Kuna tatizo la UTI au vipimo?

Friday November 9 2018

 

By Waandishi Wetu,Mwananchi

Kuna wengi wanajiuliza kama ugonjwa wa maambukizi ya njia ya mkojo, maarufu kwa jina la UTI umeibuka siku hizi au ulikuwepo lakini haukuwa ukifahamika sana.

Hii inatokana na ukweli kwamba wengi wanaojisikia kuwa na dalili za ugonjwa wa malaria, hukutwa na ugonjwa huo wa UTI baada ya uchunguzi zaidi kufanyika katika kipimo cha mkojo.

Hali kadhalika, kwa wanawake ndio imekuwa mbaya zaidi kwa kuwa hata wanapoeleza kuwa wana hali mbaya sehemu za siri, hutakiwa kupeleka kipimo cha mkono na baadaye kuambiwa kuwa wanaugua UTI.

UTI sasa ni kila sehemu kiasi kwamba matokeo yanayoonyesha tatizo hilo yameanza kutiliwa shaka. Je, ni tatizo la vipimo kutokuwa sahihi; au kuzidi kuenea kwa UTI au ni mbinu ya madaktari hasa wa hospitali binafsi kuongeza mapato ya taasisi zao.

Mkoani Kilimanjaro, usahihi wa vipimo vinavyotolewa katika taasisi binafsi za utabibu umeibua sintofahamu kwa wagonjwa, huku baadhi wakihisi wanabambikiwa magonjwa ili walazimike kununua dawa.Uchunguzi wa gazeti hili uliofanywa kwa wiki nzima kwa kuwahoji wadau wa wafya, wakiwamo wagonjwa na madaktari, umebaini uwepo wa udanganyifu katika vipimo kwa maslahi ya kibiashara.

Baadhi ya wagonjwa waliofanyiwa vipimo katika zahanati, vituo vya afya na hospitali binafsi, waliambiwa wanasumbuliwa na maambukizi ya njia ya mkojo (UTI), brurela au malaria.

“Nilibambikiwa brusela wakati nilipokwenda kituo cha afya (anakitaja), wakati sikuwa naugua ugonjwa huo,” alisema mwanamke mmoja mkazi wa Soweto mjini Moshi.

“Kichwa kilikuwa kinaniuma sana. Mume wangu akanipeleka kituo cha afya wakachukua damu, mkojo na baadae majibu yalipotoka niliambiwa nina brusela. Nilihoji sana inakuwaje?” alisema.

 Brucellosis au brusela ni ugonjwa unaoambukizwa kutoka kwa mnyama kwenda kwa binadamu na upo kwenye wanyama wa porini na wanyama wa nyumbani kama ng’ombe na dalili ni kichwa kuuma.

Mwanamke huyo alidai kuna dawa moja ilikosekana akaandikiwa akainunua duka la dawa lakini alipofika, mhudumu alimuuliza ni dawa kwa ajili ya ugonjwa gani akamjibu brusela.

 “Akaniuliza umepimia wapi nikamtajia. Akaniambia nilijua tu. Kila mgonjwa anayepita hiyo hospitali anaambiwa ana brusela. Akanishauri niende kupima hospitali ya Serikali,”alidai mwanamke huyo.

Mwanamke huyo, ambaye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema alipopimwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC, aligundulika kuwa na ujauzito na si brusela lakini tayari alishanunua lundo la dawa.

Kutokana na tatizo hilo kuzidi kuwa kubwa, mkazi wa Pasua mjini Moshi, Neema Alfonsi aliishauri Wizara ya Afya kuchunguza hospitali zinazotoa majibu yasiyo sahihi ya vipimo, hasa ugonjwa wa UTI.

“Haiwezekani kila mtu akilalamika kuumwa kichwa, anaambiwa ana UTI. Kama kama kuna maambukizi makubwa hivyo ya UTI, kwanini Serikali isitangaze huo ugonjwa kuwa ni janga?” alihoji Neema.

Hali ni kama hiyo mkoani Arusha ambako baadhi ya vituo binafsi vya afya vinadaiwa kuwapa wagonjwa majibu ya vipimo yanayoonyesha wanaugua UTI au malaria.

Uchunguzi uliofanywa na mwananchi, katika baadhi ya vituo vya afya wilayani Arumeru, umebaini kuwa licha ya jiji la Arusha kutajwa kutokomeza ugonjwa wa Malaria, bado wagonjwa wamekuwa wakipewa majibu ya yanayoonyesha wana ugonjwa huo.

Mkazi mmoja wa mjini Arusha, Ester Mallya alisema imekuwa ni nadra sana kwa mgonjwa kuelezwa kuwa haugui malaria au UTI.

“inawezekana kuna biashara wanafanya ama hawana vipimo halisi na hivyo hawatoi majibu sahihi,” alisema.

Lakini mkurugenzi wa Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya, Dk. Godlove Mbwanji ana wasiwasi kuhusu utafiti unaoonyesha kufanana kwa matokeo ya vipimo vya wagonjwa.

“Inawezekana sampling (sampuli) aliyofanya haikuwa na usawa na aliowauliza pengine wengi wanaumwa ugonjwa huo,” alisema Mbwanji.

