Kwa nini watu hupata choo kigumu?

“Nilikuwa napata choo laini (haja kubwa) kila siku, lakini baadaye kilibadilika. Nilianza kupata choo kigumu mara mbili kwa wiki.

“Nilistaajabu lakini hakikunisumbua sana mpaka nilipoanza kupata kigumu zaidi kilichoniumiza kila nilipokwenda haja kubwa,” anasimulia Jenifer Swai.

Tatizo hilo lililomkumba Swai (27), limekuwa likiwakabiliwa watu wengi nchini, japokuwa hukwepa kulizungumza.

Akisilimulia zaidi, Swai anasema ilifikia hatua alitokwa damu kila alipokwenda haja kubwa pamoja na kuota kinyama sehemu ya haja kubwa, ndipo alipokwenda hospitali na kuambiwa ana ugonjwa wa bawasiri, hivyo lazima afanyiwe upasuaji.

“Sikuwa na jinsi kwa kuwa matibabu pekee ilikuwa ni upasuaji, baada ya upasuaji nilipewa dawa na kuelekezwa namna ya kupangilia mlo wangu sasa niko sawa.”

Tatizo la kufunga choo au kupata kilicho kigumu, limekuwa sugu miongoni mwa watu wengi.

Daktari bingwa wa magonjwa ya mfumo wa chakula katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Masolwa Ng’wanasayi anasema choo (kinyesi) kimetofautiana baina ya mtu mmoja na mwingine kulingana na maumbile yao.

Anasema utofauti huo unasababisha mwingine kupata choo zaidi ya mara moja kwa siku huku wengine wakipata zaidi ya mara tatu kwa wiki.

Dk Ng’wanasayi anasema kwa kawaida mwili wa binadamu una mmeng’enyo wake wa chakula, hivyo kupata choo zaidi ya mara tatu kwa wiki ni sahihi kwa binadamu ila kupata mara mbili ni tatizo na mtu huyo lazima atapata choo kigumu.

“Baadhi ya watu wanapata choo mara mbili au tatu kwa siku, hii ni kawaida, lakini inatakiwa angalau zaidi ya mara tatu kwa wiki, lakini ikiwa chini ya hapo ni hatari kwa afya ya mhusika.”

Dk Ng’wanasayi anasema mtu anayepata choo kila siku lazima kitakuwa laini, lakini anayepata pungufu ya mara mbili kwa wiki kitakuwa kigumu.

Anasema kwa kawaida mtu akishakula chakula, baada ya mmeng’enyo mabaki huingia kwenye utumbo mpana na huko ndiko kinyesi kinakotengenezwa, kwa kuwa huwa na majimaji ambayo huchujwa na hatimaye kupatikana kinyesi.

Anasema chakula kinapoingia tumboni huchukua takribani saa sita hadi nane ndipo hufika katika utumbo mpana na huko huchukua zaidi ya saa 48 kabla ya kuwa kinyesi.

“Mabaki ya chakula yapo kama majimaji, kazi inayofanyika katika utumbo mpana ni kufyonza maji maji na kutengeneza choo; kwa kuwa utumbo mkubwa haufanyi kazi ya kunyonya chakula ila kuchanganya choo. Kila muda unavyokwenda, choo kinazidi kuwa kigumu ikiwa huyu mhusika hajapata vyakula vyenye majimaji kwa wingi,” anasema Dk Ng’wanasayi.

Pia, anasema suala la kupata choo kigumu au kupata kwa nadra, halina uhusiano na aina ya vyoo.

Akizungumzia watoto kukosa choo, anasema hupata tatizo hilo ikiwa hawapati maji ya kutosha.

Husababisha magonjwa

Dk Ng’wanasayi anasema kufunga kwa choo au kupata kigumu, ndiyo chanzo cha ugonjwa wa bawasiri.

Anasema mtu anayepata choo kigumu yupo hatarini kupata ugonjwa huo kwa sababu atakuwa akitoa choo kigumu mara kwa mara hali inayosababisha mishipa kukwanguliwa na kinyesi.

“Unaweza kupata madhara kama ugonjwa wa bawasiri, hii husababishwa na kukwanguliwa kwa mishipa ya damu ambayo kama unapata choo kigumu ile mishipa inatanuka na vitatokea vivimbe ambavyo unapojisaidia vinatoka nje na baadaye unajitokeza uvimbe mkubwa kwa nje sehemu ya haja kubwa,” anasema.

