Kwa dalili hizi, unakaribia kupata shambulio la moyo

Leo kupitia safu hii nitaeleza baadhi ya dalili kuu zinazojitokeza kwa takribani mwezi mmoja kabla ya kupata matatizo ya moyo hasa shambulio la moyo.

Watu wengi wamekuwa hawazifuatilii dalili hizo na kuzitilia maanani kwa sababu hawajui kama zinaashiria tatizo kubwa kwenye afya zao.

Unapoona dalili hizi ni vyema ukawa makini na kutafuta ushauri wa daktari kwa msaada zaidi wa kiafya kwa sababu, mara nyingi huwa zinaashiria hatari ya kupata shambulio la moyo.

Uchovu usio wa kawaida; ni moja ya dalili kuu zinazoashiria kuwa mtu yupo hatarini kupata shambulio la moyo.

Dalili hii mara nyingi hutokea zaidi kwa wanawake kuliko wanaume. Japo ni kawaida kupata uchovu kutokana na shughuli mbalimbali tunazozifanya kila siku ambazo zinatumia nguvu kubwa za mwili au pia zinatumia akili nyingi.

Ni muhimu kuutilia maanani uchovu unaodumu muda mrefu na hata kusababisha kushindwa kufanya shughuli ndogo ndogo za nyumbani.

Maumivu ya mwili yasiyo ya kawaida; nayo ni kiashiria cha shambulio la moyo.

Maumivu hayo hujitokeza sehemu mbalimbali za mwili, yakiwamo ya tumbo na kuhisi tumbo limejaa gesi, kichefuchefu au kuvurugika kwa tumbo.

Dalili hizi huwapata watu wa jinsia zote kwa kiwango sawa. Tofauti na maumivu haya ya tumbo, pia kuna maumivu ya mwili kama vile kifua na maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.

Kukosa usingizi; tatizo hili la kukosa usingizi, kiafya linahusishwa na hatari kubwa ya kupata magonjwa ya moyo na hasa shambulio la moyo na kupata kiharusi.

Hii hujitokeza zaidi kwa wanawake japo wanaume pia huwapata, lakini takwimu zinaonyesha wanawake ndiyo wanaopatwa na matatizo ya kukosa usingizi mara kwa mara.

Hivyo ni vyema kuwa makini, kama mtu anakosa usingizi mara kwa mara kwa kuchelewa kulala au kuwahi zaidi kuamka bila sababu.

Kukosa pumzi na kupata matatizo kwenye mfumo wa upumuaji mara kwa mara; pia ni dalili ya ugonjwa huo.

Wakati mwingine mtu anaweza kupata hali isiyo ya kawaida wakati wa kupumua hasa kuvuta hewa.

Mwandishi wa makala haya ni daktari kutoka Hospitali ya TMJ SUPER SPECIALIZED POLYCLINIC.