Komesha maumivu ya tumbo wakati hedhi

Katika maisha ya mwanamke ambaye tayari ameishavunja ungo huwa ni kawaida katika kila mzunguko wa mwezi kukumbana na maumivu kabla na wakati wa hedhi.

Wasichana wengi hasa ambao bado hawajazaa huwa na kawaida ya kukimbilia madukani kununua dawa za maumivu ikiwamo Ibuprufen, Hyosin, Paracetamol na Diclofenac.

Kiafya si sahihi kwa kila mzunguko wa mwezi kubugia dawa hizi ili kukabiliana na maumivu hayo kwa kuwa dawa za maumivu kwa muda mrefu zina madhara.

Ni kweli wasichana wengi hawana ufahamu wakutosha kujua kuwa yapo mazoezi yanayoweza kusaidia kupunguza ukali wa maumivu haya hivyo kuepusha na matumizi holela ya dawa hizi.

Maumivu haya kwa asilimia kubwa huwa yanavumilika na huwa si tatizo la kiafya kama ambavyo wengi hupata hofu, karibu wanawake asilimia 90 hupata maumivu ya kawaida wakati wa hedhi.

Wachache wanakuwa na dosari inayosababisha maumivu makali ijulikanayo kitabibu kama Endometriosis yaani kujipachika mahali pasipo kwake kwa tando nyororo ya nyumba ya uzazi.

Leo nitayatizama yale maumivu ya kawaida ambayo hayasababishwi na tatizo la kiafya au dosari ya kiafya.

Kujihusisha na mazoezi mepesi kama vile kuruka kamba, kucheza mziki wa haraka haraka, kufanya mazoezi yakitamaduni kama vile Yoga, kucheza michezo kama vile netball, kuendesha baiskeli, mpira wa kikapu yote haya yanapunguza ukali wa maumivu wakati wa hedhi. Mazoezi mepesi hujulikana kitaalamu kama Aerobics exercise ndiyo ambayo umoja wa madaktari wa magonjwa ya kinamama duniani wanayopendekeza wanaopata maumivu hayo kufanya. Sababu ya kisayansi ya kushauri hivi ni kutokana na wakati wa mazoezi kemikali ijulikanayo kama Endorphin huririshwa, kemikali hii huwa ni dawa ya kiasili ya maumivu ndani ya mwili.

Endophin huizuia kemikali inayozalishwa wakati wa hedhi inayojulikana kama Prostaglandin ambayo husababisha misuli ya nyumba ya uzazi kujikamua au kujikunja hali inayosababisha maumivu.

Wakati wa hedhi wanawake wengi hupata mabadiliko ya hisia yaani mood swing hali inayowafanya kuwa na hasira hivyo kemikali ya Endophin huleta hisia za furaha na kuwaepusha na hasira.

Ili kuweza kufikia lengo la kudhibiti maumivu haya ni vizuri kufanya mazoezi mepesi wakati wa kipindi cha hedhi angalau nusu saa yaani dakika 30 kwa siku.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu