MAONI: Kabla hujasambaza taarifa thibitisha ukweli wake

Tuesday October 1 2019

Ujio wa huduma za mitandao ya kijamii umeendelea kuwa moja ya maeneo yenye manufaa makubwa kwa jamii kwa kuwa inarahisisha upashanaji wa taarifa muhimu ndani ya muda mfupi.

Dunia imeendelea kukusanywa na kuwa kama kijiji kimoja ambapo upatikanaji wa habari na usambazaji wa taarifa hususani zilizo muhimu umekuwa ukifanyika kwa haraka, na mara nyingi kwa mafanikio.

Hata hivyo, ukuaji wa matumizi ya mitandao ya kijamii nao umekuja na changamoto zake hususani kutumika katika upotoshaji, kukashifu, wizi kwa njia ya mtandao na nyingine nyingi ambazo zinaendelea kuitesa jamii.

Ipo mifano mingi inayoonyesha ni kwa jinsi gani matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yamekuwa yakiwagharimu wengi kwa namna mbalimbali.

Mfano wa karibu zaidi ni ule wa mkuu wa Wilaya ya Iringa Mjini, Richard Kasesela ambaye juzi, kupitia ukurasa wake wa Twitter, aliutangazia umma kuhusu kifo cha kiongozi mmoja mkubwa nchini, hali iliyoibua sintofahamu katika jamii.

Hali hiyo ilitokana na ukweli kwamba katika siku za karibuni kongozi huyo aliripotiwa kuwa katika matibabu, hivyo mkuu huyo akaamini taarifa za kufariki kwake na kuzisambaza. Lakini baada ya kufuatilia watu wa karibu na kiongozi huyo, walikanusha madai ya kifo chake.

Advertisement

Ingawa baadaye Kasesela aliomba radhi kwa kitendo chake, akisema baada ya kufuatilia amebaini ulikuwa ni uzushi, tayari ilishaamsha hamkani kwa watu wengi ikizingatiwa kuwa mtu aliyedaiwa kufariki ni kiongozi mkubwa katika nchi na aliyefanya kazi kitaifa na kimataifa.

Somo linalopatikana katika mfano huo ambao ni mmoja unaowakilisha mingine mingi, ni kusambaza (forward) taarifa bila ya kuthibitishwa huku anayesambaza naye akiwa hafahamu kwa undani kuhusu jambo husika wala kuwa na uhakika nalo.

Tabia ya kusambaza ujumbe kama unavyoupokea haipaswi kuendelezwa kwani imekuwa ikidhalilisha watu, kuwahukumu, kuzusha taharuki na kuchochea migogoro isiyo ya msingi katika jamii. Jambo hilo linapaswa kukemewa na kila mmoja kwa nafasi yake bila ya kujali ni kiongozi au mwananchi wa kawaida.

Kwa upande wa viongozi, wao wanapaswa kuwa mfano mzuri zaidi kwa wengine kwa kutosambaza taarifa za uzushi ambazo zinaweza kuumiza watu, badala yake wasimame katika nafasi zao za kiuongozi kuhakikisha uzushi wa namna yoyote hausambazwi.

Tunaamini kuwa kilichofanywa na DC Kasesela kusambaza taarifa ile ingawa hakuwa na dhamira mbaya, kimejeruhi mioyo ya wengi.

Aidha, mamlaka zinazosimamia sheria za masuala ya upotoshaji kwa njia ya mitandao nazo zichukue nafasi yao kwa kuhakikisha tatizo hilo linadhibitiwa na haliendelei kuiumiza jamii.

Hatua si tu kukamata, kushtaki au kufunga watu bali utoaji elimu ya kutambua makosa ya namna hiyo linaweza kuwa jambo jema na lenye faida kubwa kwa kuwa litawazindua na kuwajengea watu wengi uelewa juu ya matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii.

Tunashauri suala la utoaji elimu ya kutambua matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii, hususan kwa kutuma na kusambaza taarifa za kweli, litekelezwe kwa ushirikiano wa mamlaka za Serikali na wadau wengine ikiwamo mitandao ya simu ambayo inahusika kwa kiasi kikubwa kutokana na shughuli zao za kila siku.

Tusijenge jamii ya kuamini mambo kwa juu juu ambayo baadaye yanageuka na kusababisha madhara makubwa na majuto kwa jamii.