UCHAMBUZI: Kwanza jitafute, jitambue, baada ya hapo jikubali

Saturday April 13 2019GASTON NUNDUMA

GASTON NUNDUMA 

Kujitambua ndio mwanzo wa mambo yote. Mambo makuu katika maisha ya mwanadamu huweza kuonekana pale tu mtu anapojitambua yeye ni nani hasa. Kwa kawaida wengi wetu tunajihisi kuwa kama tunavyojidhania, lakini ukweli ni kuwa bado hatujitambui.

Wengine wanajiweka katika nafasi fulani kwa kujisikiliza sauti zao za ndani. Hili ni kosa kubwa kwa vile kujipangia nafasi ni kujipandisha ama kujishusha. Jambo hili huweza kumpotezea mtu ukweli wa yeye ni nani hasa. Pengine anaweza kupoteza thamani kwa jamii yake.

Lakini, kujitambua si jambo rahisi sana. Unaweza kudhani kuwa wewe ni mtu wa aina fulani wakati si kweli. Wakati mwingine mtu hulazimika kujitafuta kwa nguvu zote kabla ya kufikia hatua ya kujitambua. Hapa zaidi ya wewe mwenyewe, wazazi na marafiki wa karibu wanaweza kuhusika.

Wazazi wanaweza kujua thamani ya mtoto wao kabla hajajitambua. Kwa mfano anaweza kulazimisha uchekeshaji au uoneshaji wa mavazi kutokana na sura au umbo analolibeba ukubwani, lakini wazazi wakamtambua kipaji chake cha sayansi na ugunduzi wa mambo ya kale tangu utotoni.

Hivyo historia ni jambo la msingi katika kujitafuta kabla ya kujitambua. Kila mtu ameumbwa na namna yake ya kufikiri, kuakisi mambo, kupambana na changamoto, kudhibiti hisia, kutunza kumbukumbu na kuendeleza mahusiano.

Kama ilivyo kwa watu wazima, watoto wanaonyesha fani zao tangu mapema. Ndiyo maana hucheza kama dakitari, injinia, mchungaji, mwana kandanda na kadhalika katika michezo yao ya mchangani. Sote tunaamini wanakua kwenye fani hizo mpaka pale wanapokuja kuathiriwa na makuzi au masomo.

Advertisement

Mara nyingi watu wanafeli kwa kushindwa kugundua nafasi zao. Wengi hudhani kuwa wapo kwa kusubiri kipato kikubwa badala ya kuzingatia kufanya kazi zao ili kuingiza kipato hicho. Wengine huona kazi za kipato cha haraka ndizo za kwao.

Tunaona wanafunzi wengi wakichagua mikondo ya masomo kwa kutazama wepesi wa ajira bila kutazama uwezo wao kwenye masomo hayo, au mahitaji ya jamii kwenye masomo hayo. Umakini wa ziada unapaswa kutumika katika kujitafuta.

Mfano mwingine tunauona kwa kijana anayedhani mafanikio ya sanaa huja baada ya kuwa msanii. Inawezekana kijana huyu akawa na mvuto mkubwa katika biashara ya sanaa kuliko kuimba, kuchonga au kuigiza. Kama angeingia kwenye sanaa katika nafasi za masoko angeweza kufanya vizuri kuliko katika nafasi anayoichagua.

Ili ufanikiwe katika hili huna budi kujua nguvu zako, kutambua mahitaji yako na kuzingatia thamani ya wanaokuzunguka. Mahatma Gandhi alisema njia nzuri ya kujitafuta ni kujishusha mbele ya watu wengine. Kwamba kuwa mdogo kutawafanya wengine wawe wakubwa na waanze kukushauri.

Kuna ukweli kwamba watu walio nje ya jambo huwa kwenye nafasi nzuri ya kulichambua kuliko walio ndani yake. Kwa hivyo wengine wanaweza kuona nguvu na uwezo wako zaidi ya unavyoweza kujiona mwenyewe. Pia, wanaweza wakakueleza mengi kwa peo zao tofauti na unavyoona kwa upeo wako binafsi.

Ugumu ni kwamba tulipokuwa utotoni hatukuwa na maamuzi ya kuzaliwa na kuishi kwenye familia tulizopenda. Tulielekezwa jinsi ya kuishi na masomo ya kusoma. Baada ya kuhitimu hatukuwa na budi kufanya kazi tulizosomea. Wengine miongoni mwetu walilazimika kuachana na fani walizozipenda.

Tulipokuwa wakubwa tulichagua aina ya maisha kama nguo za kuvaa, wake/waume wa kuishi nao, vyakula na hata vinywaji vya kutumia. Lakini, mpaka sasa hatujawaachia watoto wetu wajitafute na wajichagulie njia zao nasi tukakubali kubaki kama washauri wao.

Kwa hali ya maisha ya sasa hakuna mzazi aliye tayari kujaribu kipawa cha mwanaye. Macho yote yameelekezwa kwenye kada zenye uhakika wa ajira, na hasa zile zinazolipa kwa haraka na uhakika. Kama mtoto alizama kwenye mapenzi ya uinjinia au udakitari basi inabidi afumbe macho na masikio ili afikie malengo yake. Yule mtafiti wa masanamu ya kale ndio kabisa, inabidi awe nusu kichaa ili afikie lengo.

Zipo nyakati ambazo tulikuwa tukiwaona madakitari, mainjinia na wahasibu wakiwa wanacheza mpira au kupiga muziki. Si kwamba taaluma zao hazikuwalipa sawasawa, bali aliweza kusomea taaluma yake bila kuathiri kipaji chake halisia.

Lakini kwa woga wetu hivi sasa kama nilivyosema hakuna anayethubutu kumruhusu mwanaye ajaribu kuendeleza kipaji. Wakati mwingi tunawaza kuharibikiwa na taaluma kwa “mambo yasiyo na msingi”. Kwa kufanya hivi tungali tunaikaza kamba ya ugumu wa kujitafuta, kujitambua na kujikubali.

Walezi wengi wanaganda kwenye mawazo kuwa mafanikio ya watoto ni kuingiza kipato kikubwa tangu mapema. Fikra hizi husogeza mbali mawazo ya kujitafuta na inawezekana watu wakarejesha mawazo haya baada ya kustaafu au kuacha taaluma zao kwa namna nyingine. Kwa hiyo wachaguzi wa maisha mepesi hivi sasa wanaongezeka, na wanaojitafuta wanazidi kupungua kama si kwisha kabisa.

Bado ninaamini kuwa mamlaka zetu zinaweza kurudisha vitabu na vipindi vya ziada mashuleni. Tunapomuongelea mstaafu wa sasa tunasema ni mkulima, mfanyabiashara na mjasiriamali wa baadaye. Ataitumia taaluma yake nje ya ajira au atajitafuta na kuanza kazi ingine. Sioni vibaya kama atapewa masomo kama Sayansi Kimu tangu akiwa mdogo ili asije kushangaa baadaye.

wengine kutokata tamaa.