Zifahamu haki na wajibu wa mteja wa bima kisheria

Muktasari:

  • Siku zote hupati nguvu ya kudai haki zako kabla hujatimiza wajibu wako.

Usipojua unapokwenda, huwezi kufika na jambo usilolijua ni sawa usiku wa kiza. Huwezi kudai kitu ambacho hufahamu kuwa ni haki yako.

Siku zote hupati nguvu ya kudai haki zako kabla hujatimiza wajibu wako.

Kama kuna jambo la msingi sana kwa mteja wa bima, kabla hujaanza kuwaza kuhusu malipo ya fidia, unapaswa kufahamu haki na wajibu wako. Usithubutu kuingia mkataba wa bima kabla hujajua haki zako ni zipi na wajibu wako ni upi.

Makubaliano yoyote lazima yawe na haki kwa upande mmoja na wajibu upande mwingine. Haki za mteja wa bima ni wajibu wa mtoa huduma na wajibu wa mteja wa bima, ni haki kwa mtoa huduma za bima.

Bima inatafsiriwa kama uhamishaji hatari za kiuchumi kutoka kwa mteja au mkataji wa bima kwenda kwa mtoaji wa hiyo zinazoweza kusababisha hasara kutokana na matukio yasiyotarajiwa ambayo huathiri mali, maisha au mwili kwa kuzingatia vigezo ambavyo hutolewa na mtoaji wa bima husika.

Ingawa watumiaji wa bima nchini ni wachache lakini hamasa inayoendelea kutolewa inatarajiwa kuwa itabadilisha mwenendo ulipo kwa kuongeza idadi.

Kwa sasa watu wengi wanatumia bima ya aina moja tu hasa ya afya huku wamiliki wengi wa magari wakilazimishwa kukata kwa ajili ya abiria.

Miongoni mwa sababu zinazochangia matumizi madogo ya bima ni kukosekana kwa taarifa sahihi. Wananchi wengi hawajui wafanye nini kupata bima kujikinga na hatari mbalimbali dhidi ya mali wanazomiliki.

Lakini kwa walio tayari, ni vyema wakawatumia wataalamu waliopo kupata ushauri wa kina kwenye miradi mbalimbali waliyonayo kwenye kilimo, usafirishaji, huduma za fedha na sekta nyinginezo.

Ni haki ya mkataji bima kufidiwa hasara ya mali ambayo imeharibika kulingana na ukaribu wa mazingira yaliyo ainishwa katika sera za bima ambapo mtoaji huangalia chanzo cha ajali na athari katika mali.

Ni haki ya mteja kufidiwa hasara aliyoipata ili aweze kunufaika na mali yake kama ilivyokuwa mwanzo pindi mali yake haijaharibiwa. Fidia hiyo ni lazima isipungue na isizidi gharama ya mali husika.

Kumbuka, bima haipo kwa ajili ya kumtajirisha ama kumzorotesha mteja kiuchumi bali kumrejesha sehemu aliyokuwapo kabla hajakumbwa na matatizo. Fidia hiyo huweza kuwa katika mfumo wa fedha ama utengenezaji wa mali iliyoharibika au kupatiwa mali nyingine.

Riba ya bima ni haki ya mkataji ambayo huundwa kimkataba na sheria. Ni wajibu wa mteja kusema ukweli na kutoa taarifa zinazohusiana na mali husika inayokatiwa bima.

Kwa mfano kama ni gari, basi eleza lina muda gani tangu linunuliwe, huwa unalihifadhi wapi, eleza mazingira yote hatarishi ya sehemu unapolipaki ili mtoaji bima aweze kutambua anakukatia bima ya kiwango gani au kama anaweza kukubali au kukataa kulingana na mazingira ya mali yako.

Mfano mwingine ni wa nyumba ambayo ipo karibu na ghara la kuhifadhia vitu vinavyolipuka. Ni wajibu wa mteja kutaja hatari zote hata kama hajaulizwa.

Wajibu wa kusema ukweli hudumu katika kipindi chote cha makubaliano. Hali hii inatakiwa iwepo kabla ya kuingia hata mkataba unapokamilika.

Ni wajibu wa mteja wa bima kupunguza hasara ama kwa kujitahidi kuepusha majanga yasiyotarajiwa kadri awezavyo ili kulinda mali yake kama vile katika mlipuko wa moto sio kupuuza kwa mantiki kwamba mali hiyo ameikatia bima.

Ni wajibu wa mteja kulipa kiwango cha fedha alichopangiwa kila wakati kadri ya makubaliano na kampuni husika ya bima kumpatia mkataji sera ambazo anatakiwa akubaliane nazo.