MAONI: Stars inaweza kuishinda Guinea ya Ikweta

Zimebaki siku chache kabla ya timu ya Taifa ya soka, Taifa Stars kucheza na Guinea ya Ikweta katika mechi ya Kundi J ya hatua ya makundi kuwania kufuzu kucheza fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021.

Stars inataka kurudi kwenye fainali hizo kwa mara ya tatu baada ya kushiriki fainali za mwaka 1980 nchini Nigeria na za mwaka jana nchini Misri.

Stars itacheza na Guinea ya Ikweta Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Ijumaa kabla ya kuifuata Libya Novemba 19 na baadaye Tunisia. Mchezo baina ya Taifa Stars na Libya utachezwa Tunisia kutokana na hali tete ya usalama nchini Libya.

Kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije alisema wakati akitangaza kikosi juzi kuwa mechi hizo ni ngumu na aliwataka wachezaji wake kuzingatia nidhamu katika maadalizi yao.

Ndayiragije alisema Guinea ya Ikweta ni timu bora tofauti na mtazamo wa baadhi ya watu wanaodhani ni nyepesi.

Pia alisema mkakati wa kwanza ni kuifunga Guinea ya Ikweta nyumbani matokeo ambayo yatawaweka wachezaji wake katika mazingira mazuri ya kufanya vyema katika mechi zinazofuata.

Kocha huyo alisema katika tathimini aliyofanya timu hiyo ina wachezaji tisa waliotengenezwa katika vituo vya michezo katika klabu za Barcelona, Santander, Malaga na Atletico Madrid za nchini Hispania.

Kwa maana hiyo Guinea inaundwa na idadi kubwa ya wachezaji wenye uzoefu wa kutosha na mashindano ya kimataifa.

Kama alivyosema Ndayiragije, Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo dhidi ya Guinea ili kutengeneza nafasi nzuri kabla ya kukutana na Libya na baadaye Tunisia.

Matarajio ya Watanzania ni kuona Stars ikianza vyema mechi zake za mashindano ili kuwafanya Watanzania kuwa na imani na timu yao na hivyo kuwa nyuma ya timu kila inapocheza.

Katika soka, uzoefu ni moja ya vitu muhimu kwa timu kuweza kufanya vizuri inapokutana na timu ambayo haina uzoefu wa kutosha. Lakini uzoefu si jambo pekee linalotegemewa kwa timu kufanya vizuri.

Wachezaji kupata maandalizi sahihi, kuwa na fikra sahihi wakati wa kuelekea katika mechi, ari ya juu, kujituma na kufuata maelekezo ya mwalimu ni mambo mengine yanayoweza kusaidia timu isiyo na uzoefu kuiangusha timu yenye uzoefu.

Tunaamini hizo ndizo nguvu zetu kubwa tunazozitegemea wakati Stars itakapokutana na Guinea, Tunisia na hata Libya ambayo wachezaji wake wakati wako nje ya nchi wakicheza soka.

Tunaamini nkuwa Ndayiragije na benchi lake la ufundi watafanya kila jitihada kuhakikisha wanaingiza vitu hivyo vichwani mwa wachezaji ili wajiandae kiakili kuvaana na mataifa hayo ya Kaskazini ambayo yamekuwa yakitamba katika soka la barani Afrika, ukiachia Libya ambayo matatizo ya amani yameifanya itetereke.

Pia mashabiki ni kati ya nguzo kubwa za ushindi na ndio maana huhesabiwa kama mchezaji wa 12 uwanjani. Vyama vya soka vya nchi huamua kuzipeleka mechi ngumu kwenye viwanja wanavyotegemea kupata mashabiki wengi ili wawape nguvu zaidi wachezaji.

Tunategemea mashabiki watakaokwenda uwanjani siku za mechi za nyumbani wataonyesha uzalendo kwa kuihamasisha timu kushinda kuanzia mwanzo hadi mwisho na si kusubiri hadi timu ifunge bao ndipo mashabiki washangilie.

Tunaitakia kila la heri Taifa Stars katika mechi ya kwanza dhidi ya Guinea ya Ikweta tukifahamu kuwa ndiyo itakayoweza kusafisha njia ya matokeo mengine. Kila la heri Stars.