Wizara ya Maji kwenda kilimo kurahisisha usimamizi.

Usimamizi wa karibu wa miradi itakayotekelezwa unahitajika ili kutoa hamasa kwa wananchi ambao hawajafikiwa na miradi husika kuona haja ya kuanzisha na kuiendeleza.

Mwandishi ni mtakwimu, ofisi ya Rais - Tamisemi