MAONI: Kilio hiki katika sekta ya elimu kifike mwisho

Saturday January 19 2019

Msemo wa wahenga kuwa “kila lenye mwanzo lina mwisho” wakati mwingine unaweza kuona kama hautekelezeki. Na inapotokea hivyo kunakuwa na sababu ama zinazoelezwa wazi au zile ambazo wahusika wanaamua kukaa kimya. Utahoji, utauliza, utafuatilia lakini wao wako kimya. Wakiamua wanaibuka na uamuzi wanaoujua wao.

Hali kama hiyo ndiyo inayotaka kuonekana kwenye changamoto zilizopo katika sekta ya elimu, hususan katika eneo la mfumo wa elimu – mitaala, sera na vitabu, mitihani na mambo mengine ya namna hiyo.

Kwa miaka mingi tumesikia malalamiko, ushauri na ukosoaji katika masuala hayo, lakini ni ajabu hadi hii sasa bado tunaelezwa kwamba changamoto ziko palepale.

Kwa mfano, ni muda mrefu tangu tumesikia maoni ya wadau mbalimbali katika makongamano, semina, vyombo vya habari na maeneo rasmi kama Bunge wakizungumzia masuala hayo kwa uzito unaostahili, lakini mara nyingi ama yamekuwa yakipata majibu mepesi au kukosa majibu achilia mbali utekelezaji.

Miongoni mwa watu ambao masuala ya elimu yamekuwa kilio chao muda mrefu ni James Mbatia, mbunge wa Vunjo na mwenyekiti wa NCCR- Mageuzi, ambaye amekuwa akitumia kila fursa anayoipata kuyafafanua na safari hii amedai mfumo wa elimu hapa nchini ni wa kibaguzi na dhaifu ambao hauwezi kushindana kimataifa.

Kwa jinsi anavyobeba ajenda hiyo ni rahisi kupata majibu mepesi au ya jumlajumla, lakini ukweli unabaki palepale kwamba hoja zake zinastahili kupewa majibu yanayojitosheleza na kufanyiwa kazi ili malalamiko haya yafike mwisho.

Mathalani, hoja yake kwamba elimu imegeuka maabara ya majaribio kwa kuwa kila waziri wa elimu anayeteuliwa, huanzisha mambo yake na akiondoka yanabadilishwa inaweza kubishiwa namna gani wakati tunajua kwamba mawaziri wengi wamekuja na mambo yao na wenzao wakayabadili.

Kwa mfano tu, wapo waliofuta michezo shuleni, wengine wakarudisha, waliobadili mfumo wa upangaji matokeo ya mitihani kutoka divisheni kwenda GPA aliyefuata mwingine akarudisha mfumo wa awali.

Hivi nani hajasikia mjadala na hofu kuhusu soko la pamoja katika Jumuiya ya Afrika Mashariki ambalo litaruhusu wakazi wa nchi husika kuajiriwa mahali popote ndani ya eneo hilo. Hii inaungana na hoja ya Mbatia kwamba elimu yetu ina mfumo ambao hautuwezeshi kuingia katika soko la ushindani duniani.

Hata pale anapopambana na vitabu vibovu tunadhani ni muhimu sasa kwa wahusika kuhakikisha vitabu bora vyenye maudhui yanayofaa kwa watoto wa Taifa letu vinachapishwa na kusambazwa kote nchini.

Tunasema hivi tukikumbusha kilio cha wabunge mbalimbali na wadau wengine kuhusu vitabu vyenye thamani ya mabilioni ambavyo viliingia sokoni mwaka 2015, lakini baadaye vikaondolewa baada ya kuonekana vina makosa makubwa na havifai.

Ni kutokana na sababu hiyo tunashauri kwamba vitabu na mitalaa virejeshwe katika mikono ya wataalamu wa elimu ili kupata matokeo yanayokusudiwa.

Basi tukae kama Taifa, turudi kwenye mstari na kutumia fursa iliyopo ya kutengeneza sera mpya ya elimu kusahihisha makosa.

Tuwatumie wadau wazoefu wa elimu, bila kuingiza masilahi ya kisiasa ili kutunga sera mpya itakayobeba elimu yetu kwa miaka mingi inayokuja. Vivyo hivyo tukitoka hapo twende kutazama mitalaa itakayofaa kwa elimu yetu kwa miaka hata 50 ijayo.

Tunaweza kucheza na maeneo mengine, lakini katika suala la elimu hatupaswi kufanya mchezo hata kidogo kwa sababu ndio msingi wa maisha ya binadamu.