Wananchi wanahitaji ufafanuzi kufutwa kwa leseni za ving'amuzi

Muktasari:

  • Hata hivyo, kampuni hiyo kupitia kwa msemaji wake ilijitetea ikisema ina ving’amzi vya aina mbili, kimoja kinaonyesha chaneli za bure (FTA decoder), ambacho huuzwa Sh89,000 na kingine chaneli hizo huonekana baada ya kulipia (Pay TV Decoder) na bei yake ni Sh45,000.

Tangu Julai 27 Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilianza kutoa matangazo mfululizo kuhusu nia yake ya kusitisha leseni za kampuni za ving’amzi (visimbusi) nchini zinazokwenda kinyume na masharti ya leseni zao. Walianza na Star Media (Startimes), Julai 27 ambapo mamlaka hiyo ilitoa tangazo kwa umma lililoelezea nia yake ya kuzuia leseni ya kampuni hiyo kwa madai kuwa ilikiuka masharti yake, ikiwa ni pamoja na kutoonyesha chaneli za bure na kutolipa faini iliyotozwa jambo ambalo ni kinyume na masharti ya leseni yao.

Hata hivyo, kampuni hiyo kupitia kwa msemaji wake ilijitetea ikisema ina ving’amzi vya aina mbili, kimoja kinaonyesha chaneli za bure (FTA decoder), ambacho huuzwa Sh89,000 na kingine chaneli hizo huonekana baada ya kulipia (Pay TV Decoder) na bei yake ni Sh45,000.

Ilidai kuwa hakukuwa na mawasiliano mazuri na wateja wao kuhusu huduma inazozitoa; watumiaji wa Pay TV Decoder ambayo huuzwa bei ndogo tofauti na wale wa FTA wanaotakiwa kufanya malipo ya kila mwezi ili kuona chaneli za bure. Lakini inasema kuna namna ya kubadilisha Pay TV Decoder na kuifanya kuwa FTA kupitia kwa mawakala wake kwa kulipia Sh44,000. Kabla ya hilo kuisha, juzi Agosti 7, TCRA ilitangaza kusudio lake la kusimamisha leseni ya kampuni ya Multichoice Tanzania Limited, wamiliki wa king’amzi cha DSTV na Simbanet Tanzania Limited inayomiliki Zuku kwa kosa lilelile la kukiuka masharti ya leseni.

Tofauti na Startimes, tangazo la TCRA ambalo linaonyesha kuwa limetolewa na mkurugenzi mkuu wa mamlaka hiyo katika magazeti tofauti hapa nchini, lilieleza kuwa Zuku na DSTV wamekuwa wakionyesha chaneli zilizopo kwenye orodha ya chaneli za bure kinyume na matakwa ya leseni zao. Chaneli ambazo zinapaswa kuonyeshwa bure kwa mujibu wa TCRA ni zile ambazo zinatumia mtambo wa ardhini kama TBC1, ITV, Channel Ten, Clouds na Star TV. Ni zile tu ambazo zinatumia satellite zinazotakiwa kulipia. TCRA inawalaumu watoa huduma kuwa wamekuwa wakikiuka masharti ya leseni zao kwa makusudi hivyo kwa matangazo hayo, wasipofuata masharti ya leseni baada ya siku 30, watachukuliwa hatua.

Hili limeibua mabishano ya kisheria na tafsiri yake, kwa kuwa watoa huduma wanaona wako sahihi kwa kile wanachokifanya kulingana na leseni zao lakini mamlaka inayowasimamia kwa sheria na vipengele vya leseni, inaona wanakiuka masharti.

Sina cha kusema kuhusu mabishano haya ya kisheria na tafsiri zake kwa kuwa hata masharti hayo ya leseni sijayaona zaidi ya kuyasikia katika malumbano.

Lakini mimi na Watanzania wenzangu tunaohitaji huduma, tupo katika nafasi gani wakati huu ambao baadhi ya visimbuzi vyetu vimeacha kuonyesha chaneli za ndani kutokana na tangazo hilo la mamlaka inayosimamia sekta hiyo? Kabla ya hayo, hakuna mwananchi aliyewahi kuambiwa na Serikali kuhusu haya yanayojitokeza, kampuni husika ziliachwa zikashindana sokoni.

Ni nimuhimu kwa mdhibiti kusimamia sheria na taratibu zilizowekwa, lakini umma ambao hauzifahamu taratibu hizo haupaswi kuathiriwa na ukiukwaji wa taratibu. Mtanzania aliyenunua kisumbusi kwa kuambiwa atapata chaneli za ndani leo zikiondolewa bila kuambiwa mapema ni kutomtendea haki.

Nionavyo, utekelezaji wa sheria hii ungefanywa kwa masilahi ya umma, kama watoa huduma waliwaaahidi wateja na kutoa huduma ambayo si sehemu ya leseni yao, basi waliolipa warudishiwe gharama zao au mamlaka izungumze na watoa huduma ili waboreshe leseni yao.

Kinyume chake, wananchi watajikuta wakilazimika kununua visumbusi viwiliviwili ili kuona chaneli zote.

Ni vyema watoa huduma wakati wote wakafuata taaribu za kisheria ikiwa ni pamoja na matakwa ya leseni zao ili kuepusha usumbufu kwa watumiaji kama ilivyo sasa.

Ephrahim Bahemu 0756939401