“Angefanya utafiti vizuri angegundua wengi wanaugua ugonjwa mwingine kuliko huo.”

Alisema ingekuwa vyema kama utafiti huo ungetoa takwimu zinazoonyesha watu wengi majibu yao yanaonyesha ugonjwa fulani kuwa juu ukilinganisha na ugonjwa mwingine. Lakini Dk, Mbwanji alikiri kuwepo kwa tatizo la majibu ya vipimo kufanana, hasa kwa wanawake wanaobainika kuwa na UTI.

“Ni kweli zipo baadhi ya hospitali za binafsi, siyo zote,  ambazo zinakosa wataalamu wenye ujuzi wa kutosha, jambo linalosababisha kushindwa kutafsiri vizuri wanachokiona au kubaini kwenye sampuli wanazopima na kusababisha  kutoa majibu yasiyo sahihi,” alisema Dk Mbwanji. Alisema wakati wa kupima, wanawake wakieleza kuwa wanatoka uchafu sehemu za siri, hutakiwa kupeleka mkojo kwa kuwa hospitali hizo hazina madaktari wenye ujuzi wa kutosha. Alisema si sahihi kupima mkojo kwa tatizo la uchafu kutoka sehemu za siri.

Dk. Mbwanji alisema hospitali binafsi ni biashara hivyo baadhi ya madaktari wako radhi kukuandikia ugonjwa hata ambao hauna kwa lengo la kuhakikisha wanauza dawa na wengine huenda mbele zaidi kuwapatia wagonjwa dawa ambazo hata haikuwa lazima kutumia.

Alisema hali hiyo haiwezi kutokea katika hospitali za serikali ambako daktari hana maslahi ya moja kwa moja.

“Nimewahi ona baadhi ya madaktari wakiacha kazi tu kwa sababu waajiri wao wanawataka kuwaandikia dawa wagonjwa hata kama hawajaona ugonjwa wowote ili mradi dawa zitoke zisikose wateja,” alisema Mkurugenzi huyo.

Madaktari wengine waliohojiwa na Mwananchi kuhusu tatizo hilo, walitilia shaka vipimo vya brusela wakisema ni ugonjwa unaopatikana zaidi kwenye jamii ya wafugaji wanaokula nyama au maziwa mgando yasiyochemshwa.

 Profesa John Shao aliyebobea katika Mikrobiolojia, alisema yapo mambo mengi yanachangia kuwepo kwa majibu yanayofanana ya vipimo vya wagonjwa kutoka katika maabara, zahanati, vituo vya afya na Hospitalini.

Profesa Shao, aliyewahi kuwa mkurugenzi mwendeshaji wa KCMC, alisema vipo vishawishi vinavyofanya upimaji wa sampuli za wagonjwa,usilenge sayansi au majibu ya kisayansi. Alisema moja ya sababu hizo ni kutokuwa na wataalamu wa kutosha katika fani mbalimbali za maabara na kutokuwa na mfumo wa usimamizi na ufuatiliaji wa wataalamu waliopo wa maabara.

 “Vituo vyetu havina wataalamu wa kutosha katika kushughulikia sampuli za wagonjwa wa aina tofauti. Wanalazimka kupima kila sampuli ya mgonjwa anayefika na kuhitaji vipimo,” alisema.

“Maabara au vituo vyetu vya maabara havizingatii maadili ya upimaji stahiki. Mgonjwa atatakiwa kutoa damu lakini hafahamu inapimwaje,”alisema.

“Baadhi ya maabara kutoelewa au kutokuwa na vigezo vya upimaji wa aina fulani ya vijidudu kwenye sampuli zinazotolewa nalo ni tatizo. Maabara zinatofautiana kiuwezo na hata vifaa.” Profesa Shao alisema hakuna  mfumo unaofuatilia kama maabara kufanya kazi kulingana na uwezo au kibali chake.

Mkurugenzi mtendaji wa KCMC, Dk. Gilliard Masenga pia alithibitisha kuwapo kwa tatizo la kufanana kwa vipimo katika baadhi ya zahanati na vituo binafsi vya afya.

“Kuna shida mahali. Hakuna tishio kubwa kiasi hicho,”alisema.

 “Hapa kwangu (KCMC) inaweza kupita miezi sita hatujapata mgonjwa wa malaria. Lakini huko mitaani unasikia watu wengi wanaopima wanaambiwa wana malaria mara UTI au typhoid,” alisema.

 Dk Masenga alisema vitendo vya kutoa majibu ya uongo, husababisha usugu wa dawa kwa kuwa wagonjwa wanapewa dawa zenye nguvu kubwa kama Ciproflaxin na Gentamycin.

“Unajiuliza hivi huyu mgonjwa akipata kweli ugonjwa wa UTI au typhod au brusela utamtibu kwa dawa gani wakati ulishampa dose (dawa) ya juu kwa ugonjwa ambao wala hakuwa nao?”alihoji. Imeandikwa na Daniel Mjema, Florah Temba, Maryasumpta Kavishe, Mussa Juma na Yonathan Kossam