UCHAMBUZI: Kwa hili Nida mnapaswa kubadilika haraka

Wazo la kuanzisha vitambulisho vya Taifa kwa raia wa Tanzania na wageni waishio nchini lilianza mwaka 1968 katika kikao kilichojumuisha wajumbe kutoka nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Zambia.

Kwa wakati huo nchi za Kenya na Zambia tayari zilikuwa na vitambulisho vyao vya Taifa.

Kutokana na uhusiano wa kiusalama unaozingatia utawala wa sheria katika nchi hizo ilionekana lazima nchi za Uganda na Tanzania nazo zikatoa vitambulisho vya Taifa kwa raia wao.

Mwaka 1986, Serikali ilitunga sheria ya vitambulisho. Hata hivyo, sheria hiyo haikutumika wala kutungiwa kanuni zake.

Mwaka 2006, Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete alitia saini hati ya kuidhinisha kuanzishwa kwa chombo cha kusimamia vitambulisho vya Taifa kinachojulikana kama Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).

Faida mojawapo ya kuanzisha kwa vitambulisho hivyo ni kuongeza wigo wa mapato ya Serikali, kusaidia kumtambua mhusika kirahisi anapohitaji kupatiwa huduma katika taasisi mbalimbali kama benki, taasisi za mikopo na huduma za afya.

Pia vitasaidia kuweka kumbukumbu vizuri za uhalifu na kumtambua mhusika.

Hivyo, Serikali iliifanya Nida iwe chombo cha kusimamia na kutoa vitambulisho kwa Watanzania na wageni wanaoishi nchini kihalali.

Kumekuwa na jitihada mbalimbali za Serikali kuhakikisha Watanzania na wageni wakazi wote wanapatiwa vitambulisho hivyo.

Lakini jitihada hizo hazikuzaa matunda yaliyotajariwa kwa kipindi kirefu kutokana na sababu mbalimbali.

Ni wazi kwamba kwa wakati huu kuna umuhimu mkubwa wa kuwa na vitambulisho vya Taifa kulingana na mazingira yaliyopo na kurahisisha masula ya kiusalama.

Kuanzishwa kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambako nchi tano ziliungana na kukubaliana kwamba watu wa nchi hizo wanaweza kutembeleana bila bughudha pia kumeongeza umuhimu wa kuwa na vitambulisho hivyo.

Pamoja na umuhimu huo unaoonekana kutokana na vitambulisho hivyo lakini mchakato mzima wa upatikanaji wa vitambulisho hivyo bado umegubikwa na changamoto lukuki.

Mwanzoni Nida iliweka utaratibu mzuri wa kuwafikia wananchi kupitia mitaa na vijiji vyao ambako maafisa wa taasisi hiyo wlaiweka kambi kwa ajili ya taraibu za kujiandikisha.

Hakika watu waliitikia na kujiandikisha kwa wingi kwa ajili ya vitambulisho hivyo.

Baada ya mzunguko huo kukamilika wananchi waliobaki bila kujindikisha waliendelea kuhamasishwa kwenda Nida kwenye wilaya zote kwa ajili ya kukamilisha taratibu hizo.

Uhamasishaji huo umechagizwa zaidi baada ya Serikali kusema kwamba laini za simu lazima zisajiliwe upya kupitia mfumo wa kielektroniki kwa kutumia alama za vidole na moja ya vigezo vya usajili huo mpya ni kuwa na kitambulisho cha Taifa.

Usajili huo mpya wa kutumia vidole ulianza tangu Mei Mosi mwaka huu, na tayari Mamlaka ya Mawasiliano (TCRA) imeshatangaza kwamba ifikapo Desemba laini zote ambazo zitakuwa hazijasajiliwa zitafungiwa na hazitaweza kutumika.

Wapo watu waliojiandika tangu mwaka jana cha kushangaza hadi sasa hawajapata vitambulisho vyao hatua inayowafanya wengine kukata tamaa na kuona kama wanazungushwa.

Wapo pia watu wanashinda kwenye ofisi za Nida wakijipanga kwenye mstari kuanzia asubuhi hadi jioni lakini taarifa za kitambulisho vyao hazijapatikana au usajili wao haujakamilika licha ya kupita miezi kadhaa.

Kutokana na kuchelewa kwa taratibu za kupata kitambulisho Nida ilitangaza mwananchi kutumia namba tu ya kitambuliho wakati akiendelea kusubiri kitambulisho kamili.

Cha kushangaza bado upatikanaji wa namba ya kitambulisho cha mhusika ni kizungumkuti.

Nachelea kusema kwamba huenda hata ikafika mwakani Nida isikamilishe usajili wa Watanzania wote hata baada ya muda wa mwisho uliotolewa kwa ajili ya usajili wa laini za simu.

Ombi langu kwa Nida ijitathimini utendaji wake na kujipanga upya ili kuhakikisha Watanzania wote wanaandikishwa na kupata vitambulisho hivyo ili iwe rahisi kujisajili katika masuala ya msingi ikiwa ni pamoja na laini za simu kabla muda uliotolewa haujamalizika.

Ni wakati sasa kwa Nida kujipanga upya na kuweka kambi kila mtaa na vijiji kama ilivyofanyika awali.

Jesse Mikofu anapatikana mkoani Mwanza kwa simu 0755996593.