UCHAMBUZI: Kutojiandikisha kupiga kura kupatiwe dawa

Uandikishaji wapigakura kwa ajili ya kushiriki uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24 mwaka huu, umekamilika ukiacha funzo kubwa.

Funzo kubwa limetokana na kitendo cha Serikali kulazimika kuongeza siku tatu kutokana na idadi ndogo ya wananchi kujitokeza kujiandikisha.

Baada ya kuongezwa muda tumeambiwa idadi iliongezeka kutoka milioni 15.1 hadi kufikia milioni 19 sawa na asilimia 86 ya lengo la watu milioni 22.9.

Kwa mujibu wa ratiba ya awali, Oktoba 29 wagombea walitakiwa kuchukua fomu, hivyo ni wazi kuongezwa kwa siku za uandikishaji kutaathiri ratiba nyingine.

Ili kuepuka hali hiyo, sintofahamu hii ya watu kusuasua kujiandikisha kupiga kura inapaswa kufanyiwa kazi na mamlaka za usimamizi wa chaguzi, Serikali, wadau wa uchaguzi na vyama vya siasa.

Jambo hili halitakiwi kuchukuliwa poa na likaachwa hivihivi bila kufanyiwa uchunguzi wa kina kubaini nini ambacho kimewafanya wananchi kusuasua kujiandikisha kupiga kura.

Miongoni mwa sababu zinazoelezwa ni kupungua siasa za ushindani nchini, hasa baada ya vyama vya upinzani kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara na wananchi kupunguza imani na wasimamizi wa chaguzi zetu.

Lakini pia kuna wapo wanaoeleza kuwa kitendo cha baadhi ya viongozi kama madiwani, wabunge na wenyeviti wa vijiji na mitaa waliochaguliwa na vyama vya upinzani kujiunga na chama tawala na baadhi yao kuchaguliwa tena kushika nyadhifa waliojiuzulu kumewavunja moyo wananchi.

Sababu nyingine ambayo inatajwa ni kukosekana uhamasishaji wa watu kujitokeza kujiandikisha hasa kutokana na mfumo wenyewe wa chaguzi kutotoa fursa ya mikutano ya kampeni kuanza kabla ya kujiandikisha.

Wananchi pia wanaeleza kushindwa kutimiza wajibu wao viongozi wa vijiji na mitaa pia kunaweza kuchangia watu kutoona umuhimu wa kuchagua viongozi hao.

Lakini kuna kauli za baadhi ya viongozi kuwa ni lazima wagombea wa vyama vyao washinde nazo zimechangia kuonyesha kuwa hata kama wananchi wakijitokeza kupiga kura huenda waliowachagua wasitangazwe.

Pamoja na hizi zinazotajwa na wananchi, naamini taasisi zenye mamlaka na uchaguzi zitakuwa na sababu za zaidi za kitafiti ambazo zitabainisha kinagaubaga nini chanzo cha wananchi kutojitokeza kujiandikisha kupiga kura.

Hata hivyo wakati tukisubiri taarifa za kiuchunguzi ni muhimu sana mamlaka zinazosimamia chaguzi, kujifunza kwa kilichotokea na kama ikiwezekana zianze kutafuta dawa ya mkwamo huu.

Nasema mkwamo kwa sababu, inaweza kutokea mwenyekiti wa kijiji, diwani au mbunge kuchaguliwa na watu wasiofikia hata robo ya ambao atawaongoza.

Jambo hili litakuwa na athari, kwanza linamuondolea uhalali kiongozi aliyechaguliwa, lakini pia linamfanya akose ushawishi wa kuhamasisha maendeleo katika eneo lake.

Lakini pia kuchaguliwa na watu wachache kunamuondolea nguvu ya ushawishi kiongozi kwa kuwa watu anaowaongoza ama watakuwa hawampendi au hawamuamini.

Ikiwa suala hili litachukuliwa poa linaweza kuja kuwa na athari kubwa mbele ya safari kwa kuwa na viongozi wa kuchaguliwa ambao hawajachaguliwa na wananchi hivyo kutokuaminiwa.

Lakini pia vyombo vingine ambavyo vinahusika na udhibiti wa wanasiasa vijifunze kuwa na mipaka ya maamuzi yao, kwani badala ya kuleta amani na utulivu inaweza kuleta chuki katika mioyo ya watu.

Lakini pia ni muhimu kuruhusu uhuru wa watu kutoa maoni katika mambo mbalimbali na kupokea mawazo mbadala ili kila Mtanzania ajione anaweza kuwa na mchango ndani ya taifa lake.

Kukaa kimya na kuona si jambo la ajabu, kunaweza kusababisha athari kubwa mbeleni na wahenga walisema asiyeziba ufa atajenga ukuta.

Nitoe wito kwa ambao hawajajiandikisha, hasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa mwakani wakajiandikishe ili watimize wajibu wao wa kikatiba kuchagua kiongozi ambao wanamtaka.

Ni vyema kila mmoja akajiandikisha na kwa kufanya hivyo atakuwa ametimiza lengo lake la kidemokrasia, lakini atakuwa na uhalali wa kuchaguzi kiongozi anayemtaka.

Mussa Juma ni mwandishi mwandamizi wa Mwananchi: 0754296503.