Tatizo jingine anasema ni kutokwa na damu wakati wa kujisaidia kutokana na kukwanguliwa wa mishipa na wakati mwingine kama tatizo limekuwa kubwa matibabu pekee ni upasuaji.

Pia, anasema wengine hupata vidonda njia ya haja kubwa.

Dk Ng’wanasayi anasema tatizo kubwa zaidi linaloweza kusababishwa na kupata choo kigumu ni saratani ya utumbo mpana.

“Kukaa na choo kwa muda mrefu kwenye utumbo mpana hutengenezwa bakteria kwa wingi ambao wana athari, hawa huzalisha sumu ambayo husababisha kupata saratani kwa miaka ijayo,” anasema Dk Ng’wanasayi.

Pia, anasema itategemea mhusika anakula vyakula vya aina gani, ikiwa anakula vyakula vyenye kemikali au vilivyokobolewa kwa wingi ni hatari kwake kupata saratani miaka ijayo.

Wakati mwingine wagonjwa wanaweza kupata tatizo hilo ikiwa wanaugua kisukari, lakini Dk Ng’wanasayi anasema si wote wenye kisukari wanaweza kupata tatizo la choo kigumu.

Pia, anasema kukosa choo husababishwa na tatizo la kisaikolojia, hivyo wakati wa kujisaidia mhusika hujenga hofu na kusababisha kukakamaa kwa choo.

Fanya haya kuepuka choo kigumu

Dk Ng’wanasayi anasema hakuna maisha bila maji, hivyo ni ajabu kuona mtu anamaliza siku nzima au hata mbili bila kunywa maji.

Anasema asilimia 75 ya mwili ni maji, asilimia 85 ya ubongo ni maji na asilimia 94 ya damu ni maji.

Mtaalamu huyo anasema kwa kuwa kazi ya utumbo mpana ni kufyonza maji, ikiwa haunywi ya kutosha ni rahisi kupata choo kigumu.

Dk Ng’wanasayi anasema kwa kawaida kila siku mtu mzima anapaswa kunywa maji lita mbili mpaka tatu na hiyo inategemea uzito na umri wa mhusika.

“Hii inasaidia wakati utumbo unafyonza maji yatabaki mengine kwa ajili ya kulainisha choo, mara nyingi mtu anayekunywa maji ya kutosha hupata choo kila baada ya siku moja,” anasema.

Ng’wanasayi anasema ikiwa unataka kupata choo laini na cha kawaida, basi jitahidi uwe mtu wa kutembea tembea na si kukaa tu kwenye kiti kutwa nzima.

“Jitahidi kila siku uwe unapata muda wa kutembea tembea kwa miguu hadi dakika 60 au zaidi. Hii itakusaidia kuondoa tatizo la kufunga choo au kupata choo kigumu sana na wakati mwingine kufanya hata mazoezi ya kawaida itasadia kwa kiasi kikubwa,” anasema.

Anataja vyakula vya nyuzi (fiber) kuwa ni mingoni mwa vyanzo vya kupata choo laini na kisicho na madhara kwa mwili wa binadamu.

Anasema mara nyingi madaktari wamekuwa wakiwasisitiza wagonjwa kuhusu umuhimu wa kula vyakula vya asili na vyenye nyuzinyuzi.

Dk Ng’wanasayi anasema chakula cha asili kina nafasi kubwa katika kuimarisha afya yako kwa ujumla.

“Hakikisha pia asilimia 80 ya mlo wako kwa siku ni matunda na mboga za majani. Matunda kama ndizi na parachichi ni muhimu kula kila siku, kadhalika tumia unga wa dona na usipendelee kula vyakula vilivyokobolewa kwa wingi,” anashauri Dk Ng’wanasayi.

Pia, anasema kufanya mazoezi ya kuchuchumaa na kusimama ni mazuri na muhimu kwa mtu anayesumbuliwa na tatizo la kufunga choo au kupata choo kigumu sana.

“Hakikisha asilimia 80 ya chakula chako kwa siku iwe ni matunda na mboga za majani. Unapokuwa na hili tatizo, pendelea zaidi parachichi, papai na juisi ya ukwaju. Kula matunda siyo mpaka uumwe au ushauriwe na daktari, fanya kuwa ndiyo tabia yako kila siku na hautakawia kuona mabadiliko makubwa kwa afya yako kwa ujumla,” anasema Dk Ng’wanasayi.