MAONI: Wachezaji Taifa Stars waonyeshe ubora uleule

Monday March 9 2020

Wakati timu kongwe za Yanga na Simba jana zilivaana katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara, timu ya Taifa, ‘Taifa Stars’ inatarajiwa kutangazwa muda mfupi ujao.

Taifa Stars inatarajiwa kuanza kambi Machi 12 kujiandaa kwa mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) dhidi ya Tunisia.

Timu hiyo itaanzia ugenini Machi 27 kabla ya kurudiana Dar es Salaam Machi 30. Baada ya mechi hizo Taifa Stars itakuwa na kibarua kingine katika mashindano ya CHAN.

CHAN ni mashindano ya soka ya Afrika yanayoshirikisha wachezaji wanaocheza ligi za ndani na Tanzania imepangwa Kundi D na timu za Zambia, Guinea na Namibia.

Mashindano ya CHAN yamepangwa kuanza Aprili 4 nchini Cameroon. Tanzania itaanza kutupa karata yake Aprili 8 dhidi ya Zambia.

Muda uliobaki kabla ya Taifa Stars kucheza mechi zake ni mfupi hivyo timu hiyo inatakiwa kufanya maandalizi ya kutosha kutokana na rekodi nzuri ya timu wapinzani wake katika mashindano ya kimataifa.

Advertisement

Mchezo ulioko jirani ni dhidi ya Tunisia ambao Taifa Stars inatakiwa kushinda ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kusonga mbele katika mechi ya marudiano.

Timu hizo zitacheza mechi mbili ndani ya siku nne jambo ambalo linahitaji wachezaji wenye viwango bora vya kushindana.

Tunaamini kocha Etienne Ndayiragije atatangaza kikosi imara ambacho kitaundwa na wachezaji wenye viwango bora waliofanya vyema katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Lipo kundi kubwa la wachezaji ambalo limeonyesha kiwango bora na kuanza kuzivutia klabu za Simba na Yanga ambazo zina kawaida ya kusajili wachezaji waliong’ara katika mashindano hayo katika msimu husika.

Bila shaka Ndayiragije ameona idadi ya kutosha ya wachezaji waliofanya vizuri baada ya kupata muda wa kutembelea katika mikoa mbalimbali kusaka vipaji.

Tunatoa rai kwa wachezaji ambao wataitwa kujiunga na Taifa Stars watimize wajibu wao kwa kuitendea haki nafasi ya kuitwa katika kikosi hicho.

Uwezo ambao walionyesha katika ligi ni vyema wakauonyesha pia katika mechi za mashindano ya kimataifa kwa kuanzia na ile dhidi ya Tunisia.

Ni vyema wakaona fahari kuitwa timu ya Taifa, hivyo wana wajibu wa kucheza kwa ufanisi kwa kuwa wapo wachezaji wengi waliokuwa na shauku ya kutaka kuitumia timu hiyo, lakini hawakupata fursa hiyo.

Pia watambue kuitwa timu ya Taifa ni heshima kwao na hilo liko bayana na tumekuwa tukishuhudia jinsi wachezaji wa Ulaya wakipambana kupata namba kikosi cha kwanza katika klabu zao ili wapate fursa ya kuitwa timu zao za taifa.

Tumekuwa tukishuhudia idadi kubwa ya washambuliaji wasiokuwa na majina makubwa katika soka nchini wakichuana na nyota wa Simba, Meddie Kagere kuwania tuzo ya mfungaji bora.

Tangu kuanza msimu huu wachezaji hao wamekuwa moto kwa kucheza kwa kiwango bora hatua ambayo imenogesha ushindani wa kuwania kiatu cha dhahabu.

Tunaamini Ndayiragije atatoa nafasi kwa vijana kwa lengo la kuwajengea uwezo wa kujiamini.