Kula mahindi lishe uone faida yake

Hivi umeshawahi kula mahindi lishe? Unajua faida ya ulaji wa mahindi lishe? Wengi wetu tunakula mahindi yenye rangi nyeupe ambayo wataalamu wanasema hayana virutubisho vinavyotakiwa katika afya ya binadamu.

Kama ulikuwa hauna mpango wa kula mahindi lishe, anza sasa kwa sababu yamesheheni virutubisho mu-himu kwa ajili ya kuukinga mwili wako na ma-gonjwa mbalinbali.

Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi cha Chakula na Lishe (TFNC), Dk Eliafatio Towo anasema mahindi lishe yana rangi ya njano na yana vitamini A kwa wingi.

Dk Towo anasema vitamini A, iliyopo katika mahindi hayo humsaidia mtu kukua vizuri, kuona vizuri na vilevile ni kinga dhidi ya magonjwa.

Anasema mahindi haya pia, yanafanana na mengine ya njano na meupe ambayo sio mahindi lishe.

Dk Towo anasema siyo mahindi yote yenye rangi ya njano ni mahindi lishe.

“ Tofauti kubwa ya mahindi lishe na mengine ni kwamba mahindi lishe hutupatia faida za kilishe za vitamini A kitu ambacho aina nyingine ya mahindi haiwezi kutupatia,” anasema Dk Towo.

Anasema sifa ya mahindi lishe ni kuwa na kiwango kikubwa cha kichocheo kiitwacho Provitamin A, kwa ajili ya kutengeneza vitamini A(8mg/kg-14mg/kg) na rangi yake huwa ya karoti au rangi ya machungwa iliyokolea. “Hata unga wake ukisaga una rangi ya karoti au chungwa lililokolea, wakati mahindi ambayo siyo lishe yakuwa rangi kama nyekundu kwa mbali na hata ukiyasaga rangi yake inabaki kuwa hiyo, hivyo ni rahisi kujua,” anasema Dk Towo.

Dk Towo anasema ulaji wa mahindi lishe mara kwa mara unakinga magonjwa mbalimbali.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili Hadija Jumanne