Kutokwa damu ukeni kwa watoto, watu wazima

Muktasari:

  • Sababu za wajawazito kutokwa na damu ukeni huwa ni kuharibika kwa mimba

Tatizo la kutokwa na damu ukeni ni moja ya mambo yanayowashtua na kuwakosesha amani wanawake.

Zipo sababu za ujumla zinazochangia tatizo hili kutegemea na makundi ya wanawake.

Mara chache inaweza kutokea na kuwashtua watu wengi pale mtoto mdogo wa chini ya mwaka mmoja anapopata hali hii. Kwa watoto wa umri huu kutokwa na damu ukeni sababu huwa ni kusisimuliwa kwa tando nyororo ya nyumba ya uzazi na homoni ya kike ijulikanayo kama ostrogens inayokuwapo katika kondo la nyuma.

Hali hii ndiyo inayosababisha kutokwa na damu kiasi ukeni kwa watoto waliozaliwa.

Kwa watoto wa umri wa mwaka mmoja kuendelea sababu zinaweza kuwa ni kujijeruhi, uwapo wa kitu kigeni ukeni, shambulizi ukeni, kuporochoka kwa kitundu cha mrija wa mkojo na kuvunja ungo kabla ya wakati.

Kwa wanawake ambao wako katika umri wa kuweza kubeba ujauzito waotokwa sana damu ukeni na kupoteza fahamu ghafla mara nyingi huwa ni ujauzito ulitunga nje ya nyumba ya uzazi na kupasuka.

Wanawake ambao tayari ni wajawazito sababu za kutokwa na damu ukeni huwa ni kuharibika kwa mimba, mimba kutunga nje ya nyumba ya uzazi, shambulizi la tando nyororo katika nyumba ya uzazi na kubaki kwa mabaki ya mimba.

Kwa upande wa wanawake ambao si wajawazito matatizo ya mara kwa mara yanayochangia kutokwa na damu ukeni ni pamoja na matatizo yanayohusishwa na vichochezi (hormons).

Matatizo hayo ni pamoja na tatizo linalowapata sana lijulikanalo kitabibu Dysfunctional Uterine Bleeding (DUB), uvimbe katika ubongo, matumizi ya dawa za uzazi wa mpango, matatizo wa tezi ya Thyroid iliyopo shingoni, uvimbe au saratani katika ovari.

Sababu zingine kwa kundi hili ni pamoja na matatizo katika viungo vya uzazi ikiwamo saratani, uvimbe, majeraha ya awali ya upasuaji, matatizo ya shingo ya uzazi ikiwamo uvimbe wa kawaida, saratani au jeraha katika mlango wa nyumba ya uzazi, matatizo ya misuli ya nyumba ya uzazi (Myomas au Fibroid).

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa binadamu.