Kula yai moja la kuchemsha asubuhi

Mayai ya kuchemsha ni chakula muhimu katika mwili wa binadamu, pia yana virutubisho na madini mengi yenye faida.

Mayai yana protini, vitamini A, D, B na B12, pamoja na madini ya lutein na zeaxanthin yanayoweza kuzuia mtu kupata matatizo ya macho atakapozeeka.

Kama ulikuwa hujui! mayai yana kemikali iitwayo choline ambayo ni muhimu kwa ukuaji na afya ya ubongo wa mtoto tumboni na ndiyo maana mjamzito anashauriwa kutumia yai moja mpaka mawili kwa siku.

Ofisa Elimu Kilimo na Mifugo, Wilaya ya Kisarawe, Narcisa Lihepanyama anasema kutokana na mayai kuwa na protini nyingi, wataalamu wa masuala ya lishe wanashauri walau kula yai moja kwa siku.

“ Ni vyema ukala yai moja asubuhi wakati wa kifungua kinywa ili kujipatia virutubisho muhimu ambavyo huwezi kuvipata katika vyakula vingine,” anasema Lihepanyama.

Pia, anasema watu wanakosa madini na virutubisho muhimu ambavyo havipatikani katika vyakula vingine bila wao kujua au kutokuwa na mfumo mzuri wa kupangilia ulaji lishe bora.

Hata hivyo, ulaji wa yai moja kwa siku kunaweza kuwasaidia watoto wadogo wenye utapiamlo kuongeza urefu kulingana na utafiti wa miezi sita, uliofanywa huko Ecuador.

Utafiti uliofanywa na Shirika na Chakula Duniani (FAO) mwaka 2011, unaeleza kuwa ulaji wa mayai kwa mtoto ni wastani wa mayai 106 tu kwa mwaka, huku idadi inayotakiwa kuliwa na mtu mzima ni mayai 300.

Lihepanyama anasema mayai husaidia ukuaji wa ubongo na uwezo wa kumbukumbu.

Vile vile ulaji wa mayai unasaidia kulinda macho, huondoa sumu na husaidia kuongeza nuru ya macho na hiyo ni kutokana na kuwapo kwa kemikali za leutin na.

Lakini faida nyingine, mayai yana kaisi kikubwa cha kingi cha Omega-3, ambayo husaidia kupunguza mafuta yapatikanayo katika damu yaani ‘triglycerides’.

Mtaalamu huyo anafafanua kuwa mayai yana uwezo wa kupunguza hatari ya kupatwa na kiharusi, kwa wale wanaotaka kupungua uzito bila madhara wanashauriwa kula mayai.

Kwa upande wa urembo, yai husaidia kuboresha ngozi na nywele iwapo utachanganya yai bichi na asali walau kijiko kimoja kwa wiki mara moja kwa kupaka usoni au katika nywele, kwa muda wa dakika 20, kisha kuosha.

Hata hivyo, Lihepanyama anatahadharisha kuwa ulaji wa mayai ambayo hayajaiva vizuri, pamoja na kundaliwa katika mazingira machafu, unaweza kuhatarisha afya.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili Hadija Jumanne