MAONI: Mkutano wa Sadc fursa kwa Watanzania

Saturday June 15 2019

 

Agosti 17 na 18, Tanzania itakuwa mwenyeji wa mkutano wa 39 wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc).

Jumla ya marais 16 wa jumuiya hiyo wanatarajiwa kushiriki mkutano huo ambao pamoja na mambo mengineyo utashuhudia Rais John Magufuli akipokea kijiti cha kuwa Mwenyekiti wa jumuiya kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Mara ya mwisho mkutano huo kufanyika nchini ilikuwa mwaka 2003 wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tatu wa Rais Benjamin Mkapa.

Huu ni mkutano wenye uzito wa kipekee kwa kuwaa si tu utahudhuriwa na marais 16 kama tulivyotaja awali, lakini zaidi ya wageni 1,000 wanatarajiwa kuambatana na marais hao katika mkutano huo utakaofanyika jijini Dar es Salaam.

Upekee wa mkutano huu ndio unaotusukuma kuwasihi Watanzania kuutumia kama fursa adhimu ya kiuchumi na kichocheo cha kuongezeka mshikamano wa kibiashara katika ukanda huo.

Kama alivyosema Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi kuwa mkutano huu unaweza kuwa fursa nzuri kwa wajasiriamali nchini wakiwamo wamiliki wa hoteli, wafanyabiashara wa vyakula, usafiri na wengineo kujitokeza na kutumia nafasi hiyo kujitangaza.

Advertisement

Kwa wamiliki wa hoteli na wafanyabiashara katika sekta ya usafiri, hii inaweza kuwa fursa ya kupata kipato kwa muda wa siku chache kabla na pengine baada ya mkutano, lakini kwa wafanyabiashara ambao ni wawekezaji, ujio wa wageni hawa ni nafasi nzuri kwao kujenga uhusiano wa kibiashara ili hatimaye wafikirie kuwekeza nje ya nchi.

Mpaka sasa ni wafanyabiashara wachache mno wa Tanzania waliofanikiwa kupenya nje ya mipaka ya nchi na kuwekeza hasa upande wa sekta muhimu kama vile viwanda, mabenki na nyinginezo.

Nchi hizi ni fursa nzuri kwa uwekezaji, hivyo ni wakati wa wafanyabiashara wa Tanzania kuchangamka sio tu kwa maslahi yao binafsi lakini hata nchi kwa jumla.

Kiserikali mkutano huu usichukuliwe tu kama jukwaa lenye mtazamo wa kisiasa. Hii ni fursa nzuri kwa taasisi za Serikali kama vile Wizara ya Viwanda na Biashara, Kituo cha Uwekezaji (TIC), Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tan Trade) na nyinginezo.

Ujio wa wageni hao uwe chachu ya kutangaza vivutio vya uwekezaji vilivyopo nchini. Lakini kikubwa zaidi ni vyombo hivyo kuona namna ya kujenga uhusiano na mitandao ya kibiashara kwa ajili ya kutafuta masoko ya bidhaa za Tanzania.

Tukiwa ni nchi ambayo dira yake ya maendeleo ni kuwa na uchumi wa kati unaochagizwa na maendeleo ya viwanda, huu ni wakati wa Tanzania kuzitumia nchi za Sadc na hatimaye kuwekeza katika sekta zote kuanzia mawasiliano, utalii, biashara, madini, usafiri wa ndege, benki, lugha na nyinginezo.

Tunapozitazama nchi zote za jumuiya hii, Tanzania ina nafasi kubwa ya kunufaika kiuchumi hasa kutokana na wingi wa rasilimali ilizonazo, utulivu wetu wa kisiasa na uimara wa Serikali yetu.

Tutumie mambo haya kama kichocheo cha kuipaisha nchi kiuchumi katika ukanda wa nchi za Sadc.