MAONI: Klabu zisifanye usajili wa majina

Ligi Kuu Tanzania Bara imemalizika na Simba imetwaa ubingwa kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuzipiku timu nyingine 19 zilizoshiriki michuano hiyo msimu uliomalizika.

Wakati Simba ilitwaa ubingwa kwa kufikisha pointi 93, Yanga ilishika nafasi ya pili baada ya kupata pointi 86 ikifuatiwa na Azam iliyoshika nafasi ya tatu kwa pointi 75.

Tangu kuanza ligi hiyo Simba, Yanga na Azam zilikuwa zikipokezana kijiti cha uongozi katika msimamo wa Ligi Kuu iliyoshirikisha timu 20 za Tanzania Bara.

Baada ya kumalizika michuano hiyo, joto la usajili limeanza kwa klabu mbalimbali zilizobaki katika ligi hiyo na zilizopanda, kuanza mkakati wa kutengeneza vikosi vyao kwa ajili ya msimu ujao.

Usajili ni eneo nyeti ambalo ndio msingi wa kupata timu imara itakayoshindana kikamilifu katika ligi hiyo ambayo ndio kubwa zaidi katika ngazi ya klabu nchini.

Kwa klabu zilizopiga hatua kubwa katika mchezo wa soka duniani, usajili ni eneo linalopewa kipaumbele cha kwanza katika kuunda timu imara.

Klabu inapofanya usajili wa uhakika kwa kuzingatia ripoti na mapendekezo ya benchi la ufundi, inakuwa na nafasi nzuri ya kupata kikosi bora cha ushindani.

Katika nchi zilizoendelea, kocha ndiye mwenye mamlaka ya mwisho katika eneo zima la usajili tofauti na klabu zetu za hapa nchini ambako viongozi ndio wanakuwa na mamlaka makubwa.

Kwa kutambua umuhimu wa benchi la ufundi, klabu za Ulaya zimekuwa zikitoa fursa ya moja kwa moja kwa kocha kupendekeza aina ya wachezaji anaowataka, vifaa na mambo mengine ya kiufundi tofauti na klabu zetu za hapa nchini.

Ni vyema klabu zetu zikabadili mfumo wao wa usajili na kutoa nafasi kwa makocha kusajili aina ya wachezaji wanaotaka kutokana na programu zao tofauti na ilivyo sasa.

Tunasema hivi kwa sababu tunatambua kocha ndiye anayejua upungufu wa kikosi chake na changamoto alizokutana nazo katika msimu uliopita.

Endapo kocha atapewa nafasi ya kutoa mependekezo, atakuwa na fursa ya kusajili wachezaji bora, si kwa kufuata matakwa ya viongozi au mashabiki ambao kwao huvutiwa zaidi na majina mkubwa.

Uzoefu unaonyesha kuwa viongozi wengi wa klabu hasa za Ligi Kuu wamekuwa wakiingilia majukumu ya makocha kwa kufanya usajili bila ridhaa yao au benchi la ufundi.

Baadhi ya klabu zimekuwa zikifanya usajili kwa lengo la kushindana au kukomoana na si kupata timu imara ambayo itashiriki ligi ya ndani na michuano ya kimataifa.

Katika kipindi hiki cha usajili, tumeshuhudia baadhi ya wachezaji wakitia saini zaidi ya klabu moja kitendo ambacho ni kinyume cha sheria za soka.

Matukio ya namna hii kwa kiasi kikubwa yamekuwa yakijitokeza mara kwa mara kwasababu idadi kubwa ya viongozi wamekuwa wakifanya kazi za benchi la ufundi ambazo hawana utaalamu nazo.

Ni imani yetu kwamba katika msimu ujao,timu zetu zitajiandaa kikamilifu kwa kusuka vikosi imara vyenye kuleta ushindani uwanjani badala ya kusajili kiujanjaujanja na matokeo yakiwa mabaya zinakimbilia kudai kuonewa.

Tunaamini kwamba makocha wakipewa fursa ya kufanya usajili, watakuwa na wigo mpana wa kutengeneza vikosi imara.