UCHAMBUZI: Ligi Daraja la Kwanza ichezwe kwa ufanisi

Monday October 28 2019

 

Ligi Daraja la Kwanza Bara inaendelea kushika kasi na jumla ya timu 24 zimekuwa katika mpambano wa kusaka nafasi ya kucheza Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Timu hizo 24 zimegawanywa katika makundi mawili ambayo kila moja linajumuisha idadi ya timu 12, sasa ligi hiyo ipo kwenye raundi ya sita huku kila timu ikiwa imebakiza michezo 16 mkononi.

Ikiwa ndio kwanza imekamilisha theluthi moja ya raundi huku ikibakiza nyingine mbili, tumeshuhudia ushindani mkubwa kwa timu mbalimbali zinazoshiriki mashindano hayo katika raundi hizo sita za mwanzo tofauti na hapo awali ambapo ilikuwa ni vigumu kwa watu kuona timu zikianza kushindana katika hatua za mapema kama hizo.

Tumeshuhudia baadhi ya timu zikipata matokeo mazuri ugenini iwe ni ushindi au sare na katika hali ya kushangaza baadhi ya timu ambazo zilipewa nafasi kubwa ya kutamba kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu huu zimejikuta zikiwa kwenye wakati mgumu kwa kutokuwa na mwendo wa kuridhisha hadi sasa.

Na si tu hilo bali pia hakujaripotiwa vitendo vya hujuma kama vile upendeleo wa marefa kwa baadhi ya timu tofauti na ilivyozoeleka hapo awali na idadi kubwa ya klabu zimekuwa zikiridhishwa na matokeo mechi inapomalizika.

Kuna sababu kadhaa ambazo inawezekana zimechangia kuongezeka ushindani kwenye Ligi Daraja la Kwanza msimu huu. Kwanza ni nafasi chache za kupanda Ligi Kuu na ugumu wa mfumo unaotumika kupata timu ambazo zitakata tiketi ya kupanda daraja lakini pia uwezekano rahisi wa timu kushuka hadi daraja la pili.

Advertisement

Ifahamike kwamba timu mbili tu ndizo zitapanda Ligi Kuu moja kwa moja ambazo zitakuwa ni zile zilizoongoza makundi mawili ya Ligi Daraja la Kwanza msimu huu. Lakini pia ifahamike kwamba takribani timu nne kwa maana ya mbili ambazo zitashika mkia kwenye kila kundi zitashuka daraja hivyo hesabu za kukusanya pointi mapema ili kukwepa hatari ya kushuka inaonekana kufanyiwa kazi mwanzoni.

Pia maandalizi mazuri ambayo timu nyingi ziliyafanya kabla ya msimu kuanza kwa kufanya usajili wa wachezaji wazuri pamoja na kucheza michezo ya kirafiki, yamezisaidia kuwa na vikosi vizuri ambavyo vinaonyesha ushindani wa hali ya juu.

Ikiwa ushindani huu utaendelea kuwepo hadi mwishoni mwa msimu ni wazi kwamba tutapata timu nzuri ambazo zitaingia Ligi Kuu na kuleta ushindani badala ya kuwa wasindikizaji tofauti na ambavyo tumeshuhudia mara nyingi timu zikishuka daraja katika msimu mmoja tu baada ya kupanda

Lakini wakati ushindani kwenye Ligi Daraja la Kwanza ukizidi kuimarika, ni vyema mamlaka zinazosimamia ligi ambazo ni Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) zikaimarisha usimamizi wa ligi hiyo ili isije kuvurugika baadaye.

Kuna haja ya kuongeza uangalizi katika michezo ya ligi hiyo ili kuzuia timu na waamuzi kuhusika katika vitendo vya hujuma na upangaji wa matokeo ambavyo vimekuwa vikilalamikiwa mara kwa mara na kutajwa kushamiri kwenye Ligi Daraja la Kwanza.

Vitendo hivyo ambavyo mara kwa mara hushamiri kwenye mzunguko wa lala salama ni matokeo ya timu kulazimisha kupata matokeo kwa njia za hila badala ya kutegemea ubora na uwezo wa ndani ya uwanja.

Mwisho wa siku madhara yake huwa ni kutokea kwa vurugu ambazo husababisha uharibifu wa mali pamoja na miundombinu ya viwanja, lakini pia kusababisha timu ambazo hazina uwezo kupanda daraja huku zile zilizostahili kushindwa kufanya hivyo.

Hakuna sababu ya kusubiri hadi mambo yaharibike ndipo mamlaka husika zianze kuchukua hatua na kutoa matamko, badala yake hilo linapaswa kuanza kufanyiwa kazi mapema kabla hali haijabadilika.

Ifahamike kwamba pamoja na kutoa timu bora na ambazo zitaleta ushindani kwenye Ligi Kuu, faida nyingine ya uwepo wa ushindani wa haki kwenye Ligi Daraja la Kwanza ni kuvutia wadhamini ambao wanaweza kutoa fedha ambazo zitasaidia timu kumudu gharama za uendeshaji tofauti na sasa ambapo timu zina hali ngumu kiuchumi kutokana na ligi hiyo kutokuwa na mdhamini.

Ligi Daraja la Kwanza ni jiko la kupika na kuandaa wachezaji ambao watacheza Ligi Kuu hivyo inapokosa ubora na ushindani, tusitegemee kupata wachezaji wazuri na walio fiti na badala yake tutapata ambao hawajapevuka.